Wananchi saba kati ya kumi (69%) wanasema rushwa zilizoripotiwa kwenye ripoti ya mwaka ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ni upotevu wa fedha zao (za umma). Zaidi ya nusu ya wananchi (55%) wanaamini kuwa aina hii ya rushwa inagusa sana maisha ya yao ya kila siku, na watatu kati ya kumi (31%) wangependa kutaarifiwa kuhusu matokeo ya ukaguzi kupitia vipindi vya redio vinavyorushwa kila wiki kwa muda wa nusu saa.
Wananchi pia wanaamini kuwa Rais anapaswa kuchukua hatua juu ya matokeo ya ripoti ya CAG: Takriban wananchi sita kati ya kumi (57%) wanaamini kuwa Rais anawajibu wa kufuatilia masuala ya ukaguzi wa hesabu za serikali. Taasisi nyingine zinazotajwa kuwa na wajibu wa kufanya hivyo ni pamoja na Baraza la Mawaziri (16%) na mahakama (11%). Mbali na Rais, hakuna taasisi au mtu binafsi aliyetajwa na wananchi kwa zaidi ya 20% kuwa anawajibu wa kushughulikia masuala ya ukaguzi wa hesabu za serikali.
Matokeo haya yametolewa na Twaweza kwenye muhtasari mfupi wenye jina la Walezi wa Uwajibikaji: Ufahamu na maoni ya wananchi kuhusu taasisi za usimamizi. Muhtasari huu umetokana na takwimu kutoka utafiti wa Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaofanyika mara kwa mara kwa njia ya simu za mkononi. Matokeo yametokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,474 katika maeneo mbalimbali Tanzania Bara (Zanzibar haimo kwenye matokeo haya) kati ya miezi ya Septemba na Oktoba 2014.
Licha ya kuwepo kwa taarifa za wazi juu ya makosa ya rushwa na haja ya Rais kuchukua hatua, wananchi wana hisia kinzani linapokuja suala la adhabu kwa viongozi wenye matumizi mabaya ya fedha za umma. Mwananchi mmoja tu kati ya ishirini (6%) anafikiri kuwa wale wanaopatikana na hatia ya rushwa wanapaswa kuondolewa katika ofisi za umma, na ni mmoja tu kati ya wananchi sita (15%) anayefikiri kuwa wala rushwa wanapaswa kufungwa. Adhabu sahihi kwa wala rushwa iliyotajwa na wananchi wengi (32%) ni kufukuzwa kazi, kunyang’anywa pensheni, kunyang’anywa mafao na kulipa pesa walizofuja (30%).
Wananchi waliulizwa pia kuhusu ufahamu wao kuhusu taasisi kuu tatu za usimamizi wa fedha. Hizi hushiriki katika mchakato wa kuandaa na baadaye kufuatilia ripoti ya mwaka ya ukaguzi wa fedha nchini Tanzania; Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu (NAOT), Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu ilionekana kujulikana zaidi kuliko taasisi nyingine kati ya hizi tatu. Mwananchi mmoja kati ya watatu (34%) ameshawahi kumsikia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na mmoja kati ya sita (16%) anaweza kuelezea kwa usahihi kazi zake. Kwa kamati za bunge zenye wajibu wa usimamizi wa hesabu za serikali kuu na hesabu za serikali za mitaa, takwimu ziko chini zaidi. Wananchi watatu kati ya kumi (29%) wamewahi kusikia kuhusu PAC na zaidi ya mmoja kati ya kumi (13%) anaweza kueleza kazi zake kwa usahihi, wakati mwananchi mmoja tu kati ya wanne (26%) ameshawahi kuisikia kuhusu LAAC na mmoja kati ya kumi (11%) anaweza kueleza kazi za kamati hii.
Kwa taasisi zote tatu, wananchi wana wasiwasi juu ya uwezo wa taasisi hizi kufanya kazi bila kuingiliwa, na pia hawana uhakika na mafanikio ya taasisi hizi. Chini ya mwananchi mmoja kati ya wanne anaamini taasisi hizi za usimamizi zina uhuru wa kufanya kazi zao: kuhusu CAG (25% wanaamini ana uhuru kamili), LAAC (21%) na PAC (23%) wanaamini hivyo. Hakuna mwananchi aliyeweza kutaja mafanikio yoyote halisi ya taasisi hizi tatu. Kwa mfano, chini ya 5% ya wananchi walidhani kuwa moja ya taasisi hizi imewahi kugundua kashfa za rushwa au kuwaweka hadharani viongozi wa umma wala rushwa ndani ya kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Wananchi wengi pia wana uhakika kuwa kuna aina nyingi za rushwa ndani ya serikali, lakini wana wasiwasi kama rushwa hizi zitatajwa kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Wananchi tisa kati ya kumi (88%) wanafikiri kuwa rushwa hutolewa ili kupata cheo serikalini au kushinda zabuni, wakati zaidi ya wananchi watatu kati ya kumi (34%) wanafikiri kuwa kesi hizi za rushwa zitaandikwa kwenye ripoti ya CAG.
Elvis Mushi, Mtafiti Mkuu wa Sauti za Wananchi alitoa maoni juu ya matokeo haya na kusema "Ni dhahri wananchi wanaathirika na rushwa na wana imani ndogo na taasisi muhimu za usimamizi wa fedha kuweza kushughulikia madai yao. Hili linaeleweka ukizingatia kuwa rushwa kubwa serikalini imeibuliwa mara kwa mara lakini inaonekana haishughulikiwi ipasavyo kuzuia vitendo hivi visitokee tena. Sehemu ya tatizo ni kwamba taasisi zetu za uwajibikaji hazina meno halisi ambayo yangeweza kutumika kutoa adhabu kali kwa wanaopatikana kujihusisha na vitendo vya rushwa."
"Wakati huo huo," aliendelea kusema "wananchi hawatetei kuwepo kwa adhabu kali dhidi ya wale wanaotumia vibaya fedha za umma. Tunakosa muunganiko kati ya matamanio yetu ya kupunguza rushwa na kuongeza uwajibikaji, na kutokuwa tayari kutumia adhabu kali kufikia malengo hayo. Kinachotakiwa ni uongozi imara katika ngazi zote kuhakikisha kuwa mifumo ya uwajibikaji inafanya kazi kwa ufanisi, na kuelimisha umma kwa ujumla na wale walio madarakani juu ya taratibu na njia za kushinikiza uwajibikaji.”
0 comments:
Post a Comment