Na,Jumbe Ismailly-MANYONI 
RAIS wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania,Dk.John Pombe Magufuli ameupatia Mkoa wa Singida msaada wa vitanda 14 vitakavyosambazwa katika vituo vya kutolea huduma ili kusaidia kupunguza msongamano wa wajawazito kulala wawili wawili katika kitanda kimoja.

Akikabidhi msaada wa vitanda hivyo kwenye viwanja vya Hospitali ya Mkoa wa Singida kwa Mkuu wa Mkoa huo kwa niaba ya Rais,Mbunge wa viti maalumu Mkoa wa Singida,Aysharose Mattembe licha ya kumshukuru rais kwa niaba ya wanawake wa Mkoa huo,vile vile alitumia wasaa huo kumwombea kwa Mungu amjaalie baraka,afya na nguvu tele ili aendelee kuwatetea wanyonge. 

Hata hivyo mwakilishi huyo wa wananchi aliweka bayana pia kwamba Rais Magufuli amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba raslimali za nchi hazitumiwi ovyo na kisha kutoa mfano wa mazungumzo yaliyofikiwa muafaka kati ya Kampuni ya madini ya ACASIA na serikali kwa kampuni hiyo kukubali kulipa fedha walizokuwa wakidaiwa na serikali. 

“Nyote ni mashahidi mmeona Kampuni ya Acasia wamekubali kutulipa na hizi zote ni juhudi za Rais John Pombe Magufuli kuhakikisha kwamba raslimali za nchi zinatumika ipasavyo na raslimali za nchi zinakuwa chini ya Watanzania wote wanyonge”alisisitiza Mattembe. 

Kwa mujibu wa Mbunge huyo wa viti maalumu Mkoa wa Singida ni ukweli usiopingika na wote ni mashahidi kwamba uwajibikaji umeimarika katika maeneo mbali mbali,huku akiwahurumia watumishi wa sekta ya afya kutokana na kufanyakazi zao katika mazingira magumu. 

Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida,Dk.Emmanuel Kimario aliweka bayana kwamba katika kipindi cha kuanzia mwezi Julai,hadi Sept,mwaka huu jumla ya wanawake 12,431 wamejifungua Mkoani Singida,ambapo kati yao,wanawake 268 wamejifungulia nyumbani na kwa wakunga wa jadi. 

“Kwa data tulizonazo za kujifungua katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka huu kwa Mkoa mzima wa Singida jumla ya akina mama waliojifungua ni 12,431”.alisisitiza Kaimu Mganga mkuu huyo wa Mkoa. 

Aidha Kaimu Mganga mkuu huyo alifafanua kwamba kati ya akina mama hao,190 walijifungulia nyumbani huku akina mama 78 wakisaidiwa na wakunga wa jadi wakati waliojifungua kabla ya kufika katika vituo vya kutolea huduma walikuwa 258 na waliojifungulia katika vituo vya kutolea huduma walikuwa 11,905 na hivyo kufanya jumla ya akina mama 12,431 waliojifungua Mkoani hapa katika kipindi hicho. 

Akitoa taarifa ya hali ya upatikanaji wa dawa pamoja na vifaa tiba,Afisa Huduma kwa wateja (MSD –Dodoma),Innocent Mgisha aliweka wazi kwamba katika kipindi hicho Mkoa huo umepokea kwa kila Halmashauri mashuka 50 yenye thamani ya shilingi 600,000/=,vitanda 20 vyenye thamani ya 596,000/=magodoro 20 yenye thamani ya 3,440,000/=,vitanda vya kujifungulia akina mama vyenye thamani ya shilingi 1,002,021. 

Kwa mujibu wa Mgisha vifaa vyote vilivyotolewa na MSD na kupokelewa vina thamani ya jumla ya shilingi 121,100,000/= na kwamba kila Halmashauri itakuwa imepata vifaa tiba pamoja na dawa vyenye thamani ya shilingi 17,700,000/=. 

Akipokea msaada huo wa vitanda huku akisisitiza Halmashauri kuonyesha nia ya kumuunga mkono Rais,Mkuu wa Mkoa wa Singida,Dk.Rehema Nchimbi aliagiza kwamba kabla ya mwezi juni,2018,kila Halmashauri ihakikishe imenunua vitanda bora kumi vyenye thamani ya shilingi milioni 13 kwa ajili ya kujifungua akina mama wajawazito

0 comments:

 
Top