Kampuni ya Kimataifa ya usafiri wa anga ya Flydubai inatarajiwa kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja baina ya Dubai na Zanzibar kati kati ya wiki hii kwa lengo la kushirikiana na Zanzibar katika kukuza uchumi kupitia sekta za biashara na utalii.
Mratibu wa Kampuni hiyo Bwana Riyaz Jamal akiuongoza ujumbe wa Viongozi watatu wa Kampuni hiyo alisema hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Bwana Jamal alimueleza Balozi Seif kwamba safari hizo zinazotarajiwa kuzinduliwa rasmi jumatano ya wiki hii zitaihusisha ndege kubwa aina ya Boyeing itakayokuwa na uwezo wa kuchukuwa abiria 231 kwa wakati mmoja.
Alisema Ndege hiyo itaanzia na safari zake mara mbili kwa wiki ikilenga kutoa huduma kila siku hapo baadaye kulingana na mahitaji na uwezo wa abiria ndani ya Zanzibar pamoja na Dar es salaam.
Mratibu huyo wa Flydubai alifahamisha kwamba Uongozi wa Kampuni hiyo unakusudia kuona soko la ajira kwa Watanzania walio wengi linaongezeka Mjini Dubai.
Bwana Jamal alieleza kuwa Watanzania wanaofanya kazi Mjini Dubai kwenye makapuni mbali mbali ya biashara yakiwemo yale yanayotoa huduma za usafiri wa anga wamefikia 600 tu ikilinganishwa na idadi ya Wakenya inayokadiriwa kufikia Laki 600,000.
Aliongeza kwamba Kampuni ya Kimataifa ya Flydubai iko tayari kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuanzisha pia miradi mikubwa ya huduma za biashara katika viwanja vya ndege {duty free }.
Alisema Kampuni hiyo ambayo ni mshirika mkuu wa shirika la ndege la Kimataifa la Gulf Air imekuwa na uwezo na taaluma ya kutosha katika kutoa huduma hizo sehemu mbali mbali Duniani.
“ Tumeshuhudia mabadiliko makubwa ya matengenezo ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar ambayo kampuni yetu inaweza kutoa huduma hizo endapo itapatiwa fursa hiyo “. Alisema Bwana Riyaz Jamal.
Naye kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema wazo la Kampuni hiyo ya Flydubai lina muelekeo wa kusaidia kupunguza usumbufu wa abiria wa Zanzibar wanaohitaji safari za moja kwa moja za Mashariki ya Kati.
Balozi Seif aliipongeza Kampuni hiyo kwa uwamuzi wake wa kuwekeza katika sekta ya usafiri wa anga jambo ambalo litaongeza kasi ya uchumi na mapato ya Taifa sambamba na kutoa fursa za ajira.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliueleza Uongozi wa Kampuni ya Flydubai kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaangalia mpango wa muda mrefu wa kuimarisha sekta ya utalii.
Alisema Sekta hiyo hivi sasa imepanuka zaidi kiasi kwamba Taifa linaitegemea mno katika kuongeza mapato yake ikisaidia zao kuu la uchumi Karafuu liliopo hivi sasa.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment