Na,Jumbe Ismailly-Singida 

WATAALAMU wa Idara ya Mipangomiji katika Halmashauri ya Manispaa ya Singida wametakiwa kutekeleza mipango inayopangwa na wadau wa maendeleo na siyo kuifanyia mabadiliko,ili kuepuka dhana kwamba serikali imekuwa mstari wa mbele kupanga mipango isiyotekelezeka kikamilifu na kwa wakati uliopangwa.

Changamoto hiyo imetolewa na diwani wa kata ya Unyamikumbi,tarafa ya Mungumaji,katika Manispaa hiyo,Shabani Ikaku kwenye mkutano wa uwasilishaji wa mpango wa jumla (Master Plan) na kujenga uwezo juu ya utekelezaji wa miradi ya uendelezaji miji (ULGSP) uliofanyika kwenye chuo cha ufundi VETA mjini hapa.

Ikaku ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya huduma za jamii katika Halmashauri hiyo alifafanua kuwa pamoja na master plan inayochorwa kwenye maeneo ambayo wananchi tayari wameshawekeza kwa namna mbalimbali,suala la kuwalipa fidia litakuwa ni gumu sana.

“Wasiwasi wangu ni kwamba master plan hii ambayo tunaichora kwenye maeneo ambayo tayari wananchi wameshawekeza kwa namna mbalimbali kuja kuwalipa fidia itakuwa ni vigumu na itatugharimu gharama kubwa sana ili kupata eneo ambalo tunalolihitaji kwenye master plan”alisisitiza diwani huyo kwa masikitiko.

Kwa mujibu wa Ikaku changamoto nyingine watakayokumbana nayo kwenye mipango hiyo ni suala la wataalamu wa mipangomiji kusimamia master plan ya Manispaa hiyo ili iweze kutekelezwa vizuri,kutokana na kile alichodai kuwa pamoja na mara kadhaa Manispaa hiyo imekuwa ikiweka master plan,lakini baadhi ya wataalamu wasiokuwa waaminifu hudiriki kubadili matumizi pasipo kufuata taratibu.

“Lakini wakati tunatenga master plan hiyo tunakuwa pamoja na wataalamu katika mikutano na katika vikao halali na vya kisheria hiyo ndiyo changamoto kubwa inayosababisha kutofautisha matumizi ambayo yalikuwa yamekusudiwa na jamii na baadaye kuonekana matumizi mengine,na hapo ndipo wananchi wanapoonyesha wasiwasi wao na serikali juu ya utekelezaji wa masterplan”alifafanua diwani huyo.

Hivyo diwani huyo alitumia fursa hiyo kuisihi serikali pamoja na watumishi waliopewa dhamana hiyo kuwa waaminifu kwa kila masterplan wanayoweka ili waweze kuitekeleza kama ilivyokusudiwa na iweze kuleta mwelekeo mzuri wa picha kama ilivyotarajiwa.

Naye diwani wa kata ya Mitunduruni,Pantaleo Matiko Sorongai pamoja na kukubaliana na mpango huo kuwa ni mzuri,lakini hata hivyo alionyesha hofu yake katika utekelezaji kwa sababu maeneo yote yaliyoainishwa katika mpango huo mengi yamepimwa na yana watu wanayoyamiliki maeneo hayo.

“Sasa unapokuwa na master plan ambayo huna sehemu ya kufanya utekelezaji inakuwa ni kiini macho…maeneo mengine wanayosema ya kuweka viwanja vya ndege,dampo kule maeneo yapo lakini katika eneo hili la Kisaki na wapi sioni kama kutakuwa na uwezekano wa kutekeleza kwa sababu maeneo hayo yote bado yatazua migogoro ya ardhi na wananchi wanaomiliki maeneo yale”alisema kwa kujiamini.

Mwezeshaji katika mkutano huo,Dk Wilfred Kazaura alifafanua kwamba idadi kubwa ya miji imekuwa na shida sana kutokana na kuendelezwa bila mipango na kwamba kwa Tanzania miji mingi sana haina master plan,na endapo utakuta mji wenye master plan itakuwa ni ya muda mrefu sana.

“Kwa ujumla wake ni kwamba miji yetu imekuwa na shida sana kwa sababu miji imeendelezwa bila mipango,kama hii bila master plan na kwa Tanzania sasa miji mingi sana haina master plan na yenye master plan zingine ni za miaka mingi iliyopita”alifafanua.

“Kama Dar-es-Salaam ina master plan ya mwaka 1979,ambayo imeshaexpire ndiyo maana mnaona stration ya mji ilivyo,kwa hiyo sasa hivi wanasema afadhali miji hii inayokuwa yote iwe na master plan na ni mkakati wa serikali kuwa miji yote ni lazima iwe na master plan ili iweze kuendelezwa sawasawa kwa utaratibu ambao umeainishwa kisheria na serikali,bila master plani mji unakuwa unajikulia wenyewe”alisisitiza mwezeshaji huyo.

0 comments:

 
Top