Na Jumbe Ismailly- Singida 

MAADHIMISHO ya sherehe za Kitaifa za Maulid ya Mtume Mohammad (SAW) kwa mwaka huu zinatarajiwa kufanyika Mkoani Singida katika Kijiji cha Shelui,wilaya ya Iramba,Mkoani Singida.

Katibu wa Bakwata Mkoa wa Singida,Alhaji Buruhani Mlau aliyasema hayo wakati akiongea kwenye ofisi za Bakwata Mkoa wa Singida na wenyeviti na makatibu wa matawi,maimamu wa misikiti wa wilaya ya Singida pamoja na masheikh kutoka katika wilaya ya Singida vijijini.

Alhaji Mlau alifafanua kwamba BAKWATA makao makuu kwa kupitia barua ya Katibu mkuu wake ya Feb,11,mwaka huu wameupatia heshima Mkoa wa Singida kuwa mwenyeji wa maadhimisho ya sherehe hizo

“Napenda kuwataarifu kuwa Bakwata Makao makuu taifa kupitia barua ya katibu mkuu wa taifa yenye kumbu kumbu imeandikwa hapa ya tarehe 11,feb,mwaka huu wametupatia heshima ya kuwa wenyeji wa maadhimisho ya maulidi ya Mtume wetu(SAW) kitaifa katika Mkoa wetu wa Singida, wilaya ya Iramba mwaka huu wa 2016”alifafanua katibu huyo.

Hata hivyo Alhaji Mlau alitumia fursa hiyo kuomba ushirikiano wa dhati kutoka kwa viongozi,waislamu wa ngazi zote pamoja na wadau mbali mbali ili kufanikisha sherehe za maadhimisho hayo yanayotarajiwa kufanyika mwezi disemba,2016.

“Kipekee tunawashukuru waislamu,viongozi pamoja na wadau mbali mbali wa wilaya ya Iramba kwa dhamira yao ya ushirikiano walioanza kuuonyesha kwa kupokea na kuanza maandalizi”alisisitiza Mlau.

Aidha Katibu huyo aliweka bayana kwamba kwa kuwa heshima hii ni ya Mkoa mzima,hivyo wilaya zote ukiondoa wilaya ya Iramba zinaagizwa kuchangia shilingi 1,500,000/= na kuziwasilisha kabla ya nov,30,mwaka huu na kukatiwa stakabahi stahili.

Alhaji Mlau hata hivyo alisisitiza kwamba pamoja na majukumu mengine,kila katibu wa wilaya akishirikiana na walezi katika wilaya awasilishe mapema kwa katibu wa Mkoa miradi ya baraza watakayoona ni vyema ikafunguliwa ama kuzinduliwa na viongozi kutoka makao makuu kupitia sherehe hizo.

0 comments:

 
Top