Na,Jumbe Ismailly-Itigi
MBUNGE wa jimbo la Manyoni magharibi (CCM),Yahaya Masare amewaagiza watumishi wa Halmashauri mpya ya Itigi kusimamia kwa karibu makusanyo na matumizi ya fedha zinazopatikana kutokana na vyanzo mbalimbali vya mapato yakiwemo mapato ya ndani ya Halmashauri hiyo.

Mbunge huyo alitoa wito huo kwenye mkutano wa kwanza wa uzinduzi wa baraza la madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Itigi,wilayani Manyoni uliofanyika mjini Itigi.

Aidha Masare hata hivyo huku akikwepa kumung’unya maneno kwa watendaji hao alifafanua kwamba kuna changamoto nyingi zilizopo katika Halmashauri ambazo hata kwenye Halmashauri hiyo hazina budi kuepukwa,hususani kwa upande wa kitengo cha makusanyo ya mapato ya ndani ya Halmashauri.

“Suala la makusanyo ya fedha za Halmashauri siyo kubwa mimi naomba nishauri Halmashauri kwenye kikao cha kwanza tujipange kutumia mfumo mpya wa ukusanyaji wa mapato,mnaanza lini lakini tuwe na mtazamo huo”alifafanua.

Alisisitiza mbunge huyo kwamba endapo Halmashauri itafanikisha kukusanya mapato yake ya ndani kwa kutumia mfumo huo mpya upo uwezekano wa kuwabaini watendaji wasiokuwa waaminifu wanaokusanya mapato kwa kutumia vitabu viwili tofauti.

Hata hivyo Mbunge Masare alitumia fursa hiyo pia kutoa taarifa kwa watendaji wa Halmashauri hiyo kwamba Halmashauri hiyo ni moja kati ya Halmashauri nchini zilizokumbwa na tatizo la janga la njaa.

“Sisi Halmashauri yetu ni miongoni mwa Halmashauri nchini ambazo zimekumbwa na janga la njaa,sisi Halmashauri ya Itigi ni miongoni mwa wakulima wazuri sana na mara zote huwa hatulii njaa mwaka huu mvua hazikunyesha kwa mtiririko mzuri kwa hiyo kuna baadhi ya maeneo,siyo yote yana shida ya njaa”alisisitiza kwa masikitiko makubwa.

Hata hivyo aliweka bayana kwamba yeye kama mbunge wao amelipigania suala hilo kwa kuanza walipoapishwa na mheshimiwa Raisi alipolihutubia Bunge,wiki iliyofuata alifanikiwa kupata tani mia mbili na ugawaji unaendelea na barua za namna ya kugawa zipo kwa Mkurugenzi mtenfaji.

Naye mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Itigi,Ally Minja akiwashukuru madiwani kwa kumchagua kuwa mwenyekiti aliwakumbusha juu ya umuhimu wa kudumisha umoja na mshikamano mara matokeo yanapotangazwa na kukubali kuwa aliyeshinda kashinda na kwamba naye ataweza kushinda kwa siku nyingine.

“Tuwe na umoja na mshikamano wa kweli na wa dhati kabisa na kukubali kabisa kwamba leo mwenzangu katangulia na mimi kesho nitatangulia,usipende sana kila atakayekutangulia ukawa na vita naye kwani tukianza kupambana wenyewe kwa wenyewe hakuna kitakachoendelea”aliweka bayana Minja.

Hata hivyo kwa mujibu wa Minja alitumia wasaa huo kuwaomba madiwani wenzake kwamba ni vyema wakapambana katika maendeleo badala na kupambana au kununiana kutokana na kukosa nafasi uliyotegemea kushika baada ya kutochaguliwa kushika wadhifa huo.

0 comments:

 
Top