Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Alhajj Maalim Seif`Sharif Hamad, amewasisitiza wazazi na walezi kubadilika ili kuwapatia watoto wao elimu ya dini na dunia bila ya ubaguzi.

Akifungua Ijtimai ya siku tatu katika kisiwa cha Fundo Wilaya ya Wete Pemba, Alhajj Maalim Seif amesema amri ya kutafuta elimu imekuja kwa watu wote bila ya kubagua jinsia.

Makamu wa Kwanza wa Rais amefahamisha kuwa bado wazazi wamekuwa wakiwapa majukumu mazito ya kifamilia watoto wa kike, hali ambayo imekuwa ikiwakosesha elimu inayostahiki tofauti na ilivyo kwa watoto wa kiume.

Amesema kabla ya kuwapa majukumu hayo ni vyema kuwajengea misingi imara ya elimu ili iweze kuwasaidia katika maisha yao ya baadaye.

Aidha Maalim Seif amehimiza umuhimu wa kulinda maadili, mila na desturi za Zanzibar, ili kujikinga na vitendo viovu vikiwemo, matumizi ya dawa za kulenya na maambukizi ya virusi vya Ukimwi.

Akizungumzia kuhusu Utalii, Maalim Seif amesema Serikali haina nia ya kuilazimisha sehemu yoyote kukubali Utalii, bali imekuwa ikiwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa sekta hiyo kwa maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.

Amesema sio kila utalii unaharibu maadili ya jamii, isipokuwa kitu cha msingi ni kudhibiti utalii wenyewe ili uendane na mazingira halisi ya eneo husika.

Amesema ziko nchi nyingi za kiislamu zinazofanya biashara ya Utalii zikiwemo Malaysia na Uturuki bila ya kuathiti utamaduni wao, na hivyo kukuza uchumi wao na kuongeza kipato cha wananchi.

Amesema ikiwa Zanzibar itajikita kuenzi utamaduni, mila na silka zao, watalii wa kiwango cha juu wanaweza kuvutika na kuja kufanya utalii wa kiutamaduni.

Amekiri kuwa Serikali ilifanya makosa wakati wa kuanzisha utalii kwa kutozingatia hadhi ya watalii wanaoingia nchini, na kwamba sasa imejipanga kuchukua watalii wenye viwango vya kimataifa watakaoweza kushirikiana na kuleta tija kwa jamii.

Amesema Serikali ina dhamira ya kweli ya kuendeleza dhana ya utalii kwa wote, na kwamba itafikiwa ikiwa wananchi watakubali kuifanyia kazi.

Amewapongeza wakaazi wa visiwa vya Fundo na Uvinje kwa kuanzisha Umoja wa waislamu wenye lengo la kusogeza mbele maendeleo ya dini ya Kiislamu.

Mapema akisoma risala ya Ijtimai hiyo, ustadh Suleiman Khamis Mbwana amesema Ijtimai hiyo inayofanyika kila baada ya miaka miwili, imekuwa chachu ya kutoa na kupokea elimu kwa waislamu mbali mbali.

Amesema katika kuendeleza harakati za Ijtimai hiyo wanakusudia kujenga msikiti mkubwa katika eneo hilo, skuli ya maandalizi pamoja na madarasa ya watu wazima, ili kuweza kuimarisha maadili ya kiislamu.

Wameiomba serikali pamoja na wafadhili kuchangia ujenzi huo ili uweze kukamilika na kuanza kazi ya kutoa taaluma.

Hassan Hamad, OMKR

0 comments:

 
Top