Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameipongeza kamati ya Haki,maadili na madaraka ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kusimamia misingi ya kisheria na haki za wabunge.

Mhe. Hemed ametoa Pongezi hizo alipofanya mazungumzo na Kamati hiyo katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani.

Amesema Kamati hiyo ni muhimu sana kwa Bunge ambapo kwa misingi ya Sheria iliyopo inawajibika vyema kwa kuweza  kusimamia nidhamu ndani na nje Bunge na kufanikisha malengo yaliyokusudiwa na wabunge hao katika kuwatumikia wananchi wa Tanzania.

Mhe. Hemed amesema Kamati hiyo inasimamia misingi ya maadili kwa kuhakikisha Bunge linajengeka kwa kufata maadili na uwajibikaji kwa viongozi hao na kusema  kuwa muhimili wa Bunge upo Imara kwa maslahi ya Watanzania wote.

Aidha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewataka wajumbe wa kamati hiyo kuendelea kulitumikia Bunge kwa kuwajibika na kuongeza mashirikiano baina yao jambo ambalo litaongeza uwajibikaji katika majukumu yao ya kila siku.

Sambamba na hayo Mhe. Hemed ameipongeza kamati hiyo kwa kuamua kukutana na kamati ya maadili na kinga za wajumbe ya baraza la wawakilishi la Zanzibar kwa lengo la kubadilishana uzoefu,na kusisitiza mashirikiano baina yao ili kuzidi kubadilishana mawazo ya kuendesha na kusimamia kamati hizo.

Mhe. Hemed ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt Hussein Ali Mwinyi kwa kuendelea kuijenga Tanzania yenye maendeleo na kuwataka viongozi wa kamati hizo kuwasaidia viongozi hao katika kuiletea Tanzania maendeleo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Haki maadili na madaraka ya bunge Mhe EMMANUEL A. MWAKASAKA ameshukuru Bunge kwa kuwaaamini kuwateuwa katika Kamati hiyo na kuahidi kusimamia vyema majukumu  yao kwa ueledi ili kujenga nidhamu ndani ya Bunge kwa maslahi ya Tanzania.

Pia mhe MWAKASAKA amemshukuru Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Mhe. Dkt. Tulia Akson kwa kuisimamia Kamati hiyo katika kuendesha majukumu yao ikiwemo kuwapatia mafunzo ya mara kwa mara jambo ambalo linawaongezea uzoefu katika majukumu yao ya kila siku.

Nae Mwenyekiti wa Kamati ya maadili na kinga za wajumbe ya Baraza la Wawakilishi Mhe. PANYA ALI ABDALLA amesema kuwa Baraza limefarijika kwa ujio wa Kamati hiyo hatua ambayo imetoa fursa ya kuwakutanisha wajumbe wa Kamati hizo za Mihimili  miwili kuweza kubadilishana mawazo na kumuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa wataendeleza mashirikiano hayo kwa kuongeza nidhamu ndani ya Muhimili mitukufu ya kutunga na kubadilisha sheria.

Wakati huo Makamu wa Pili wa  Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amekutana na Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania Sheikh Abdullah Alsheryan Ofisini kwake Vuga ambapo katika mazungumzo yao yalijikita katika kukuza mashirkiano baina ya Zanzibar na Saudi Arabia nchi ambazo zina udugu wa kihistoria katika Nyanja tofauti.

Katika hatua nyengine Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amemuomba Balozi huyo kuwaomba  wawekezaji wa Saudi Arabia kuja kuwekeza Zanzibar hasa kuzingatia Serikali ya Awamu ya Nane imefungua mlango wa uwekezaji katika Nyanja tofauti.

Abdulrahim Khamis

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

0 comments:

 
Top