Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali alisema kwamba kizazi kipya kinapaswa kuelewa azma ya waasisi wa Taifa la Tanzania Marehemu Mzee Abeid Aman Karume na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wakati walipokuwa mstari wa mbele kudai Uhuru na haki za jamii ya Watu wote.
Alisema watoto waliowengi wa kizazi kipya bado wanaendelea kuwa njia panda wakikosa kumbu kumbu kadhaa za Viongozi waasisi ambazo zingewapa fursa na nafasi pana ya kuelewa malengo sahihi ya waasisi hao.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akizungumza na Wajumbe wa Bodi ya Udhamini wa Mfuko wa kuwaenzi Waasisi wa Taifa la Tanzania ulioongozwa na Mwenyeki wake Kanal Mstaafu Kabenga Nsa Kaisi aliokutana nao Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Alisema yapo mataifa mengi duniani kama Vietnam, Jamuhuri ya Watu wa China na Korea ya Kaskazini yenye Historia kubwa ya kuenzi kazi na kumbu kumbu za waasisi wao kitendo ambacho Bodi hiyo itastahiki kuiga mfano huo.
Balozi Seif alifahamisha kwamba wapo baadhi ya watu wanaoendelea kuzidhihaki kazi zilizofanywa na waasisi wa Tanzania kiasi kwamba iwapo hakutakuwa na juhudi za makusudi kizazi kipya kinaweza kupotea na kukosa Historia yao.
Alitolea mfano wa Mapinduzi Daima yanayodhihakiwa na baadhi ya watu hao wakikosa kuelewa dhamiri halisi inayokusudiwa ya kuyaenzi yale yote yaliyotangazwa mara baada ya Mapinduzi ya Mwaka 1964 ambayo yatamstawisha Mwananchi wa Taifa hili katika maisha yake yote.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwahakikisha Wajumbe wa Bodi ya Udhamini wa Mfuko wa Kuwaenzi Waasisi wa Tanzania kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatoa kila aina msaada utakaohitajika na Wajumbe hao ili kuona malengo waliyojipangia yanafanikiwa vyema.
Aliwashauri wajumbe wa Bodi hiyo kuwasiliana na wazee wanaoielewa vyema Historia ya Uhuru wa Tanganyika na Mapinduzi ya Zanzibar ili iendelee kuenziwa na kizazi kipya.
Alieleza kwamba Kizazi kipya ni vizuri kikajengewa mazingira bora ya kujifunza moyo wa kujitolea kupitia waasisi wa Taifa la Tanzania ambalo linaendelea kuwa chuo kwa baadhi ya Nchi washirika kupata Taaluma ya Historia yake.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alielezea faraja yake kutokana na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kuona umuhimu wa kupitisha Sheria ndani ya Bunge 2004 ya kuunda bodi ya Udhamini wa Mfuko wa kuwaenzi waasisi wa Taifa la Tanzania.
Mapema Mwenyekiti wa Bodi hiyo Kanal Mstaafu Kabenga Nsa Kaisi alisema jukumu kubwa la Bodi hiyo ni kukusanya kumbu kumbu za waasisi Taifa la Tanzania na kuzihifadhi kwa faida ya vizazi vipya.
Kanal Mstaafu Kabenga alisema bodi tayari imeshaandaa mikakati ya jinsi ya kupata uwezo wa kifedha zitakazokidhi uanzishwaji wa vituo viwili vya Kumbu kumbu vitakavyowekwa Tanzania bara na Zanzibar.
Alifahamisha kwamba Wajumbe wa Bodi hiyo watasimamia kuonba kwamba mchango wa Viongozi waasisi haufanyiwi dhihaka na kazi kubwa ya wajumbe hao ni kusimamia taaluma ili Jamii ifahamu azma hya waasisi hao katika kupigania Uhuru na haki za Mwafrika.
“ Kazi yetu inayofanana na wenzetu inatupa faraja kuona Mtaifa ya Dunia hii yanaendelea kuwaenzi waasisi wa Nchi zao.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment