Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdullah amewapongeza Wananchi wa Kijiji cha Dole kwa ushirikiano wao mkubwa unaochangia  sehemu ya utulivu wa Taifa uliyopo hivi sasa  Nchini.

Akisalimiana na Waumini na Wananchi wa Kijiji hicho mara baada ya kukamilisha kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa kwenye Msikiti wa Ijumaa wa Kijiji hicho Mheshimiwa Hemed Suleiman alisema Taifa linahitaji utulivu utakaotokana na Wananchi wenyewe unaohitajika kuelekezwa kwenye Maendeleo.

Alisema ushirikiano unaosisitizwa kila mahali ndio jambo la msingi litakaloiongezea nguvu Serikali katika muelekeo wake wa kuwaletea Maendeleo Wananchi wake kama ilivyoahidi wakati wa Kampenzi za kutangaza Sera kwa ajili ya kazi hiyo ya Utumishi.

Mheshimiwa Hemed Suleiman aliwaeleza Waumini na Wananchi hao wa Dole kwamba Serikali ya Mapinduzi chini ya Rais wake Dr. Hussein Ali Mwinyi imekusudia kudhibiti Mapato ya Taifa na kusisitiza kwamba hatua zinazoendelea kuchukuliwa hazikusudii kumkomoa Mtu.

Akiendelea kuikumbusha jamii juu ya uovu wa suala la Udhalilishaji linaloonekana kuiathiri Jamii kila wakati Mheshimiwa Hemed Suleiman alisema fursa ya dhamana kwa Watuhumiwa na vitendo hivyo imefutwa ili kuondosha unyama huo uliokithiri sehemu nyingi hapa Nchini.

Alisisitiza umuhimu wa mapambano dhidi ya vitendo vya utelekezaji, Ubakaji na udhalilishaji lazima yaanzie kwenye familia mitaani ili kunusuru kizazi kipya kinachotarajiwa kuwa dhamana katika usimamizi wa Utumishi wa Umma hapo baadae.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alibainisha kwamba suala la Mila na Utamaduni likiendelea kuimarishwa  litasaidia kurejesha Silka ya Watu wa Taifa hili zilizoleta sifa pembe zote za Dunia.

Akitoa mawaidha ya sala ya Ijumaa Mwanazuoni maarufu Nchini Sheikh Fadhil Suleiman Soraga alisema Amani na upendo unaoongozwa na ushirikiano ndio jambo la kutiliwa mkazo linaloibua mapenzi na kuondoa chuki baina ya Watu mahali popote pale.

Sheikh Soraga aliupongeza na kuushukuru mfumo ulioanzishwa na Rais wa Zanzibar Dr. Husein Ali Mwinyi na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla wa kujumuika na waumini wa Dini ya Kiislamu katika ibada ya Sala za Ijumaa Misikiti tofauti Nchini.

Alisema mfumo huo pamoja na mabo mengine unaowapata fursa Viongozi hao kutoa salamu pamoja na muelekeo wa Serikali wa kuwahudumia Wananchi unaongeza heshima, kuleta mapenzi pamoja na kupunguza joto la Kisiasa lililokuwa likiviathiri Visiwa vya Zanzibar kwa muda mrefu.

Akitoa shukrai kwa niaba ya Waumini na Wananchi wa Kijiji cha Dole Imamu wa Msikitiwa Ijumaa Sheikh Rashidi Salum Daudi alitumia fursa hiyo kumueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman changamoto zinazowakabili waumini na Wananchi hao.

Sheikh Rashid alizitaja changamoto hizokuwa ni pamoja na mwendo kasi wa vyombo vya moto vinavyotumia Bara bara hiyo wakipendekeza kuekewa matuta, mizozo ya Ardhi, Kabati la kuhifadhia Vitabu vya Dini kweye Msikiti huo pamoja na hitilafu ya huduma za Maji zinazotokana na kuvuja kwa Bomba la Maji sehemu hizo.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewaagiza Wahandisi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar {ZAWA} kulifanyia marekebisho Bomba kubwa la kusambazia maji safi na salama liliopo pembezoni mwa Bara bara Mkabala na Msikiti wa Ijumaa wa Dole.

Mheshimiwa Hemed alionya kwamba kazi hiyo lazima ianze mara moja na hata kama Wahandisi hao watalazimika kukesha hapo hapo ilimradi Wananchi wa eneo hilo lazima warejee kupata huduma ya Maji safi na salama walioikosa kwa takiban miezi Mitatu sasa kutokana na hitilafu hiyo.

Alisema haiwezekani kuona lita kadhaa za maji safi na salama kikiendelea kupotea  Mitaani huku Wananchi wakipata changamoto ya kukosa huduma hiyo muhimu kwa ustawi wa Jamii.

Mapema Sheha wa Shehia ya Dole Mzee Hamdani Marejeo alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba hitilafu hiyo ya kupotea kwa maji safi kutokana na kupasuka kwa Bomba hilo hivi sasa ina miezi Mitatu na tayari wameshachukuwa hatua za kuiarifu Mamlaka iliyosimamia Rasilmali hiyo lakini bado hakuna jitihada zilizochukuliwa.

Mzee Marejeo alisema inashangaza kuona Miti na Migomba iliyopo sehemu hiyo inaendelea kunawiri wakati wale waliokjusudiwa kuipata huduma hiyo wamekuwa wakisumbuka kwa kipindi chote.

 Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top