Jumla ya maswali ya msingi Mia Moja na Thalathini na Tisa (139) na maswali ya nyongeza Mia Tatu na Thalathini na Saba (337) yaliulizwa na kujibiwa pamoja na kujadili Taarifa mbali mbali za Kamati za Kudumu za Baraza la Wawakilishi katika Mkutano wa sita wa Baraza la kumi la wawakilishi.
Hayo yameelezwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdullah katika hotuba yake wakati akiakhirisha Mkutano wa Sita wa Baraza la Kumi la Wawakilishi Chukwani Zanzibar.
Amesema Mkutano huo uliweza kujadili Taarifa kumi (10) za Kamati za Kudumu za Baraza la Wawakilishi, Taarifa moja (1) ya Kamati ya Kanuni na Sheria Ndogo Ndogo na Taarifa ya Kamati ya Wabunge watano (5) wanaowakilisha Baraza la Wawakilishi katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Amesema taarifa zilizowasilishwa zitakuwa chachu kwa Serikali katika kutatua changamoto walizozigundua wakati wa kupitia Taasisi mbali mbali za Serikali, na kuwapongeza wajumbe kwa kuendelea kuisimamia, kuikosoa na kuishauri Serikali katika mambo mbali mbali yanayolenga kuboresha maendeleo ya ustawi wa wazanzibari.
’’Ni ukweli usiofichika kuwa taarifa za kamati hizi ni kioo cha kufikia maendeleo ya kweli’’ alisema
Kuhusu muelekeo wa Serikali ya Awamu ya Nane katika miradi ya maendeleo Mhe. Hemed ameeleza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza miradi ya fedha za kupunguza athari zilizotokana na ugonjwa wa Uviko 19 katika Taasisi mbali mbali za Serikali zikiwemo Sekta za Elimu, Afya, Maji na Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na kueleza kufurahishwa kwake kwa hatua iliyofikia miradi hiyo.
’’Katika utekelezaji wa miradi hiyo kumekuwa na mafanikio makubwa na kama wakandarasi wataendana na kasi waliyoanza nayo basi naamini kuwa tutapunguza shida za wananchi katika nyanja mbali mbali’’ Mhe. Hemed
Aidha ametumia fursa hiyo kuwataka Mawaziri waliopata miradi hiyo kuendelea kuwasimamia wakandarasi na washauri elekezi ili kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa kiwango kinachokubalika, inamalizika kwa wakati na inaendana na thamani halisi ya fedha zilizotumika.
Sambamba na hayo Mhe. Hemed amewaomba wananchi kushirikiana na viongozi wa majimbo katika kufuatilia miradi mbali mbali inayoendelea katika Majimbo yao na kueleza kuwa ushirikiano wao ni muhimu sana ambao kutarahisisha utekelezaji wa miradi hiyo kwa wakati.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewaomba wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Viongozi wa ngazi zote kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi na kushiriki kikamilifu katika zoezi la kuhesabiwa kwa lengo la kupanga vizuri mipango ya maendeleo.
Kuhusu mvua zinazotarajia kuanza Nchini Mhe. Hemed amewataka wananchi kujiandaa kukabiliana na mvua hizo hasa kusikiliza taarifa kutoka Mamlaka ya hali ya hewa na taasisi nyengine zinazohusika ili kupata taarifa zaidi na kuchukua tahadhari juu ya maradhi mbali mbali ya miripuko.
Akigusia uwajibikaji Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewaagiza Makatibu Wakuu kuwasimamia Watendaji walio chini yao kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi, uadilifu na uwajibikaji kwa kufuata Sheria na Utaratibu wa Utumishi wa Umma ili kuleta tija kwa Serikali.
Katika hotuba hiyo Mhe. Hemed amekemea tatizo la rushwa linaloendelea Nchini na kueleza kuwa vitendo hivyo ni adui wa maendeleo ambavyo vinazorotesha huduma zinazotolewa na Serikali kutowafikia wananchi ipasavyo na kuagiza Mamlaka ya kupambana na rushwa na uhujumu wa uchumi
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi kuunga mkono juhudi za Serikali katika kukuza uchumi wa Nchi kwa kuongeza mapato kupitia njia sahihi ya kutoa na kudai risiti wanapofanya miamala mbali mbali na kuwataka wafanyabiashara kutumia mashine za kieleketroniki kwa lengo la kuboresha huduma zao.
’’ Nawaomba wananchi kuunga mkono juhudi hizi zinazochukuliwa na Serikali yetu za kukuza mapato kwa kudai risiti mara baada ya kununua bidhaa. Aidha, nawataka wafanyabiashara kuzitumia vizuri mashine hizo na kutoa risiti kwa mwananchi pale wanaponunua bidhaa’’.
Aidha ameziagiza Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa upande wa Zanzibar kushirikiana kwa pamoja kuwasimamia na kuwaelimisha wafanyabiashara watakaokwenda kinyume na miongozo ya Serikali katika ukusanyaji wa mapato kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi yao, na kuongeza kuwa Serikali imejipanga kukusanya mapato na kuhakikisha wafanyabiashara wanapata faida katika biashara zao.
Akigusia suala la kulinda miundombinu mbali mbali Mhe. Hemed amesema Serikali haipendezwi na tabia ya baadhi ya wananchi kuharibu miundomnbinu ikiwemo ya maji, taa za barabarani na umeme na kuwataka wananchi kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama wanapokuwa na taarifa za watendaji wa matendo hayo ili kuwakamata wahusika wa vitendo hivyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameitaka Wizara ya Biasahara na Maendeleo ya Viwanda kwa kushirikiana na Taasisi husika kusimamia vyema bei za bidhaa ili kuepuka kupanda bei kiholela hasa katika kipindi kijacho cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Kikao cha Baraza la kumi la Wawakilishi kimeakhirishwa hadi Jumatano ya tarehe Ishirini na Saba Aprili 2022 saa Tatu Kamili Asubuhi
Abdulrahim Khamis
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment