Watanzania wanapaswa kuwacha woga na kuanza kujenga dhana ya kujaribu katika kufikiria kuanzisha miradi tofauti ya kiuchumi itakayotoa fursa za ajira hasa kwa vijana na kuwaongezea kipato chao ili kukidhi mahitaji yao ya kimaisha.

Ushauri huo umetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi katika tafrija maalum ya kutimia mwaka mmoja tokea kuanza kutoa huduma hapa nchini kwa Kampuni ya Kimataifa ya Usafirishaji wa vyombo vya usafiri ya Be Forward. JP iliyofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency Kilimanjaro iliyopo Mjini Dar es salaam.

Balozi Seif alisema wapo baadhi ya watu na taasisi tofauti hapa nchini ambazo zimekuwa na uwezo mkubwa wa kujiongezea mapato zaidi kwa kuanzisha miradi ya kiuchumi lakini zinashindwa kufanya hivyo kwa kuhofia kupata hasara.

Alisema wakati umefika kwa taasisi hizo kuiga mfano wa makampuni na taasisi nyengine za kigeni akatolea mfano zile za nchini Japani ili kuona zinakwenda sambamba na mabadiliko ya kiuchumi yaliyopo hivi sasa ulimwenguni.

“ Kwa nini jamii yetu hasa wafanyakazi wa umma waendelee kuwa na hofu hii wakielewa kwamba bila ya kujaribu hakutapatikana maendeleo yoyote yale “. Alisisitiza Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliipongeza Kampuni hiyo ya usafirishaji wa vyombo vya usafiri ya Be Forward. JP Tanzania kwa mchango wake mkubwa katika kusaidia uchumi wa Tanzania.

Aliuomba Uongozi wa Kampuni hiyo kufikiria wazo la kufungua tawi lake jengine Visiwani Zanzibar ili kuona huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo zinastawisha pande zote mbili ya Tanzania.

Akizungumzia suala la usafirishaji na utoaji wa bidhaa na vyombo vya usafiri Bandarini Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameiomba Mamlaka ya Mapato Tanzania { TRA } kuongeza nguvu za ziada katika kushughulikia utoaji wa mizigo kwa wakati muwafaka.

Alisema hatua hiyo itawarahisishia wananchi kutoa mizigo yao kwa haraka na kuepuka kutozwa fedha nyingi wakati makosa yanapotokea hufanywa na baadhi ya watendaji wa Taasisi zinazosimamia mapato.

“ Inafikia wakati wananchi hutozwa fedha nyingi na wakati mwengine wakalazimika kulipia fidia kwa bidhaa na mizigo yao wanapotaka kutoa bandarini. Unapochunguza ukweli mara nginyi makosa yanayotokezea hayasababishwi na wao “. Alifafanua Balozi Seif.

Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya usafirishaji wa vyombo vya usafiri ya Be Forward. JP Bwana Hironori Yamakawa alisema kampuni hiyo tayari imeshasafirisha zaidi ya magari 4,000 kutokea Japan na kuingia Dar es salaam hadi mwezi Oktoba mwaka huu.

Bwana Yamakawa alisema taasisi yake iliyotoa ajira kwa zaidi ya wafanyakazi 300 wa Kitanzania imekuwa ikipata mafanikio makubwa kutokana na ushirirkiano mkubwa uliopo kati ya uongozi wa Taasisi hiyo na wazawa.

Mkurugenzi Mkuu huyo wa Kampuni ya usafirishaji wa vyombo vya usafiri ya Be Forward. JP alielezea faraja yake kutokana na huduma zinazotolewa na taasisi yake kwa kusafirisha vyombo vya usafiri kutoka Japani hadi Tanzania.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Tawi la Tanzania Isaac Mbinile amewapongeza wafanyabiashara, Taasisi za Umma na zile binafsi kwa uwamuzi wao wa kushirikiana na Kampuni hiyo ulioleta mafanikio makubwa.

Kampuni ya Kimataifa ya usafirishaji wa vyombo vya usafiri Be Forward. JP imekuwa ikitoa huduma za kusafirisha magari kati ya Japani hadi Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati.

Katika Tafrija hiyo maalum ya kutimia kwa mwaka mmoja wa Be Forward. JP iliyoambatana na muziki laini ilijumuisha pia utolewaji wa zawadi kwa washirika na wateja wa Kampuni hiyo.

Zawadi hizo ni pamoja na vyombo vya mtandao wa mawasiliano ya Internet { Ipad }, Mipira na Pampu zake, T. Shirts, Vikombe vya chai pamoja na Gari ndogo aina ya Toyota Passo 2004.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top