Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba wakati umefika kwa Skuli za Zanzibar kutumia Mpango Kazi ambao Uongozi wa Skuli husika unapaswa ukusanye matokeo mara baada ya vijana wao kufanya mitihani ili kufanya uchambuzi utakaobainisha maeneo yanayotakiwa kufanyiwa kazi.

Alisema Uongozi wa Skuli ukijipanga upya kwa kushirikisha Wanafunzi katika kukabiliana na mapungufu yaliyozorotesha matokeo ya wanafunzi waliopita kazi ya kutekeleza yale yaliyokubalika wakati wa tathmini hiyo inakuwa rahisi na kuleta mafanikio makubwa.

Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda alieleza hayo katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Riziki Pembe Juma wakati wa hafla maalum ya kuwapongeza Wanafunzi waliofanya vizuri katika Mitihani yao ya Taifa ya Kidato cha Pili na cha Nne katika Skuli ya Sekondari ya Mahonda.

Alisema Utaratibu au Mpango Kazi huo wa kupata mafanikio endelevu ya Elimu { Systematic Quality Work } ukifuatwa ipasavyo kila mwaka utasaidia kunyanyua ufundishaji na hatimae Skuli za Zanzibar zitanyanyua viwango vya ufaulu.

Balozi Seif alisema ni jukumu la Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kuhakikisha kwamba Skuli zote Nchini zinawekewa utaratibu maalum wa kuzipima kila mwisho wa Mwaka kwa lengo la kunyanyua ubora wa Skuli zote Visiwani Zanzibar.

Aliwapongeza Wanafunzi wote wa Skuli ya Sekondari ya Mahonda waliofaulu vizuri mitihani yao na kusema kwamba mafanikio yaliyopatikana hayakuja kama mvua bali ni matunda ya mshikamano yaliyoonyeshwa baina ya Walimu, Wazee Kamati ya Skuli pamoja na Wanafunzi wenyewe.

Hata hivyo Balozi Seif aliwanasihi wanafunzi wasiofaulu mitihani yao wasivunjike moyo kwani milango ya kujiendeleza zaidi kielimu hapa Nchini ipo mingi ambayo hutowa fursa kwa wanafunzi hao kuendelea na mafunzo mengine ya kujijengea hatma njema ya maisha yao ya baadae.

Alifahamisha kwamba wapo watu wengi Nchini ambao hawakufaulu katika Mitihani yao ya Taifa kwa mara ya kwanza lakini hawakukata tamaa na badala yake walifanya jitihada ya kujiendeleza zaidi na hivi sasa baddhi yao wanahesabiwa kuwa wataalamu katika fani za Ualimu, Udaktari na hata Kilimo.

Aliwanasihi Wazee kujitahidi katika kuwashajiisha Vijana wao kupenda elimu na pale wanapofanya vizuri katika mitihani hiyo Wazee wanapaswa kujenga Utamaduni wa kuwazawadia vijana hao ili kuwatia moyo zaidi.

Balozi Seif Ali Iddi aliushukuru Uongozi wa Skuli ya Mahonda pamoja na Kamati ya Wazazi ya Skuli hiyo kwa uamuzi wake wa busara wa kutenga siku maalum ya kuwapongeza Vijana wao waliofaulu vyema katika Mitihani yao ya Kidato cha Pili na Cha Nne.

“ Nawapongeza kwa dhati wale wote waliosaidia kufanikisha hafla hii ya wanafunzi wetu, wakiwemo Walimu Wazazi, Kamati ya Skuli na wale wote ambao sikuwataja”. Alisisitiza Balozi Seif.

Alieleza kwamba Utamaduni huo ni mzuri na ni vyema ukaendelezwa katika miaka mengine ijayo kwa vile unasaidia kupatikana kwa maendeleo ya kielimu yanayokuwa endelevu katika muda wote.

Akisoma Risala ya Walimu, Wanafunzi na Wazazi wa Skuli ya Mahonda Mwalimu wa Sekondari wa Skuli hiyo Mwalimu Dadi Salim Rashid alisema kiwango cha ufaulu kwa Wanafunzi waliofanya mitihani ya Kidato cha Pili na cha Nne kimeongezeka ikilinganishwa na Miaka iliyopita nyuma.

Mwalimu Dadi alisema idadi ya Wanafunzi waliofaulu kwa Kidato cha Pili imefikia wanafunzin106 kati ya Wafafunzin177 waliofanya mitihani wakati Kidato cha Nne Mwanafunzi pekee wa Daraja la Pili ndani ya Wilaya ya Kaskazini B ametokea Skuli hiyo ya Sekondari Mahonda.

Alisema Wanafunzi 50 wa Daraja na Nne na 6 wa Daraja la Tatu wamefanikisha kuinawisha uso skuli hiyo ya Mahonda ambayo kwa kipindi kirefu imekuwa ikizorota katika ufaulu wa wanafunzi wake.

Hata hivyo mwalimu Dadi alisema Skuli ya Sekondari ya Mahonda bado inakabiliwa na changamoto kadhaa zinazozorotesha ufanisi wa kufanya vizuri wanafunzi wake akizitaja baadhi yake kuwa ni pamoja na uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi na kutomalizika kwa ukumbi wao wa Mitihani.

Mapema Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “B” Nd. Issa Juma Ali alisema sababu zinazopelekea wanafunzi kukosa kufaulu mitihani yao ni dhima inayobebwa na Wazazi ambao baadhi yao hupenda kuisukumia lawama Serikali Kuu iliyokwisha toa muongozo.

Nd. Issa alisema Viongozi wa Kamati za Maskuli wanapaswa kufanya juhudi za ziada katika kuwatafuta Vijana wa Mitaani waliopata elimu ya kutosha ili watenge muda wa kusaidia masomo ya ziada kwa wanafunzi wanaojiandaa kufanya mitihani yao ya Taifa.

Katika hafla hiyo Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Riziki Pembe Juma alikabidhi Mashine ya Fotokopi kwa skuli ya Sekondari ya Kitope iliyotolewa na Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi kukamilisha ahadi aliyotoa kwa uongozi wa Skuli hiyo miezi michache iliyopita.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top