Na,Jumbe Ismailly-Singida
YOHANA KUBANDA ni mwanamuziki wa nyimbo za injili aliyeanza kupenda muziki huo alipokuwa na umri wa miaka 8 tangu kuzaliwa kwake.
“Naitwa Yohana Kubanda ni mkazi wa Mtaa wa Bomani mjini Singida ni mwanamuziki wa nyimbo za injili Tanzania niliyezaliwa katika Kijiji cha Igoma,Hospitali ya Bugando, iliyopo Mkoani Mwanza,Okt,10,1986”hivyo ndivyo Kubanda alivyoanza kusimulia historia ya maisha yake.
Mwanamuziki huyu ambaye ni mtoto wa tatu wa familia ya watoto saba wa Mzee Leonard Kubanda anasema alianza kuupenda muziki wa kizaire wa nyimbo za bolingo tangu alipokuwa darasa la tatu,mwaka 1994.
Anasema alianza darasa la kwanza katika shule ya msingi Ikizu 1993 hadi mwaka 1999 ambapo mwaka 2002 hadi 2006 alijiunga na masomo ya sekondari katika shule ya Lake iliyopo Sahara jijini Mwanza.
Alizitaja sababu za wazazi wake kumpiga vita za kukiendeleza kipaji chake kuwa ni pamoja na wazazi wake kutokuwa na mwamko wa elimu,kutokupenda mtoto wao kusoma zaidi ya kufanyakazi za nyumbani kama vile kuchunga ng’ombe.
“Nilianza kuupenda muziki tangu mwaka 1994 wakati huo nikiwa darasa la tatu nilianza kucheza muziki wa bolingo wa kizaire na kutokea kupendwa na mwalimu wangu wa darasa, mwalimu Syilivester Komanya ambaye kwa sasa ni marehemu na mungu ailaze roho yake peponi,(amina)”alisema Kubanda.
Anawataja ndugu zake wengine kuwa ni pamoja na Farida Kubanda (FID Q) aliyesoma hadi kidato cha nne,Emanueli Kubanda,Mashimba Kubanda,Alfa Kubanda,Sundi Kubanda Edina Kubanda na Joyce Kubanda.
Anasema wakati akiwa darasa la tatu,alipoanza kucheza muziki wa nyimbo za kizaire,wazazi wake (baba na mama) waliupinga mpango wake huo kwa kudai kuwa ni uhuni japo kwake yeye kucheza nyimbo za kizaire zilimfanya ajipatie mahitaji mbali mbali ya shule kwa kuwa alikuwa akisoma katika mazingira magumu sana.
Anazitaja sababu za kupenda muziki kwamba tangu akiwa mdogo shuleni alikuwa akishirikishwa sana katika mashairi na kwaya shuleni chini ya usimamizi wake mpendwa,mwalimu Komanya ambaye kwa hivi sasa ni marehemu.
Anafafanua kuwa wazazi wake walimzuia kudansi na kuimba nyimbo za kizazi kipya wakisema kuwa ni uhuni,wakati mziki wa injili hakuzuiliwa na mtu yeyote yule kwani alikuwa tayari alishajitegemea katika maisha ya mtaani.
Anafafanua kwamba ilipofika mwaka 1996 wakati Taifa lilipopatwa na msiba wa ajali ya MV Bukoba na kwa kuwa mwalimu Komanya alikuwa ni mwandishi wa nyimbo za mashairi na ngonjera pale shuleni,alitunga wimbo ambao alikabidhiwa yeye pamoja na wenzake watatu.
Anasema mwalimu Komanya aliwafundisha wimbo huo kama kwaya wakashindwa kukariri vizuri na anakumbuka baada ya kushindwa walichapwa viboka visivyokuwa na idadi kwani kwa wakati huo shuleni kulikuwa hakuna idadi ya viboko vya kuchapwa kama ilivyo kwa sasa.
Anasema baada ya kichapo hicho wenzake hawakuweza kurudi tena shuleni lakini yeye alirudi kwa kuwa aliona akibaki nyumbani ni lazima wazazi wake wangemuambia aende kuchunga mifugo,wakati yeye alikuwa akipinga kabisa kazi hiyo isiyokuwa na faida kwake zaidi ya masomo.
“Mwalimu Komanya aliniomba niimbe hilo shairi peke yangu nashukuru Mungu nilifanikiwa,na baada ya hapo tukatamatisha maombolezo kwa wimbo huo na hapo ndipo nilipoanza kuupenda muziki toka moyoni mwangu kwa kuwa baba na mama yangu hawakupenda kudansi wala kuimba” alisisitiza Kubanda.
Anasema kutokana na msimamo mkali wa wazazi wake alikuwa akishiriki kudansi kwa siri kubwa sana na kujipatia fedha kwa ajili ya mahitaji yake shuleni.
Anaweka bayana Kubanda kwamba siku moja ambayo haitatokea kuisahau ni baada ya kudansi kwenye tamasha la CocaCola na kujipatia zawadi nyingi na za kutosha na aliporudi nyumbani akawakuta wazazi wake,walikuwa tayari wameshapata taarifa kuwa kijana wao anafanya uhuni majukwani.
Anasema kufikishwa kwa taarifa hizo kuwa yeye anashirikiana na vijana waliotoka mjini kufanya uhuni majukwaani hapo ndipo alipigwa kipigo cha mbwa mwitu na hivyo kumfanya awaulize wazazi wake swali kwamba hawaoni kuwa hawamtendei haki?
“Niliendelea kuwauliza kuwa mimi nakwenda shule nakanyaga chini sina viatu,nguo za shule zimetoboka mabegani, nikawaambia toka mnipeleke shule hata daftari hamninunulii na wakati mifugo mnayo,kalamu na daftari siku zote nilikuwa nikipewa na mwalimu wangu’alisisitiza.
Anasema baada ya kuona mateso hayo anayopata kwa wazazi wake aliamua kutembea kwa miguu umbali wa kilomita 65 kutoka Kijiji cha Magu kuelekea Bunda mjini na Kijiji cha Nyamuswa kuelekea Bunda mjini kwenda kwa mjomba wake,Sweya Petro ambaye kwa sasa pia ni marehemu ambapo hata hivyo hakufanikiwa kumkuta.
Anasema baada ya kumkosa mjomba wake Bunda mjini alilazimika kulala kwa siku mbili kwenye kituo cha mabasi cha Bunda na ndipo baada ya kuzidiwa na njaa alimkumbuka mjomba wake mkubwa na alipomuuliza mdogo wake amekwenda wapi,alikamatwa na kurudishwa tena kwa wazazi wake.
Anabainisha kwamba baada ya kufikishwa nyumbani kwa wazazi wake na mjomba wake mkubwa ndipo wazazi wake walimpa adhabu ya kwenda kuchunga mifugo na kulima,ndipo alipoamua kurudi tena shuleni kuendelea na masomo baada ya kuombewa msamaha na mwalimu wake aliyemtaja kwa jina la Komanya.
Anafafanua kuwa baada ya kumaliza masomo ya darasa la saba wazazi wake walishindwa kumsomesha aliamaua kutoroka nyumbani na kwenda mjini kuanza maisha ya mtaani huku akiendelea kusoma biblia kumuomba zaidi mungu ili aweze kumsaidia katika maisha yake,licha ya kwenda katika ofisi za serikali kuwaomba msaada wa masomo ya sekondari,ambapo hata hivyo hakufanikiwa.
“Siku moja kulikuwa na Tamasha la CRDB Bank mjini Musoma kama kawaida yangu nilishiriki na kufanikiwa kushinda Akaunti ikiwa na fedha taslimu shilingi 50,000/= bahati nzuri Muhasibu wa Benki mwaka 2000 akaniita na kuniuliza maswali kadhaa kisha akanichukua na kuamua kuishi na mimi na huku nikirudi shule kwa gharama zake mwenyewe hadi nikamaliza elimu ya sekondari mwaka 2004”alifafanua.
Anasema Kubanda kwamba alibahatika kurekodi albamu yake ya nyimbo za kidunia iliyokuwa ikiitwa “Mapenzi sio pesa” albamu hiyo ilimpa shoo nyingi na kumfanya afurahie kipaji chake kwa kuwa Baba yake mlezi hakumzuia kuimba wala kudansi na alimuunga mkono kwa kila hatua.
Anasema mwaka 2005 akiwa mjini Singida alikutana na Mhandisi mmoja mwenyeji wa Nchini Uganda aliyetambulika kwa jina la Jonathan na anakumbuka ilikuwa ni katika shoo ya Miss Singida na baada ya kushuka jukwaani alimwita na kumpa fedha na kumtaka aimbe nyimbo za kidini na kumshauri aachane na nyimbo za kidunia.
Anaweka bayana kuwa japo alikubali kwa shingo upande kwa kuwa alikuwa akilipwe fedha akakubali kurekodi albamu hiyo ambayo ndiyo ya kwanza inayoitwa “Raha ya Moyo” na baada ya kumaliza kurekodi albamu hiyo ndipo Mhandisi Jonathan kila wakati alimuomba aachane na muziki wa kidunia.
Hata hivyo Kubanda alisisitiza kwamba ilikuwa ngumu sana kwake kwa kuwa kichwani alikuwa ameshasuka nywele tayari kwa ajili ya sho za kidunia.
Anasema baada ya hapo ndipo alipomuuliza swali mtumishi huyo kutokana na kuwa na nywele hizo akiamua kumtumikia Mwenyezi Mungu je kanisa halitamtenga ambaye alimjibu kwamba kama amebatizwa na anamjua Mungu naye pia anamuomba amtumikie Mwenyezi Mungu kwani sauti yake inafaa aimbe nyimbo za Mungu atabarikiwa sana.
Anasema mwaka 2010 kupitia Albamu yake ya Raha ya Moyo ilimpa nguvu na kumfanya atoe albamu yake ya pili ilikuwa ikiitwa “Mpende Bwana Mungu wako” na anashukuru albamu hiyo iliungwa mkono na viongozi wake wa dini na kufanikiwa kufanya uzinduzi na kuzinduliwa na Naibu Spika kwa wakati huo alikuwa Bwana Job Ndugai ambaye kwa sasa ni Spika wa Bunge na anamshukuru sana kwa yeye kumuunga mkono.
Hata hivyo Kubanda anaweka bayana kwamba kwa sasa ana albamu mpya iitwayo “Narudi Nyumbani” ambayo ilizinduliwa na Mbunge wa jimbo la Ubungo,Saed Kubenea na kwamba albamu hiyo imegharimu shilingi milioni saba ambayo ameshutia Nairobi,Dar-es-Salaam,Zanzibar pamoja na baadhi ya maeneo ya Singida.
Kubanda hata hivyo anazitaja changamoto anazozipata katika muziki wake ni uhaba wa vifaa vya muziki wa bendi,watu kutokubali kuimba akiwa na nywele nyingi kichwani wakidai kuwa ni muhuni pia,wakati anavyojua mtu anayemjua mungu huwa hana alama na mwenyezi mungu kaamua kumtumia kupitia kipaji chake.
“Kwa kuwa sina menejimenti yeyote inayonisaidia zaidi ya kupata sapoti kutoka kwa viongozi wake wa dini na kanisa lake kwa ujumla,kuna wakati fulani nilikata tamaa lakini nilipewa moyo na Padre Edward Mapunda wakati ule kabla hajawa askofu kwani kwa sasa ndiye askofu wetu wa jimbo letu la Singida mjini”anasisitiza.
Anafafanua msanii huyo kwamba wakati askofu Mapunda akiwa nje ya nchi masomoni alimzawadia gitaa aina ya Galatone lenye thamani ya shilingi 350,000/= hivyo askofu wake alimtia moyo mpaka leo anaendelea kumtumikia Mwenyezi mungu.