Mambo na kazi kubwa inayoendelea kufanywa na Chama cha Mapinduzi katika kusimamia utekelezaji wa Ilani na Sera zake ndani ya Serikali zote mbili inapaswa kuelezwa na hatimae ifahamike vyema kwa wananchi pamoja na jamii yote hapa Nchini.
Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi alieleza hayo katika hafla fupi ya kukabidhi msaada wa vifaa vya Ofisi akitekeleza ahadi aliyoupa Uongozi wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Wilaya ya Mjini hapo ofisini kwao Miti ulaya Mjini Zanzibar.
Vifaa hivyo ambavyo ni Kompyuta moja, Printa yake pamoja na Mashine ya Foto kopi vitasaidia pia Jumuiya nyengine za CCM Ofisini hapo vikiwa na thamani ya shilingi za Kitanzania Milioni Tatu na Laki Tano { 3500,000/- }.
Mama Asha akiwa pia na wadhifa wa Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Kaskazini “ B “ alisema wananchi wataelewa kazi hiyo kubwa iwapo Viongozi wa CCM Ngazi mbali mbali watafanya juhudi za makusudi katika kuyaeleza mafanikio hayo kwa Wananchi.
Alisema tabia ya kusubiri Viongozi wa ngazi ya juu kuyaeleza mafanikio hayo na wale wengine wa ngazi za kati wakijibweteka ni ya hatari na inaweza kudhoofisha nguvu za Chama hicho.
Alifahamisha kwamba wananchi walio wengi ndani ya Taifa hili wana imani na matarajio ya kukiona chama cha Mapinduzi kinaendelea kuiongoza Tanzania kwa vile sera na ilani yake ndio iliyopata ridhaa ya Umma.
“ Tunataka kuona Chama cha Mapinduzi kinaendelea kuongoza Taifa hili katika muda wote “. Alisema Mama Asha.
Alieleza kwamba kazi za Chama hutekelezwa na wanachama wote wakisimamiwa na viongozi wao wa ngazi zote.
Mama Asha aliwafahamisha Viongozi hao wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa na Wilaya ya Mjini kwamba muda wote atakuwa tayari kushirikiana nao katika kuona utekelezaji wa ilani ya CCM na Sera zake unafanikiwa ipasavyo.
Alisema wakati umefika kwa viongozi na wanachama wote wa Chama hicho kuwadharau watu na hata wale viongozi wa upinzani wenye tabia ya kukejeli maendeleo yaliyofanywa na CCM ambayo yako wazi.
Akitoa shukrani kwa niaba ya viongozi wenzake Mwenyekiti wa Jumuiya Wazazi Mkoa wa Mjini Ndugu Ali Othman Said alimpongeza Mama Asha kwa jitihada zake za kusaidia jamii katika maeneo mbali mbali hapa Nchini.
Nd. Othman alisema jitihada hizo zimekuwa zikishuhudiwa na wananchi bila ya kujali itikadi za kisiasa, Kidini na hata kijinsia.
Akimuhakikishia Mama Asha utumiaji sahihi wa vifaa hivyo Mwenyekiti huyo wa Wazazi Mkoa Mjini alisema Chama Wazazi Wilaya na hata mkoa kimepata nguvu za utekelezaji mzuri wa majukumu yake kutokana na msaada huo.
Alielezea faraja yake na kusema kwamba vifaa hivyo kwa kiasi kikubwa vitapunguza matumizi makubwa ya fedha za Jumuiya hiyo ambapo kazi zake nyingi zilikuwa zikifanywa kwa malipo katika maeneo ya nje jambo ambalo lilikuwa likiondosha usiri wa kazi za Jumuiya hiyo.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment