Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameupongeza Umoja wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii Tanzania kwa kuanzia umoja huo kwa lengo la kuendeleza kutoa huduma bora kwa Jamii.

Mhe. Hemed ameeleza hayo Ofisini kwake Vuga alipokutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Umoja huo kwa lengo la kupata maelekezo kutoka kwake juu ya uboreshaji wa huduma zao.

Mhe Hemed amesema ni jambo la kupongezwa kwa kufikiria kuanzisha umoja huo wakiwa na lengo la kuzidisha ushirikiano na kuwataka kujikita zaidi katika mambo yatakayosaidia kukuza uchumi wa Tanzania.

Makamu wa pili wa rais amesema amefarijika sana  kuona umoja huo unaandaa mafunzo mbali mbali ya kiutendaji ili kuhakikisha wanakuza uzoefu baina yao na kueleza kuwa uzoefu huo utaimarisha Huduma za Kijamii.

Aidha Mhe. Hemed amewaeleza wajumbe hao kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina malengo mengi ya kukuza uwekezaji kupitia Taasisi mbali mbali za Kijamii ikiwemo Mifuko ya Hifadhi ya Jamii iliopo nchini  kwa lengo la kuwekeza miradi mbali mbali ya maendeleo.

Mhe. Hemed ametumia fursa hiyo kuitaka mifuko ambayo inafanya kazi zake Tanzania bara  kuja kuwekeza Zanzibar na kueleza kuwa SMZ itaweka masharti ya kusimamia miradi hiyo na kuwahakikishia uwezekano wa kurejesha fedha zinatakazotumika katika miradi hiyo.

Pia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewaeleza viongozi wa umoja huo kuwa  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaamini kuwa Mifuko hiyo ni katika sehemu ya kuisaidia Jamii kwa mambo mbali mbali na kuwataka kuhakikisha wanasimamia sheria zilizopo katika kendesha Taasisi hizo.

Akizungumza kwa niaba ya viongozi hao Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF)Bwana Mussa Ibrahim Iyombe amemueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa umoja huo umefarijika kwa Nia Njema ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuthamini juhudi zinazofanywa na Mifuko ya hifadhi ya Jamii Tanzania na kumuahidi kuendeleza ushirikiano uliopo baina yao kwa Maslahi ya Taifa.

Aidha Bwana Iyombe amemuhakikisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa mifuko ya Hifadhi ya Jamii Tanzania Bara wataangalia namna bora ya kuja  kuwekeza Zanzibar kwa kufata taratibu salama kwa Maslahi ya Taifa.

Abdulrahim Khamis 

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top