Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema kufanya vizuri kwa Timu za Michezo za Baraza la Wawakilishi ni jambo liloiletea heshima Zanzibar.

Mhe. Hemed ameyasema hayo katika Hafla ya kuzipongeza timu za wanamichezo wa Baraza la Wawakiishi iliyofanyika katika ukumbi wa Golden Tulip Uwanja ndege Zanzibar.

Amesema kufanya vizuri kwa timu hizo katika mashindano ya Mabunge ya Afrika Mashariki ni ishara ya kuitangaza Zanzibar kwa kurejesha heshima ya Michezo ndani na nje ya Nchi.

Mhe. Hemed ametumia fursa hiyo kuwapongeza wajumbe wa Baraza la Wawakiishi kwa kushiriki vyema katika mashindano hayo  na kuwaahidi kuwa Serikali kupitia wadau mbali mbali wa michezo wataendelea kuunga mkono timu hizo ili miaka ijayo zizidi kufanya vyema katika mashindano hayo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewashukuru wadau mbali mbali wa maendeleo kwa kuziunga mkono timu hizo na kueleza kuwa hatua hiyo ni kuonesha namna wanavyomuunga mkono Mhe. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi katika kuinua Michezo Zanzibar.

Mhe. Hemed ametumia fursa hiyo kuwaomba wadau hao kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Awamu ya Nane katika kuhakikisha Zanzibar inaimarika kimaendeleo katika nyanja mbali mbali ikiwemo Michezo.

Sambamba na hayo Mhe. Hemed amevishukuru vyombo vya habari kwa kuyatangaza mashindano hayo ambapo wamerahisisha wazanzibari kujua timu hizo zinavyoshiriki katika mashindano hayo.

Kwa upande wake Spika wa Baraza la Wawakiishi Mhe. Zubeir Ali Maulid amewashukuru Maspika wa Mabunge ya Afrika Mashariki kwa kuiridhia Baraza la Wawakiishi kuweza kushiriki katika mashindano hayo kwa mara ya kwanza hatua ambayo imeweza kukuza mashirikiano zaidi kwa mabunge hayo.

Mhe. Zubeir amesema kuwa ushiriki za Zanzibar katika mashindano hayo umeamsha ari ya michezo kwa wajumbe wa Baraza la Wawakiishi kwa kuwaweka tayari kiakili na kimwili.

Nae Mwenyekiti wa Michezo Baraza la Wawakiishi Mhe. Hamza Hassan  Juma ameeleza kuwa Michezo ndani ya Baraza la Wawakilishi imeasisiwa miaka mingi nyuma kwa lengo la kuwajenga Wawakilishi kiakili ili kuwajibika vyema katika majukumu yao ya kuwawakilisha wananchi katika chombo hicho.

Nae katibu wa Baraza la Wawakiishi Zanzibar Raya Issa Mselem amesema Uongozi wa Baraza la Wawakilishi unampongeza Spika kwa kusimamia ushiriki wa Timu hizo kwa mara ya kwanza katika mashindano hayo na kuahidi kuwa timu hizo zitaendelea kufanya vizuri katika kila mashindano zitakayoshiriki.

Abdulrahim khamis

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top