Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze, ametajwa na Apoliticial pamoja na taasisi ya World Economic Forum’s Global Future Council on Agile Governance kama mmoja wa watu 50 wenye ushawishi mkubwa ulimwenguni wanaohamasisha mageuzi ya kiutawala. Eyakuze ni mmoja wa Waafrika watatu tu kwenye orodha hiyo na mmoja wa watu kumi na moja ambao sio watumishi wa serikali.


Orodha ya watu 50 wanaohamasisha maboresho na mageuzi ya kiutawala imekusanywa kutokana na mapendekezo ya wataalamu, kisha utafiti kufanywa kwa  waliopendekezwa na baadaye mapendekezo hayo kupitiwa na taasisi ya World Economic Forum. Washiriki huchaguliwa kutokana na sifa mbalimbali za uongozi zikiwemo: kuweka msisitizo kwenye matokeo, ubunifu na kufanya majaribio, pamoja na mahusiano na wadau kijamii, kitaifa na kimataifa. Aidan Eyakuze alichaguliwa kama mmoja wa watetezi bingwa wa wananchi wa kawaida.

 

Orodha hiyo ina lengo la kuangazia wanasiasa, watumishi wa umma na wajasiriamali wanaoweka msukumo wa mabadiliko katika serikali kote ulimwenguni. Kabla ya janga la Covid-19, serikali zilikuwa zinatafuta namna ya kutumia fursa za ubunifu pamoja na kupunguza athari zake. COVID-19 imekuza changamoto hii, na kuongeza umuhimu wa serikali zote duniani kuwezesha mbinu mpya za kukabiliana na mtikisiko wa kijamii na kiuchumi.

 

Apolitical ni mtandao wa watumishi wa umma katika nchi zaidi ya 160. Jukwaa hilo ambalo limebuniwa na kufadhiliwa na serikali mbalimbali, huandaa hafla, mikutano ya wadau, mafunzo na makala kwa watumishi wa umma ambazo husaidia katika utekelezaji wa majukumu yao.

 

Baraza hilo la mabadiliko ya utawala hukutanisha wataalamu kutoka upande wa wafanyabiashara na serikali ili kusukuma mageuzi ya kiutawala yanayochochea ubunifu na kukuza ukuaji wa uchumi.

 

Aidan Eyakuze alisema: “Ni heshima kubwa kujumuishwa katika orodha hii ya wanamageuzi wa kiutawala. Inatia moyo sana kuona majina ya watumishi wa umma kutoka nchi mbali mbali ambao wanaamini kwamba serikali hufanya kazi vizuri pale inapokuwa wazi, bunifu na sikivu. Wananchi wanapokuwa na uhuru wa kujieleza, kuchangia mawazo bunifu an kufanya kazi kwa umoja, ndipo wanapojiletea maendeleo.. Najivunia kuwa sehemu ya harakati za wabunifu wanaoshawishi utawala mpya  unaowaheshimu na kuwajibika kwa wananchi"

0 comments:

 
Top