Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Ndugu Hemed Suleiman Abdulla amwataka wananchi kuendelea kudumisha amani iliyopo Nchini kwani ndio inayopelekea kukuwa sekta ya uwekezaji na utalii na kukuza mahusiano mazuri na Nchi mabali mbali.
Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi Jimbo la Bububu na Jimbo Mtoni Wilaya wa Mfenesini Kichama katika Tawi la CCM Kizimbani ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kukiimarisha Chama na jumuika zake.
Mhe. Hemedi ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema Ilani ya Chama cha Mapinduzi inasisitiza kudumisha Amani na Utulivu Nchini hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha anailinda Amani iliyopo kwa maslahi ya Taifa.
Aidha Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa amesisitiza kuepuka makundi na migawanyiko ndani ya Chama Cha Mapinduzi na kuwataka Viongozi na wana CCM kushirikiana katika kutekeleza Ilani ya CCM, kukiimarisha Chama na kuzitekeleza ahadi walizozitowa wakati wa Uchaguzi wa Dola wa mwaka 2020.
Amesema wajibu Viongozi wa CCM wa ngazi mbali mbali kushirikiana pamoja kukiimarisha Chama na kuitekeleza kwa vitendo Ilani ya CCM ili Chama cha Mapinduzi kiiendelee kutawala na kushinda kwa kishindo katika uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2023.
Sambamba na hayo Mhe. Hemed amewaonya na kusema Chama cha Mapinduzi kitawachukulia hatua za kinidhamu wale wote ambao wanatumia Vyeo vyao kwa kwenda kinyume na maelekezo ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa kuwagawa wanachama, kuleta migogoro ndani ya chama ambayo inazorotesha Ukuwaji wa Chama na mikakati ya ushindi wa kishindo 2025.
Katika ziara yake hiyo Mhe. Makamu amewaeleza wana CCM wa Jimbo la Bububu kuwa Serekali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi itawajengea barabara yao ya Mndo kwa kiwango cha Lami ambayo itawaondoshea usumbufu wa kufuata huduma ya usafiri masafa ya mbali kwa shughuli binafsi na za kibiashara.
Akimkaribisha Mgeni Rasmi Katibu wa Siasa, Itikadi na Uenezi Ndugu Khamis Mbeto amewaomba wanachama wa CCM kushikamana katika kukijenga Chama na kuondoa tofauti zao kufanya hivyo kutapelekea CCM kushinda katika Uchaguzi wa Dola wa 2025.
Mbeto amesema kazi iliyopo mbele yetu kwa sasa ni kukuimarisha Chama na Jumuiya zake na sio kupanga safu za Viongozi watakaogombea katika Uchaguzi ujao kwani kufanya hivyo ni makosa na chama hakitasita kumchukulia hatua za kinadhamu kiongozi ama mwanachama yoyote atakaebainika kufanya hivyo.
Akitoa shukurani za CCM Mkoa wa Magharibi Kichama Mwenyekiti wa CCM Mkoa huo Ndugu Moh'd Rajab amesema wanachama wa CCM Mkoa wa Magharibi wamefarijika kumuona Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa anatembelea Majimboni kujionea utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Mwenyekiti Rajab amewaomba Viongozi wa Wilaya na Majimbo kufanya kazi kwa ushirikiano, usawa na kutenda haki kwa wanachama wote kwani kufanya hivyo watakajinga Chama na Jumuiya zake na kushinda katika uchaguzi ujao
Nao viongozi wa Jimbo la Bububu na Jimbo la Mtoni wamesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetekeleza vyema Ilani ya CCM kwani maendeleo yanaonekana ndni ya Majimbo hayo ikiwemo Hospital ya Wilaya, maji safi na salama pamoja Miundombinu ya barabara.
Viongozi hao wamewaomba wanachama wa CCM na wananchi kuendelea kukiamini chama cha Mapinduzi na Ufikapo Uchaguzi Mkuu wa 2025 waichague CCM ili kiendelee kushika madaraka na kuwatumikia wananchi wake.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Ndugu Hemed Suleiman Abdulla ameendelea na ziara yake ya kukiimarisha Chama Cha Mapinduzi kwa kuyatembelea na kupokea taarifa mbali mbali za CCM katika Jimbo la Bububu na Mtoni.
Nao wanachama wa Chama Cha Mapinduzi wamemshukuru na kumpongeza Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Ndugu Hemed Suleiman Abdulla kwa kuamua kutembelea Majimbo yao na kumuahidi kuwa watayafanyia kazi yale yote aliyowaelekeza ikiwa ni pamoja na kuendelea kukiimarisha Chama Cha Mapinduzi kunzia ngazi ya Shina hadi Taifa ili kukiletea ushindi chama hicho katika Uchaguzi Mkuu ujao 2025.
Imetolewa na kitengo Cha Habari ( OMPR)
0 comments:
Post a Comment