Mwenyekiti wa Mtandao wa Afya na Elimu wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki Bibi Kokushubila Kairuk alisema kitendo cha baadhi ya Viongozi na washirika wa maendeleo kuendelea kuunga mkono Taasisi za Umma na zile binafsi huleta faraja katika Jamii.
Bibi Kokushubila alieleza hayo wakati akipokea msaada wa vifaa vya michezo vilivyotolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Mtaa wa Mikocheni Mjini Dar es salaam.
Vifaa hivyo vikiwa ni pamoja na Seti ya Jezi, Mipira ya kandanda na Vikapu, soksi, Bukta pamoja na sare za mlinda Mlango kwa ajili ya Timu ya Chuo Kikuu hicho viliwasilishwa Chuoni hapo na Daktari wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Dr.Juma Mbwana Mambi kwa niaba yake vikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi Milioni Moja.
Bibi Kokushubila alisema michezo ni moja ya eneo linalounganisha jamii hasa Vijana ambayo linahitaji kupewa msukumo kwa vile huchangamsha Vinjana hao Kiakili na kimawazo.
Mwenyekiti huyo wa Mtandao wa Afya na Elimu wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki alimpongeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwa msaada wake huo ambao umeleta faraja kwa Wanafunzi sambamba na Uongozi wa Chuo hicho.
Bibi Kokushubila alisisitiza umuhimu wa kuendelezwa kwa ushirikiano baina ya Taasisi husika na washirika wa sekta ya Michezo ili kuona fani hiyo inapata nguvu zaidi kwa vile tayari imeshaonyesha muelekeo wa kutoa ajira kwa kundi kubwa la Vijana.
Mapema akiwasilisha msaada huo wa Vifaa vya Michezo Dr. Juma Mbwana Mambi kwa Niaba ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Mh. Balozi Seif aliahidi kuendelea kusaidia sekta ya michezo kutokana na umuhimu wake kwa hivi sasa.
Dr. Mambi alisema juhudi zitaendelea kuchukuliwa na Mh. Balozi ili kuona michezo Nchini inadumishwa na kuendelezwa zaidi kwa faida na ustawi wa Jamii yote.
Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki kiliopo Mikocheni Mjini Dar es salaam mbali ya kutoa Taaluma ya Elimu ya Afya pia kinadumisha michezo kwa nia ya kuwajenga afya wanafunzi na walimu wake.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment