Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT wazalendo Zanzibar Juma Duni Haji amewahimiza wafuasi wa chama hicho ambao hawajapata kitambulisho cha Uzanzibar ukaazi (zan ID) kufuatilia ili waweze kupata haki yao hiyo ya kikatiba.

Haji  alitoa wito huo  kwa nyakati tofauti wakati wa ziara ya kumtambulisha Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Othman Masoud Othman  kwa Viiongozi wa Mikoa, Majimbo pamoja na Matawi mkoa wa kusini Unguja katika Maeneo ya Makunduchi na Dunga.

 

Alifahamisha kuwa wako vijana wengi tayari wamefikia umri  wa miaka 18 ambao kwa mujibu wa katiba ni lazima wapatiwe kitambulisho hicho lakini takwimu zinaonyesha waliowengi bado hawajapatiwa.

 Alifahamisha kuwa kama mtu hana kitambulisho hicho hawezi kupata chochote kile, hasa ajira katika visiwa vya Zanzibar.

“Nakuombeni muende mkaombe na kama mkizuiwa nileteeeni hao masheha waliokuzuieni” Alisema Haji ambaye anajuilikana kwa jina la Babu Juma.

Alisema kama vijana hao hawajafanya taratibu za kuomba Zan ID watakuwa wamejikosesha haki ya kikatiba katika nchi yao.

“Tulikuwa tukipata taabu sana katika kupata kitambulisho lakini mungu ameleta mabadiliko ya utawala na Waziri husika ametangaza kabisa kuwa hakuna sababu ya mtu kinyimwa kitambulisho twendenii” alisema Haji.

Aliwataka wananchi hao wasisubiri kipindi cha uchaguzi kwani kunaweza kuwa kugumu.

Aliwataka wananchi hao wahimizane katika kudai haki yao hiyo kwani waziri keshasema kuwa atakae zuiliwa aende afisini kwake kutoa taarifa ili aliyekwamisha achukuliwe hatua.

Alisema kuwa mtu mmoja mmoja itakuwa ngumu kwenda kwa waziri basi aliwaambia wafuasi hao kukusanya taarifa zotena kuzipeleka kwenye afisi za chama ili wachukue hatua.

Alisema kitambulisho hicho licha ya umuhimu wa mambo mengine pia kimekuwa kigenzo kikubwa katika kuwa mpiga kura Zanzibar na kueleza kwa sababu hiyo ni vyema wananchi na wanachama wote kukipigania kwa hali yoyote ile.

“Sisi tunania ya kuongoza nchi na hatuwezi kuongoza kama hatujashinda uchaguzi na kama hatuna Zan ID hatuwezi kupiga kura kwa maana hiyo twendeni tukafanye maombi ili uchaguzi ukifika tuwe na wapiga kura wengi” alisema haji.

Akimkaribisha Mjumbe wa kamati Kuu wa chama hicho ambaye pia ni Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar  alimtaka kulichukulia hatua suala la baadhi ya masheha ambao huleta vikwanzo kwa wananchi kupata kitambulisho hicho.

Kwa upande wake Othman alisema kama ACT wanataka kuchukuwa nchi ni lazima wawe na Zan ID kwani ndizo zitakazowafanya wawe wapiga kura.

“Safari tunayokwenda tunahitaji chama madhubuti na mabadiliko yanaletwa na uchaguzi  na kama hatuna vitambulisho hatuweizi kupiga kura”  alisema Othman.

Alisema kutokana na umuhimu huo itakuwa busara sana kwenda kutafuta kitambulisho hicho kwa hali yoyote ili waweze kuwa wapiga kura katika daftari  la Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Mkurugenzi wa Mipango na Chaguzi wa chama hicho Omar Ali Shehe alisema huu ni wakati wakipigania haki hiyo ili wawe na nguvu ya kuiondoa ccm madarakani.

0 comments:

 
Top