Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amewataka Wakuu wa Mikoa wote kuzisimamia  fedha zilizotengwa kwa zoezi la utambuzi wa Anwani za Makazi ili zitumike kama zilivyokusudiwa.

Mhe. Hemed ameeleza hayo katika Kikao Kazi kilichowakutanisha Wakuu wa Taasisi za Serikali kuhusu utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi Zanzibar kilichoketi Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar.

Amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeamua kutenga Fedha isiyopungua Billioni 28 kwa zoezi la utambuzi wa Anwani za Maakazi ambapo zitaelekezwa kwa Ofisi za Wakuu wa Mikoa yote nchini na kueleza kuwa Mgao wa fedha hizo unazingatia na Ukubwa wa mkoa na wakaazi wake.

‘’Mgao wa fedha hizi umezingatia ukubwa wa Mikoa na uhalisia wa Idadi ya wananchi waliopo katika kila Mkoa’’Mhe. Hemed

Amesema Serikali haitamvumilia mtu yoyote atakaejaribu kutumia fedha hizo kwa matumizi mengine sheria itachukua mkondo wake

Makamu wa pili wa rais ametaka wakuu wa taasisi husika kuheshimu fedha hizo ili zoezi lililopangwa liweze kufikiwa na kukamilika kwa wakati uliopangwa na liweze kuleta tija kwa nchi yetu.

‘’Fedha hizi ziende zikatumike zilivyokusudiwa na tutazifatilia kwa karibu kuona zinatumika zilivyokusudiwa’’ alisema

Sambamba na hayo Mhe. Hemed amewataka watendaji wanaosimamia Mfumo huo kutumia Taaluma zao pamoja na Busara ili kuwafikia wananchi wote ili waweze  kutoa mashirikiano na kuweza kukamilika kwa zoezi hilo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewataka viongozi hao kuwajibika katika maeneo yao kulingana na  nafasi zao katika taasisi na kuwataka kuendelea kuwaelimisha wananchi umuhimu wa zoezi hilo ili waweze kushiriki kikamilifu.

Mhe. Hemed amesisitizi kushirikishwa kwa wananchi katika maeneo yao wakati wa utekelezaji wa mfumo wa Anwani za Makazi ili waweze kuwajibika kikamilifu katika utambuzi wa maeneo yao na kurahisisha kukamilika kwa mfumo huo.

Mhe. Hemed ametumia fursa hiyo kuwataka watendaji wa mfumo huo kutoa taarifa kwa Mamlaka husika kwa changamoto zozote zile watakazokutana nazo katika maeneo yao ya kufanyia kazi ili kuweza kutatuliwa changamoto zao kukamilisha zoezi hilo na likamilike kama lilivyopangwa.

Aidha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewaagiza Wakuu wa Mikoa wote kuzisimamia Kamati walizoziunda juu ya usimamaizi wa Sensa Ya watu na makazi ili kufanikisha zoezi hilo kwa urahisi zaidi.

Nae Waziri wa Nchi Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Mhe. Dkt Khalid Salum Muhamed ameeleza kuwa ni vyema kwa wananchi kujenga uelewa zaidi juu ya Programu hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa na kuwataka wadau husika kuendeleza kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa jambo hilo.

Aidha Waziri Dkt Khalid ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi kwa kuanzisha dhana ya kuwepo kwa Anwani za Makazi kwa maslahi ya watanzania.

Kwa upande wake Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape M. Nnauye (MB) amemuhakikisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa Wizara anayoisimamia ikishirikiana na Wizara yaujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar inaendelea na zoezi hilo ambapo amemuahidi kuwa litakamilika kwa wakati na kwa lengo lililokusudiwa.

Amesema wizara hizo zinasimamia vyema zoezi hilo kwa lengo la kuifikisha Tanzania kukuwa kiuchumu kwa njia za kidigitali ili kuendana na Dunia ya kidigitali.

‘’zoezi hili ni mwanzo wa safari ya kuelekea katika Tanzania ya kidigitali’’ amesema

Abdulrahim khamis

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top