Na Jumbe Ismailly-Mkalama

SHIRIKA lisilokuwa la kiserikali linalojishughulisha na utoaji wa huduma za maji safi na salama nchini la Life Time Wells kwa kushirikiana na serikali za vijiji katika Halmashauri ya wilaya ya Mkalama wametumia zaidi ya shilingi milioni 400 kuchimba visima vya mdundiko 37 katika Halmashauri ya wilaya hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya wilaya ya Mkalama,Bwana Gedfrey Sanga aliyasema kwenye mkutano wa hadhara wa Kijiji cha Ilunda,wakati alipokwenda kuwasalimia wananchi waliokuwa kwenye mkutano ulioitishwa na diwani wa kata ya Ilunda,Bwana Mohammed Imbele.

Aidha Bwana Sanga alifafanua kwamba kati ya kiasi hicho cha fedha kilichotumika,Shirika hilo limetumia shilingi milioni 481 na serikaali za vijiji shilingi milioni 37 na kwamba wafadhili hao wanachimba visima vya mdundiko kwa masharti kuwa kila kijiji kuchangia shilingi milioni moja.

Hata hivyo baada ya kukamilisha uchimbaji wa visima hivyo,Mkurugenzi mtendaji huyo aliwahakikishiaa wananchi hao kwamba wafadhili hao watarudi tena wilayani hapa mwezi januari,mwaka ujao na hivyo endapo watakuwa wamekamilisha michango yao watawekwa kwenye orodha ya kuchimbiwa visima wanavyovihitaji.

Kwa mujibu wa Bwana Sanga Halmashauri hiyo itasaidia kutoa wataalamu kwa ajili ya kwenda kutoa mafunzo kwa mafundi wa Kijiji ili kisima kinapokuwa na matatizo waweze kusaidia kutengeneza wao wenyewe badala ya kutegemea mafundi kutoka nje ya Kijiji.

Awali akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ilunda,diwani wa kata ya Ilunda,Bwana Mohamedi Imbele alikiri kuifahamu kero ya upatikanaji wa maji,na kwamba ameshaanza kuishughulikia kwa kuiomba Kampuni ya mawasiliano ya simu za mkononi ya Airtel,iwachimbie visima katika vijiji vya Iambi,Ilunda pamoja na Nkungi.

“Ofisi yangu imefikia uamuzi wa kukuandikia barua ya ombi hili kutokana na kuona kuwa Kampuni hii ipo karibu sana na jamii,hivyo ni vizuri kutusaidia kutatua changamoto hii kwa wananchi wa kata ya Ilunda na kwa kuwa ninyi ni wadau wakubwa wa maendeleo”alisisitiza diwani Imbele.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi,Bwana Edward Mtaturu,Bwana John Daaudi na Bwana Charles Mpinga pamoja na kutaka kufahamishwa juu ya utaratibu utakaotumika kuchimbiwa visima hivyo lakini walilalamikia pia kutokamilika kwa muda mrefu kwa ujenzi wa Kituo chao cha afya.

Kwa mujibu wa Bwana John Daudi mradi wa ujenzi wa kituo hicho cha afya umeanza tangu mwaka 2008 na mpaka sasa ni miaka minane hakijakamilika,licha ya kuchangia nguvu zao bila mafanikio na kuomba wapetiwe majibu yatakayoonyesha ni lini wataanza kupata huduma katika kijiji hicho.

Wananchi wa Kijiji cha Ilunda,tarafa ya Nduguti hulazimika kufuata huduma ya maji safi na salama umbali wa kilomita tatu kutoka wanapoishi,licha ya sera ya taifa inayomtaka kila mwananchi kupata huduma hiyo kwa umbali usiozidi mita 400 kutoka nyumbani kwake

0 comments:

 
Top