Mabalozi wanayoiwakilisha Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mataifa Rafiki Ulimwenguni wataendelea kuwa na jukumu la kuitunza Heshima ya Tanzania katika misingi imara itakayoimarisha Uhusiano mzuri uliopo kati ya pande hizo mbili.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake Vuga wakati akiwaaga Mabalozi Saba wapya wa Tanzania walioteuliwa hivi karibuni kuiwakilisha Nchi katika Mataifa tofauti Duniani uliofanywa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli.

Balozi Seif Ali Iddi alisema yapo mafungamano mazuri ya muda mrefu yaliyopo baina ya Tanzania na Nchi Rafiki ambazo Wanadiplomasia hao wa Tanzania wana kazi kubwa ya kuhakikisha kwamba uwajibikaji wao unaleta tija na faida kwa mafungamano hayo katika pande zote mbili.

Balozi Seif aliwaeleza Mabalozi hao kwamba Mataifa ya Qatar, Oman, Uganda, Kenya, Belgium na Korea Kusini yamekuwa mshirika mkubwa na Tanzania katika kuimarisha Sekta za Maendeleo zinazosaidia kustawisha maisha ya Wananchi.

Alisema Zanzibar ikiwa ni sehemu ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania inahitaji kuendelea kuungwa mkono na Mashirika na Taasisi za Mataifa hayo ambapo Mabalozi hayo watakuwa na jukumu la kufanya ushawishi utakaopelekea azma hiyo inafanikiwa vyema.

Akigusia Nchi ya Sudan ambayo Tanzania imeamua kufungua tena Ubalozi wake baada ya kuufunga katika miaka ya 90 kutokana na hali ngumu ya uchumi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimtaka Balozi atakayesimamia Ofisi hiyo kufanya juhudi katika kuhakikisha fursa za masomo zilizokuwa zikitolewa na Nchi hiyo zinarejea kama kawaida.

Alisema Sudan ni Nchi iliyokuwa ikiifadhili na kuisaidia sana Tanzania na Zanzibar kwa jumla nafasi nyingi za masomo hasa katika fani za Elimu ya Dini ya Kiislamu na Historia.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Mabalozi wenzake Balozi wa Tanzania Nchini Oman Balozi Abdulla Kilima alisema jukumu walilokabidhiwa na kukubali kulibeba watahakikisha wanalitekeleza kwa nguvu zao zote.

Balozi Kilima kwa niaba ya wenzake wamewaahidi Watanzania kwamba watazingatia kuilinda Heshima iliyopo ya Taifa lao inayoendelea kushamiri katika Nyanja za Kimataifa.

Mabalozi aliyozungumzao nao Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na kuwaaga ni pamoja na Balozi Pindi Chana anayekwenda Nchini Kenya, Balozi Silima Kombo Haji anayekwenda Sudan na Balozi Joseph Sokoine anayekwenda Nchini Belgium.

Wengine ni Balozi Abdulla Kilima anayeiwakilisha Tanzania Nchini Oman, Balozi Matilda Masuka atakayekwenda fungua Ubalozi Mpya Nchini Korea Kusini, Balozi Grace Mgwano anayekwenda Nchini Uganda na Balozi Fatma Rajab anayekwenda Nchini Qatar.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top