Na,Jumbe Ismailly-IRAMBA 
KITUO cha Msaada wa kisheria kwa Wanawake (WLAC) kimesema ukatili wa kijinsia ni tatizo kubwa kiulimwengu na kwamba utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) unaonesha kuwa kati ya asilimia 12 mpaka 25 ya wanawake duniani wamefanyiwa vitendo vya ukatili,aidha wa kiuchumi,wa kingono na ama wa kimwili. 

Mratibu wa mradi wa kuelimisha jamii kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia na ukeketaji kutoka Kituo cha msaada wa Kisheria kwa wanawake na Watoto,Viviani Kweka aliyasema hayo kwa nyakati tofauti katika Kijiji cha Maluga na Ng’ang’uli vilivyopo katika kata ya Maluga wakati wa kuutambulisha mradi wa kuelimisha jamii kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia pamoja na ukeketaji. 

Aidha Kweka aliweka bayana kuwa mraddi ulianza kutoa elimu hiyo kwa wasaidizi wa kisheria,Maofisa Ustawi wa jamii,Maofisa Maendeleo ya Jamii,jeshi la polisi kupitia dawati la jinsia,makundi ya vijana na wanawake pamoja na shule za msingi kwa ufadhili wa Shirika lisilokuwa la kiserikali la The Foundation For Civil Society. 

Kwa mujibu wa Mratibu huyo kwa takwimu za mwaka 2016 zilizofanywa na UNICEF zinaonesha kwamba katika tafiti zilizofanyika katika nchi 30 duniani,takribani wasicha milioni 200 wamefanyiwa ukeketaji na kati ya nchi hizo,27 zipo Afrika na Tanzania ikiwa mojawapo. 

“Kwa hiyo tunaweza kuona kwamba ukatili wa kijinsia bado ni tatizo kubwa sana hapa nchini kwetu”alisisitiza Kweka. 

Kuhusu nini kifanyike kukabiliana na hali hiyo,Mratibu huyo alibainisha kuwa njia pekee ni kutoa elimu kwa wananchi itakayosaidia kuwabadilisha,wakafunguka na kubadilisha mitazamo yao waliyokuwanayo dhidi ya wanawake na watoto. 

Hata hivyo Kweka ambaye pia ni Wakili kutoka WLAC alitumia mafunzo hayo kutoa wito kwa wananchi wanaofanyiwa vitendo vya ukatili huo kujenga utamaduni wa kuvunja ukimya na kufunguka na kutoa taarifa kwenye sehemu husika kama vile wajumbe wa mashina ya nyumba kumi,wenyeviti wa vijiji na vitongoji,maofisa watendaji wa kata na vijiji. 

Kwa mujibu wa Vivian kinachosababisha ukatili wa kijinsia katika Kata ya Maluga pamoja na sehemu nyinginezo ni watu kukumbatia mila potofu,ambapo mila na tamaduni kwa kiasi kikubwa zinasababisha ukatili wa kijinsia sambamba na uelewa mdogo kwamba ukatili wanaofanyiwa watu ni kinyume cha sheria. 

Kwa upande wao Wawezeshaji wa mafunzo hayo,Mwanasheria kutoka WLAC,Robert Chuwa aliwashauri wananchi wa kata hiyo kujenga utamaduni wa kuandika wosia ambao kwa kiasi kikubwa utawasaidia sana wanawake ambao ndiyo waathirika wakubwa pale inapotokea mmoja anapofariki. 

Naye Wakili wa Kujitegemea,Benjamin Kalume alisema ukatili unaofanyika katika Kijiji cha Maluga ni ukatili wa kimwili ambao ni kinyume kabisa na sheria zilizopo Tanzania na vitendo vya ukatili vinavyofanywa katika Kijiji hicho ni vya kipigo kwa wanawake.

0 comments:

 
Top