Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla alisema uamuzi wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli wa kuutaka Mfuko wa Tasaf kufanya Kazi maeneo yote ya Nchini  ni jambo la msingi litakaloleta ustawi Zaidi hasa kwa Wananchi wa Kaya Maskini.

Alisema Watanzania walio wengi wanaendelea kushuhudia jinsi Mfuko huo wa Maendeleo ya Jamii Tanzania ulivyokomboa maisha ya Wananchi wa kipato cha chini na kwa sasa baadhi wao wameanza kujihakikishia upataji wa mahitaji yao ya msingi.

Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla alieleza hayo wakati akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania Nd. Ladislaus Mwamanga alipofika Afisini kwake kuelezea Mikakati ya Mfuko huo kwa Awamu ya Tatu ya utekelezaji wake.

Alisema upo ushahidi wa wazi katika uimarikaji wa Miradi mbali mbali ya Maendeleo ya Jamii akitolea mfano Sekta ya Elimu baada ya kupata msukumo kupitia Mfuko wa Tasaf ambapo hata takwimu za idadi ya uandikishaji wa Wanafunzi wa Elimu ya msingi imepanda sana.

“ Ukweli nimefarajika na kukiri kwamba Wananchi Wananchi wengi wa Kaya Maskini hasa Vijijini wamefaidika na matunda ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania”. Alisisitiza Mh. Hemed.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema wakati kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu Tasaf kimeshaanza kuonyesha muelekeo mzuri katika utekelezaji wake, aliuhakikishia Uongozi huo wa juu wa Mfuko huo kwamba Ofisi yake kama Msimamizi Mkuu kwa upande wa Zanzibar itaongeza ushirikiano Zaidi ili malengo ya mfuko huo kufikia maeneo yote yalete tija.

Mheshimiwa Hemed aliupongeza mfumo Mpya wa Teknolojia ya sasa ya Mtandao katika utoaji Fedha utakaotumiwa na Mfuko huo katika Awamu ya Tatu Kipindi cha Pili cha Tasaf.

Amewataka Watendaji wote watakaohusika na Uekelezaji wa Miradi ya Tasaf Kipindi cha Pili lazima wazingatie vyema masuala ya uadilifu katika majukumu watakayopangiwa.

Mh. Hemed alisisitiza kwamba  Zanzibar itaendelea kujitahidi kufanya vizuri Zaidi kwenye Utekelezaji huo na pale itakapojichomoza changamoto yoyote hatua za haraka zitachukuliwa ili kuleta ufanisi uliokusudiwa.

Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {Tasaf} Nd. Ladislaus Mwamanga alisema Jumla ya Wana Kaya Elfu 1,320 Tanzania Bara na Zaidi ya Mia Moja upande wa Zanzibar wametosheka na Mradi ya Kaya Maskini ambapo wameamua kujitoa baada ya Maisha yao kubadilika.

Nd. Mwamanga alisema Tasaf imekamilisha zoezi la uhakiki kwa Wananchi wa Kaya Maskini ikilenga maisha ya Wanajamii wa Kaya Maskini lazima yabadilike katika kuimarisha Uchumi ndani ya Kaya hizo.

Alisema hatua ya kuvijengea uwezo wa Taaluma Vikundi vya Kuweka na kukopa  utazingatiwa kwa vile takwimu zinazonyesha kwamba eneo hilo lina mchango mkubwa wa kupunguza umaskini.

Nd. Ladislaus Mwamanga alisisitiza kwamba kwa vile miradi mingi inayoanzishwa kupitia mfuko huo itakuwa endelevu Wananchi wanaosimamia miradi hiyo lazima wafanye kazi ya ziada katika kufanikisha uwajibikaji wake.

Mkurugenzi Mkuu huyo wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {Tasaf} aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Wananchi wake kwa hatua kubwa iliyofikiwa ndani ya miradi ya Tasaf na matokeo yake Zanzibar imekuwa mfano katika utekelezaji wake.

 Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top