Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejizatiti kuimarisha Makaazi bora ya Wananchi wake kwa ujenzi wa Nyumba za Kisasa ili kwenda sambamba na Falsafa ya Chama cha Afro Shirazy Party ya kuhakikisha ustawi wa Jamii unakuwa katika kiwango kinachokwenda na wakati.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo mara baada ya kukagua maendeleo ya Mradi wa ujenzi wa Nyumba za Kisasa katika Mtaa wa Kwahani zitakazostawisha Maisha bora ya Wananchi wa eneo hilo.
Balozi Seif alisema fikra za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein katika kuona Maendeleo ya Makaazi ya Wananchi yanaimarika yamezingatia mawazo ya Rais wa kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.
Alisema jitihada hizo za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zinaonyesha wazi kwamba maeneo yote ya Zanzibar Mijini na Vijijini kwa sasa yanakaribia kuwa na fursa na huduma zote muhimu zinazostahiki kuzipata Mwanaadam hali inayoonyesha kupungua kwa mitaa ya ng’ambo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwahakikishia Wananchi kwamba Nyumba zinazojengwa Mtaa wa Kwahani zimelengwa kupewa Wananchi waliovunjiwa nyumba zao katika maeneo hayo.
“ Nyumba hizo hatopewa Mtu mwengine Zaidi ya Wakaazi wa Kwahani na vizuri kwamba kumbukumbu zao zote zimehifadhiwa Serikalini na wala hazipangishwi kama baadhi ya Watu wanavyofikiria”. Alisisitiza Balozi Seif.
Alielezea faraja yake na inapendeza kuona kwamba Wahandisi pamoja n Washauri Elekezi wanaosimamia miradi mbali mbali ya Miundombinu ya Ujenzi hapa nchini inaendeshwa na Wazalendo wenye bila ya ushiriki wa wataalamu wa kigeni.
Akitoa Taarifa ya Mradi wa Ujenzi wa Nyumba hizo za Kwahani Mshauri Elekezi wa Ujenzi huo Mhandisi Andrian Eradius ujenzi huo unaendelea kwa Mabloki Matatu yanayokadiriwa kuwa na uwezo wa kuhudumia Familia 70 pamoja na sehemu za Maduka kwa Wale Wananchi waliokuwa na miradi katika eneo hilo.
Mhandisi Adrian alisema harakati za ujenzi wa majengo hayo hivi sasa ziko asilimia 98% kwa Bloki C, Asilimia 95% Bloki B na lile Bloki A kazi zinaendelea kwa hatua ya uwezekaji paa.
Mshauri Muelekezi huyo wa Mradi wa Nyumba za Kwahani aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Waziri wa Fedha na Mipango kwa jitihada ilizochukuwa za kuwapatia ushirikiano hasa kaika changamoto iliyojitokeza na uhaba wa Mchanga katika kuendeleza kwa wakati Ujenzi huo.
Alisema Mradi huo ulipangwa kukabidhiwa Serikalini Mwezi huu lakini kutokana na sababu za kuibuka kwa maradhi yanayosababisha homa kali ya mafua {Corona} mradi huo sasa unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa Mwezi wa Septemba Mwaka huu.
Mapema Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Balozi Mohamed Ramia alisema Wananchi wa Mtaa wa Kwahani ndio walengwa watakaofadikiwa na mradi huo na haitapendeza kuja kuona ndani ya kipindi cha Miezi sita makaazi hayo yanakaliwa na Watu wa nje ya Mtaa huo.
Balozi Ramia alisema Majengo hayo yatakapokamilika yatakuwa na uwezo wa kuhudumia Familia Sabini ingawa zilizopo kwenye kumbukumbu ni Familia 40. Hivyo zile nyumba zitakazobakia zitawahudumia wale Wananchi watakaovunjiwa katika Awamu ya Pili na Tatu ya Mradi huo.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment