Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imetakiwa kuweka program maalum wa mafunzo kwa walimu wanaotaka kujiendeleza katika vyuo mbali mbali vya elimu nchini.

Wito huo umetolewa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad katika skuli ya Chasasa Wete, wakati akitoa majumuisho ya ziara yake ya siku mbili kwa taasisi za elimu Kisiwani Pemba.

Amesema bila ya kuwepo program hiyo, suala la kujiendeleza kwa walimu litaendelea kuwa gumu, na badala yake walimu wachache wenye uwezo na uwenyeji ndani ya serikali, ndio watakaoendelea kunufaika na masomo hayo ya Ualimu.

Amesema program hiyo pia itasaida kuwadhibiti walimu kwenda masomoni kwa wakati mmoja, na kuziacha skuli ziliwa na upungufu mkubwa wa walimu, hali inayochangia kupatikana kwa matokeo mabaya ya wanafunzi katika mitihani ya Taifa.

Kuhusu maslahi ya walimu, Maalim Seif amesema serikali inatambua matatizo yanayowakabili walimu ikiwa ni pamoja na mazingira magumu ya kazi pamoja na maslahi duni, lakini inaendelea kuchukua hatua kuona kuwa wanajengewa mazingira bora na maslahi yanayoridhisha.

Amesema katika kufikia hatua hiyo, tayari Wizara ya Elimu imeshakamilisha mpango wake wa utumishi “Scheme of Service” na kukabidhiwa rasmi kwa Wizara ya Utumishi wa Umma, ikiwa ni Wizara pekee hadi sasa iliyokamisha zoezi hilo.

Amefahamisha kuwa mpango huo utaiwezesha serikali kuongeza maslahi ya walimu kwa kuzingatia kiwango cha elimu na muda wa utumishi.

Akizungumzia changamoto zinazoikabili Wizara ya Elimu zikiwemo upungufu wa walimu wa sayansi, dakhalia na uvamizi wa maeneo ya skuli na vyuo vya ualimu, Makamu wa Kwanza wa Rais ameishauri Wizara hiyo kufanya juhudi za makusudi kuona kuwa matatizo hayo yanapatiwa ufumbuzi.

Wakati huo huo Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mhe. Zahra Ali Hamad amesema Wizara hiyo ina mpango wa kutoa mikopo kwa Skuli za Ufundi za Kengeja na Mikunguni, ili ziweze kujitafutia vifaa.

Amesema matatizo makubwa yanayozikabili Skuli hizo ni pamoja na ukosefu wa malighafi zikiwemo mbao pamoja na vitendelea kazi, vitu ambavyo Wizara itaweza kuvitoa kwa njia ya mkopo, na kwamba kwa mujibu wa taaluma hizo wataweza kurejesha mikopo hiyo.

Aidha amesema Wizara inakusudia pia kuanzisha digirii ya msingi ya Ualimu, ili kuimarisha elimu ya msingi maskulini, yatakayokwenda sambamba na maslahi ya walimu.

Amesema hatua hiyo itasaidia kuwaendeleza walimu kitaaluma, pamoja na kupatikana kwa walimu wenye sifa katika kujenga msingi bora wa elimu kwa watoto.

Kabla ya majumuisho hayo Maalim Seif alipata fursa ya kutembelea kampas mpya ya Chuo cha Ualimu cha Benjamin Mkapa iliyoko Mchangamdogo, Chuo cha Kiislamu Micheweni na skuli ya Sekondari ya Wanawake Utaani.

Hassan Hamad (OMKR)

0 comments:

 
Top