Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Viongozi na Watendaji wa Taasisi na Mashirika ya Umma wana wajibu wa kubadilika na kubuni mbinu zitakazowezesha kuongeza mapato kwa Taasisi hizo kwa faida ya Taifa na Jamii kwa jumla.

Amesema Serikali Kuu haiwezi kuleta maendeleo bila ya kuwa na vianzio madhubuti ambavyo ni pamoja na ukusanyaji wa mapato yanayokusanywa kupitia taasisi zilizopewa jukumu la kushughulikia makusanyo katika vianzio mbali mbali.

Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akizungumza na Wakurugenzi na Mameneja wa Matawi ya Benki ya Watu wa Zanzibar { PBZ }, Shirika la Bima { ZIC }, Shirika la Meli pamoja na Shirika la Taifa la Biashara Zanzibar { ZSTC } waliopo Tanzania Bara hapo katika jengo la Ofisi ya Uratibu wa shughuli za SMZ Mtaa wa Magogoni Jijini Dar es salaam.

Mkutano huo pia ulilenga kumtambulisha rasmi kwa Wakurugenzi hao Mkuu wa Ofisi ya Uratibu wa shughuli za SMZ Mjini Dar es salaam Ndugu Issa Mlingoti Ali aliyeteuliwa hivi karibuni na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein kushika wadhifa huo mpya.

Balozi Seif alisema Taasisi na Mashirika yanayosimamia fedha lazima yaongeze jitihada mara dufu katika ukusanyaji wa mapato ili kukidhi mahitaji na matarajio ya Taifa kwa vile hali ya fedha sio nzuri katika kipindi hichi.

Alisema suala hili ni vyema likaenda sambamba na matumizi bora ya fedha za Serikali na kuwataka Wakuu wa vitengo waendelee kusimamia vyema na kuwa wakali kwa kuwadhibiti watendaji waliokosa uaminifu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba wapo baadhi ya watumishi wa Umma wanaoendelea kukosa uaminifu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku na kuamua kujilimbikizia fedha na mali kinyume na taratibu na imani za Dini wanazozifuata.

“ Tumekuwa tukishuhudia ndani ya mashirika na Taasisi zetu za Umma kujichomoza Vijana wasio na maadili ya kazi na kuamuwa kujilimbikizia mali na fedha katika kipindi kifupi tokea wapate ajira na kuwakuta tayari wana uwezo wa kumiliki majumba na magari tofauti na kiwango wanachokipata katika mishahara yao ya mwezi ”. Alionyesha kusikitishwa kwake na tabia hiyo Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imeshaanza na utaratibu wa kupunguza matumizi ya fedha yasiyo ya lazima katika Taasisi zake kwa lengo la kupata nguvu ya utekelezaji kwa yale mambo yasiyo ya msingi na muhimu.

Aliwapongeza Viongozi na Watendaji wa Taasisi na Mashirika ya Umma yanayowajibika Tanzania Bara kwa jitihada wanazochukuwa katika kutoa huduma kwa Wananchi mbali mbali wa Tanzania sambamba na kukusanya mapato yanayosaidia Taifa.

Nao kwa upande wao Mameneja na Waguruigenzi hao wa Taasisi za SMZ zinazotoa huduma upande wa Pili wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania walielezea mafanikio na changamoto wanaopambana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao waliyopangiwa ya kila siku.

Meneja wa Shirika la Bima la Zanzibar Tawi la Dar es salaam Ndugu Imam Ally Makame alisema Uongozi wa Bodi ya Shirika hilo unaangalia maeneo ya Mikoa tofauti Nchini Tanzania ili iwekeze miradi yake kwa lengo la kujitanua katika kutoa huduma zao zinazokubalika na wateja mbali mbali.

Nd. Imam alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba mapato makubwa ya Bima yanayokusanywa na Shirika hilo yanapatikana katika Mikoa mbali mbali Tanzania Bara.

Alisema mafaniko hayo yamechangia kubuniwa mbinu za kuwasiliana na Taasisi nyengine za Fedha Zanzibar na upande wa Bara katika kuangalia namna ya kujenga jengo la kudumu litakalopunguza gharama kubwa zinazotumika kwa kukodi majengo ya huduma.

Kwa upande wake Menaja wa Benki ya Watu wa Zanzibar { PBZ }Tawi la Dar es salaam Ndugu Mohammed Bakari alielezea kwamba Benki hiyo kwa sasa haina mpango wowote wa kutaka kujenga majengo yake ya kudumu kwa upande wa Tanzania Bara.

Nd. Mohammed alisema hatua hiyo inakuja kutokana na sababu za Kibenki kulazimika kujenga Majengo yao kwa kutumia Mfuko wa Benki husika jambo ambalo kwa sasa nguvu zao wameamua kuendelea kuzielekeza katika biashara zaidi kwenye majengo ya kukodi.

Meneja wa Shirika la Meli Zanzibar Ndugu Salum Ahmad Vuai amemueleza Balozi Seif kwamba Uongozi wa Taasisi hiyo uko katika harakati za kutaka kujenga Jengo kubwa la ghirofa litakalokuwa Kitega uchumi cha shirika hilo katika Mtaa wa Magomeni Mjini Dar es salaam.

Nd. Ahmad alisema kinachoendelea kwa sasa ni Uongozi wa Shirika hilo kutafuta hati miliki katika eneo hilo ili wapate uhakika wa kuanzisha mradi huo baada ya kukamilika kwa mazungumzo na taasisi za fedha za Zanzibar kwa hatua ya mashirikiano katika ujenzi huo.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Frais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top