Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameipongeza Kampuni ya Uwekezaji ya Basra Textile Milles kwa kazi kubwa ya kukifufua upya Kiwanda cha nguo cha Cotex kilichopo Mtaa wa Chumbuni inayokweda sambamba na azma ya Serikali ya kuimaisha Sekta ya Viwanda Nchini.
Akifanya ziara fupi ya kukagua maendeleo ya uimarishaji wa miundombinu ya Kiwanda hicho inayotarajiwa kukamilika mwezi Oktoba mwaka huu kwa Awamu ya kwanza Balozi Seif alisema hiyo ni kazi nzuri ambayo faida itakayopatikana itasaidia sio kwa wawekezaji bali kwa Taifa na Vijana katika suala la ajira.
Alisema kiwanda cha Cotex kwa miaka mingi kimekuwa eneo la magofu lililokuwa likilalamikiwa na Wananchi kwa kutoendelezwa licha ya Serikali Kuu Kiwanda hicho kumpa Muwekezaji aliyeshindwa kukiendeleza kwa Zaidi ya Miaka 25 iliyopita nyuma.
Balozi Seif alisema nia thabiti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuwashawishi Wawekezaji wa ndani na nje ya Nchi kuanzisha miradi ya Kiuchumi itakayosaidia kutoa ajira kwa kundi kubwa la Vijana sambamba na kuongeza Mapato ya Taifa.
Aliushauri Uongozi huo wa Kampuni ya Uwekezeaji wa Basra Textile Milles kujitahidi kuzalisha bidhaa zenye kukidhi viwango vya masoko ya Kitaifa na Kimataifa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuhakikishia Uongozi huo kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kuendelea kutoa msukumo ili kuona malengo ya kuanzishwa Mradi huo kwa vile yanawagusa Wananchi moja kwa moja yaweze kufanikiwa.
Mapema akimtembeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi katika maeneo mbali mbali ya Kiwanda hicho Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda hicho Bwana Ahmed Osman Osman alisema harakati zinazoendelea hivi sasa ni ufungwaji wa mashine ili kukamilisha Awamu ya Kwanza.
Bwana Osman alisema majaribio ya kwanza wa uzalishaji wa Kiwanda hicho unatarajiwa kuanza rasmi Mwezi Oktoba mwaka huu kwa hatua za uzalishaji wa Vitenge, Vitambaa vya sare za Skuli, Mashuka ya Vitanda vya Majumbani na hata Mahotelini.
Alisema hatua hiyo ya awamu ya kwanza itawezesha bidhaa zitakazozalishwa mbali ya kutumika Nchini lakini pia mpango umeshatayarishwa wa nyengine kuuzwa katika Mataifa ya Magharibi mwa Bara la Afrika.
Naye kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Basra Textile Milles Bwana Said Hassan alimueleza Balozi Seif kwamba Awamu ya kwanza iliyochukuwa gharama za Dola za Kimarekani Milioni 21.3 itawezesha kutoa ajira 454 za Wafanyakazina Awamu ya Pili Wafanyakazi 1,200.
Bwana Said Hassan alisema Awamu ya Tatu itakayotoa ajira 1,600 itakwenda sambamba na ununuzi wa zao la Pamba kutoka Tanzania bara ili kuimarisha uwezo wa Wakulima Wazalendo.
Alifahamisha kwamba yapomatumaini makubwa ya ubora wa mashine zilizopo kuzalisha bidhaa za kiwango cha juu kwa asilimia 90% kitakachosafirishwa katika masoko ya Nchi za Umoja wa Ulaya na Marekani.
Akitoa shukrani katika ziara hiyo Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Balozi Mohamed Ramia aliuhakikishia Uongozi wa Kiwanda hicho kwamba Serikali kupitia Wizara hiyo inazingatia kuzipatia ufumbuzi changamoto ndogo ndogo zilizojitokeza wakati wa harakati za uimarishaji wa Kiwanda hicho.
Balozi Ramia alisema Kiwandi hicho kilichoanza kuwa tegemeo kubwa la ajira kwa kundi la Vijana ni eneo muhimu litaloleta faida kwa Wananchi wa Visiwa vya Zanzibar.
Waziri wa Fedha alielezea matumaini yake kwamba wale wafanyakazi Wahandisi waliomo ndani ya Taasisi za Serikali wakati umefika wa kutumia Taaluma yao katika Sekta ya Viwanda inayozidi kuimarishwa hapa Nchini.
Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment