Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Taifa la Tanzania hivi sasa linahitaji kuendelea kuwa na hali nzuri ya amani kuliko wakati mwengine wowote kutokana na kwamba linapita katika kipindi cha kuundwa kwa Katiba mpya.

Balozi Seif alieleza hayo wakati wa hafla fupi ya kuweka jiwe la Msingi la Msikiti Mkuu wa Ijumaa wa Kijiji cha Peramiho uitwao Masjid Jidah akiwa katika ziara ya siku mbili Mkoani Ruvuma kukagua shughuli za maendeleo, kiuchumi pamoja na ustawi wa jamii.

Alisema zipo dalili za wazi zinazoonyesha baadhi ya watu, viongozi na hata makundi ya kijamii na kidini zinaanza kujikita katika kuichezea amani ya nchi jambo ambalo ni hatari kwa hatma ya wananchi.

Balozi Seif alisema kwamba Kizazi cha sasa na kile kijacho kinahitaji kutengenezewa mazingira mazuri ya mfumo wa maisha yao ili kiepukane na wimbi la migogoro inayoonekana kuyakumba mataifa mbali mbali duniani.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaasa waumini hao wa Dini ya Kiislamu wa Peramiho kuendelea kushikamana kama dini yao inavyosisitiza suala la kutunza amani, utulivu na kuvumiliana baina yao na wale wa imani nyengine.

Alisema wapo baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu wanaopenda kuleta mtafaruku ndani ya maeneo ya dini vitendo ambavyo havina tija na ni lazima viepukwe kwa hali yoyote ile.

“ Tumeshuhudia mfano wa ushirikiano ulioonyeshwa hivi karibuni na makundi ya dini na madhehebu mbali mbali yalipoamua kucheza mechi ya kirafiki iliyozikutanisha timu za amani na Mshikamano katika dhana ya kudumisha umoja jambo ambalo sisi tulio nyuma yao tunapaswa kuliiga “. Alisema Balozi Seif.

Alisisitiza kwamba waumini na hata wananchi wote nchini wanapaswa kujifunza matokeo ya kutetereka kwa amani yaliyotokea katika nchi tofauti ulimwenguni ambazo hivi sasa hali ya maisha ya wanawake na watoto yamekuwa hatarini.

Alifahamisha kwamba nchi hizo hivi sasa hazikaliki kutokana na kuichezea amani yao hali inayopelekea hata shughuli za kiuchumi na maendeleo kushindwa kutekelezeka.

Akitoa taarifa fupi ya ujenzi wa Msikiti huo wa Ijumaa wa Kijiji cha Paremiho mjumbe wa kamati ya Masjid Jidah Sheikh Ali Namawela alisema tathmini ya ujenzi wa msikiti huo inakisiwa kugharimu shilingi za Kitanzania Milioni Sitini { 60,000,000/- } hadi kukamilika kwa msikiti huo.

Sheikh Ali alisema kuyumba kwa ujenzi wa msikiti huo kunatokana na wachangiaji wengi wa msikiti huo kuchelewa kupata malipo ya fedha zao kutokana na mauzo ya mazao yao ya kilimo.

Mjumbe huyo wa Kamati ya Uongozi wa Msiki huo alifahamisha kwamba hadi sasa ujenzi unaoendelea wa hatua ya msingi umeshafikia gharama ya shilingi milioni Kumi.

Katika kuunga mkono juhudi za waumini hao wa dini ya Kiislamu Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alichangia shilingi Milioni 1,500,000/- ili kuendeleza harakati za ujenzi huo.

Balozi Seif pia akaahidi kuchangia matofali elfu 10,000 kuendeleza ujenzi huo pamoja na kuahidi kuchangia mabati itakapofikia hatua ya uwezekaji ili kutoa fursa na nafasi nzuri kwa waumini hao kufanya ibada zao katika mazingira mazuri.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top