Viongozi wa ngazi mbali mbali wa Chama cha Mapinduzi leo wamehudhuria hitma ya kumuombea Dua Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni Marehemu Salmin Awadh Salmin.

Hitma hiyo iliyoandaliwa na Kamati ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Chama cha Mapinduzi wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi imefanyika katika ukumbi wa Afisi Kuu ya CCM Kisiwwandui Mjini Zanzibar.

Akitoa kumbusho la wajibu wa kifo kwa kila nafsi kwenye Hitma hiyo Naibu Katibu wa Mufti Kuu wa Zanzibar Sheikh Nauman Jongo alisema kifo ni mtihani mzito ambao kiumbe amewekewa pazia la kutojua kitamfika lini.

Sheikh Jongo alisema kwamba mtihani huo ni somo linalotoa ukumbusho kwa kila mja kuelewa kuwa iko siku ataacha watoto, mali na kila alichokuwa akikipenda ndani ya nafsi yake.

“ Kifo ni mtihani mzito ambao kiumbe kamwe haelewi lini kitamfika kwamba anaweza akajiandaa “. Alisema Sheikh Nauman Jongo.

Alifahamisha kwamba waumini kwa mujibu wa muongozo wa Dini wanatakiwa kuwa na huzuni wakati mmoja kati yao yanapomfika mauti wakijikumbusha kuwa Marehemu mwnezao amekwenda safari ndefu ya milele.

Akitoa shukrani kwa washiriki wa Hitma hiyo Mjumbe wa Kamati ya Wawakilishi wa CCM Mh. Hamza Hassan Juma aliwaomba wana CCM wote kuendelea kutoa ushirikiano wakati wanapopatwa na mitihani hasa vifo.

Mh. Hamza alisema utaratibu huo ambao umezoeleka kwa wanachama wengi katika sehemu tofauti Nchini unaleta faraja na upendo miongoni mwa wanachama wenyewe.

Wakati huo huo Wajumbe wa Kamati ya wawakilishi wa CCM walitoa mkono wa pole kwa fanilia ya Marehemu Salmin Awadhi Salin wakitekeleza utaratibu waliojipangia wakati inapotokea msiba baina ya wana Kamati hao.

Akiiongoza Kamati hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikabidhi ubani kwa familia hiyo hapo Nymbani kwa Marehemu Mtaa wa Mzalendo Magomeni Mjini Zanzibar.

Ubani huu tunaootoa ni utamaduni tuliojiwekea katika Kamati yetu ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Chama cha Mapinduzi “ Alisema Balozi Seif.

Balozi Seif aliendelea kuwaomba ndugu na jamaa wa marehemu Salin wawe na moyo wa subira hasa kip[indi hichi kifupi cha kuondokewa na mpendwa wao waliomzoea.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top