Na,Jumbe Ismailly-Singida
HALMASHAURI ya Manispaa ya Singida imetumia jumla ya shilingi 2,103,069,123/= katika ujenzi wa mradi wa maji unaofadhiliwa na Benki ya Dunia katika kipindi cha kuanzia mwaka 2012 hadi sasa.

Kiasi hicho cha fedha ni kati ya jumla ya shilingi 5,503,375,803/= zilizotarajiwa kutolewa na Benki ya Dunia kwa ajili ya mradi wa kuchimba visima kwenye vijiji kumi vya Halmashauri ya Manispaa ya Singida.

Kaimu Mhandisi wa maji wa Manispaa ya Singida,Niyok Gasto alisema hayo katika mahojiano maalumu na gazeti hili lililotaka kufahamu ni kiasi gani cha fedha zilizotolewa na Benki ya Dunia kwa ajili ya mradi wa maji uliopo katika vijiji kumi vyaa Manispaa hiyo.

Aidha mhandisi huyo alifafanua kuwa miradi ya vijiji sita vilivyopo katika awamu ya kwanza ya mpango huo wa Benki ya Dunia ulitarajiwa kutumia jumla ya shilingi……wakati kwa awamu ya pili ya mpango huo uliotarajiwa kuvihusisha vijiji vinne ulitengewa jumla ya shilingi……

Kwa mujibu wa Mhandisi huyo,vijiji vilivyokuwa katika mradi wa maji awamu ya kwanza ni pamoja na Kisaki,Mwankoko “A”,Mtipa.Mtamaa “B”,Ititi na Unyianga wakati kwa awamu ya pili alivitaja vijiji hivyo kuwa ni Mtamaa “A”,Uhamaka,Mwankoko “B” na Manga.
“Miradi iliyopangwa katika awamu ya pili ya mradi huu unaofadhiliwa na Benki ya Dunia katika vijiji vya Mtamaa “A”,Uhamaka,Mwankoko “B” na Manga hakuna hata mmoja ulioanza kutekelezwa kutokana na Benki ya Dunia kutoleta fedha za miradi hiyo mpaka sasa”alisisitiza Mhandisi huyo.

Kuhusu masharti yanayotakiwa ili Kijiji kiweze kupatiwa mradi wa maji kupitia ufadhili wa Benki ya Dunia,Gasto aliyataja kuwa ni pamoja na uhitaji wa wingi wa idadi ya watu,hali ya kijiografia ya Kijiji husika na uwepo wa vyanzo vya maji katika eneo husika.

Alisema katika kipindi chote tangu kuanza kwa miradi hiyo mwaka 2012 mpaka sasa ni miradi ya vijiji viwili tu ndiyo ambayo imekamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi kati ya miradi ya vijiji kumi iliyofadhiliwa na Benki ya Dunia katika Manispaa hiyo.

“Kwa miradi ambayo haijakamilika inatokana na upatikanaji hafifu wa fedha maana hela haziji kwa wakati unaotakiwa na zikipatikana ni pungufu na mpaka sasa ni shilingi 2,103,069,123/= zimetumika katika miradid hiyo na shilingi 3,276,124,140/= zimebakia”alisisitiza Mhandisi huyo wa maji Manispaa.

Katika hatua nyingine Mhandisi wa ujenzi wa Kampuni ya Exlent General Contractors Ltd ya jijini Dar-es-Salaam,Kagweza Kahendaguza ameulalamikia uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida kwa kushindwa kumlipa malipo ya awali ya kazi ya kuchimba kisima katika Kijiji cha Uhamaka.

Kwa mujibu wa mhandisi huyo pamoja na kufanyakazi kwa uaminifu lakini cha kushangaza mpaka sasa bado hajalipwa hata kiasi kidogo cha malipo yake ya awali na kila alipofuatilia aliambiwa kuwa Benki ya Dunia bado haijaleta fedha za miradi hiyo.

Hata hivyo Mhandisi Kahendaguza alifafanua kwamba licha ya kufanyakazi katika wakati mgumu,vile vile alimwazima mhandisi wa maji wa Manispaa hiyo,tofaali za kujengea tenki la maji katika mradi wake wa maji uliopo Kijiji cha Mtamaa,lakini mpaka sasa bado hajamrudishia.

Alisema baada ya kuambiwa hakuna fedha za kumlipa kutokana na kazi aliyofanya,ndipo aliamua kwenda ofisi za TAMISEMI kuulizia na alihakikishiwa kwamba Manispaa hiyo imepokea shilingi milioni 914 kwa ajili ya kuwalipa wazabuni wa miradi ya maji na alipokwenda kudai,jibu liliendelea kuwa hakuna kiasi chochote kilichopokelewa.

Kibaya zaidi mhandisi huyo alibainisha kuwa kutokana na mhandisi huyo naye kuwa na kampuni inayofanyakazi ya ujenzi wa kuchimba visima,hivyo aliamua kujilipa kwanza yeye kabla ya wazabuni wengine na kujikuta akimaliza kiasi cha fedha kilichopokelewa kwa ajili ya kazi hiyo.

Alibainisha pia kwamba baada ya kuitwa na mkurugenzi wa Manispaa hiyo na kuongea naye ana kwa ana aliahidiwa kulipwa kutokana na fedha kiasi kupokelewa na alipokwenda kwa mhandisi kwa ajili ya kusainiwa hati ya malipo yake,alikataliwa na kuambiwa hakuna fedha kwa wakati huo.

Hata hivyo alipotakiwa kuzungumzia malalamiko ya mzabuni huyo wa kampuni ya Exlent General Contractors Ltd,Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida,Joseph Mchina aliahidi kumaliza kero za wazabuni wa miradi ya maji katika kipindi kisichozidi wiki mbili na wala siyo zaidi ya muda huo.

0 comments:

 
Top