Serikali ya Awamu ya Nane imedhamiria kukuza uchumi wake kupitia sekta ya Viwanda ili kutatua changamoto ya ajira kwa vijana.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alitoa kauli hiyo wakati alipofanya ziara ya kukagua eneo maalum la Viwanda vidogo vidogo liliopo Amani Mkoa wa Mjini Magharibi.
Alisema serikali ya awamu ya nane chini ya uongozi wa Dk. Hussein Ali Mwinyi imeamua kuweka mkazo katika Sekta ya uwekezaji kwa kuwakaribisha wawekezaji kuekeza katika eneo la viwanda.
Wakati akitembelea maneo mbali mbali ya eneo hilo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwahakikishia waekezaji waliopewa nafasi ya kuekeza kuwa serikali itaendelea kutoa ushirikiano unaostahiki.
Mhe. Hemed aikiwa katika ziara yake hiyo aliwashauri wawekezaji hao kuweka mazingira mazuri ya kazi zao kwa kuajiri watu muhimu watakaotoa msaada kwa wamiliki wa viwanda hivyo akitolea mfano kuajiriwa kwa Mtu wa rasilimaliwatu pamoja na wahasibu kutasaidia kuweka sawa majukumu ya kazi.
Katika ziara yake hiyo Makamu wa Pili wa Rais aliwasisitiza wamailiki waliopewa nafasi katika eneo hilo la uwekezaji kwamba serikali ya awamu ya nane sio muumini wa kodi kubwa hivyo kile kiasi ambacho wanapaswa kulipia serikalini wachukuwe jitihada za maksudi katika kuhakikisha kodi hizo wanalipa ndani ya wakati stahiki.
“Serikali hii ni muumini wa kodi ndogo hivyo nawaomba sana ndugu zangu wawekezaji kusiwe na visingizio katika suala zima la ulipaji wa kodi kwa serikali”Alisema Makamu wa Pili
Aidha, Mhe. Hemed aliuagiza uongozi wa mamlaka ya uwekezaji Zanzibar kupitia upya sheria ya viwango vya kodi ili kila muwekezaji aweze kufahamu kiwango cha kodi anayostajiki kulipia bila ya kuathiri upande wowote ule.
Makamu wa Pili Rais alieleza faraja yake kwa jitihada nzuri zinazochukuliwa na uongozi wa mamlaka ya uwekezaji zanzibar katika kuhakikisha wawekezaji wanapewa maeneo ndani ya kipindi cha muda mfupi jambo ambalo linaashiria utayari kwa kuondoa urasimu na kuyafanyia kazi maelekezo ya Rais Dk. Mwinyi.
Akifanya majuumuisho baada ya ziara hiyo Mhe. Hemed alisema hakuridhishwa na baadhi ya mazingira katika eneo hilo kwa kufanywa jaa la kuhifadhia vifaa vilivyopitwa na wakati nakuahidi kuwa serikali itatoa maamuzi ndani ya kipindi cha muda mfupi.
Aliwagiza uongozi mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) pamoja Bodi ya mapato zanzibar kukaa pamoja na kuangalia upya taratibu za ulipaji wa kodi ili kuepusha serikali kupteza mapato yake kutoka kwa waekezaji.
“Lazima tupate mapato yanayoendana na wakati tulionao, kodi ile ya miaka ya zamani squre mita moja kwa Dola ishirini lazima tuingalie tena” Alisema Mhe. Hemed
Makamu wa Pili wa Rais aliwathibitishia wawekezaji wapya waliopewa maeneo hivi karibuni kuwa serikali inawakaribisha na wasisite kuwasilisha changamoto zozote zinazowakabili katika utendaji wa kazi zao.
Nae, Mkurugenzi wa Mamlaka ya kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) Ndugu Sharif Ali Sharif alimshukuru Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa ziara yake hiyo ambayo imekuwa ni chachu kwa mamlaka hiyo kuweza kufanyakazi kwa bidii ili kufikia lengo la serikali ya Awamu ya Nane la kukuza uwekezaji nchini.
Pamoja na mambo mengine Mkurugenzi Sharif alimueleza Makamu wa Pili wa Rais kuwa maelekezo aliyoyatoa watahakikisha wanayachukulia hatua kwa ushirikiano kati ya Mamlaka hiyo na wizara ya nchi afisi ya rais uchumi na uwekezaji.
Nao wawekezaji wa waliopewa nafasi ya kuekeza katika eneo hilo la viwanda vidogo vidogo wameipongeza Serikali ya Awamau ya Nane chini ya uongozi wa Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji ambayo yamewasaidia kuendesha kazi zao bila ya usumbufu.
Aidha, wawekezaji hao walishauri Serikali kupitia mamlaka ya uwekezaji zanzibar kuaanda majengo kwa kuyakarabati ili yaweze kutoa fursa kwa wawekezaji wanapofika nchini kufunga vifaa vyao na kuanza kazi moja kwa moja.
Eneo la uwekezaji la viwanda vidogo vidogo Amani limeanza rasmi kufanyiwa shughuli za uwekezaji tangu mwaka 1976 ikiwa ni adhama ya Rais wa awamu wa kwanza Sheikh Abeid Amani Karume la kuhakikisha Zanzibar inapiga hatua katika uwekezaji kupitia sekta ya viwanda.
Kassim Abdi
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment