Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi amewanasihi Wananchi wa Jimbo hilo kuelewa kwamba jukumu na wajibu wa kulinda miradi yao ya Maendeleo waliyoianzisha wao wenyewe na ile iliyopata msukumo wa Serikali Kuu kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo limo ndani ya mikono yao.

Amesema wapo watu katika baadhi ya maeneo hapa nchini huamua kuiharibu miundombinu kwa utashi wao ambayo imeanzishwa kwa ajili ya kuwahudumia Wananchi walio wengi bila ya kufikiria usumbufu utakaowapata wana Jamii hao hapo baadaye.

Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo katika hafla fupi ya kukabidhi Mipira kumi ya kusambazia maji safi na salama pamoja na Tangi la Kuhifadhia maji kwa ajili ya Wananchi wa Kijiji cha Kilombero hapo katika Tawi la Chama cha Mapinduzi Kilombero Wilaya ya Kaskazini “B”.

Mipira pamoja na Tangi hilo vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi Milioni Tatu ni utekelezaji wa ahadi aliyowapa Wananchi wa Kilombero wakati alipokuwa akizindua Mradi wa Maji safi na salama wa Kijiji hicho katika wiki za hivi karibuni.

Balozi Seif aliwaeleza Wanachama hao wa CCM pamoja na Wananchi wa Kilombero kwamba huduma za maji safi na salama zinazoendelea kuimarishwa na Serikali Kuu kwa kushirikiana na washirika wa Maendeleo ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2010 inayokaribia kumaliza muda wake mwaka huu wa 2015.

“ Maji ni uhai na maisha ya kila siku yanayomstahikia kupata kila kiumbe wakiongozwa na Mwanaadamu na ndio maana yakatiliwa mkazo ndani ya Ilani ya CCM “. Alifafanua Balozi Seif.

Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope aliwahimiza na kuwakumbusha Wananchi hao wajitokeze kwa wingi kupiga kura wakati utakapowadia kwa kuwachagua Viongozi wote watakaosimamishwa na Chama cha Mapinduzi ambao ndio wenye uwezo kamili wa kulinda amani na utulivu wa Taifa.

Balozi Seif alitahadharisha kwamba wakati wa kuwachagua Viongozi vibaka, matapeli na wababaishaji kwa hivi sasa umepitwa na wakati kutokana na mfumo na mbadiliko ya Dunia uliopo hivi sasa.

Mapema Diwani wa Wadi ya Upenja Bibi Asha Abdulla alisema Wananchi wa Kijiji cha Kilombero wamemuhakikishia Balozi Seif kumuunga mkono kwenye harakati zake za kuendelea kuwania nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Kitope wakati utakapowadia.

Diwani Asha alisema Balozi Seif akiwa Mbunge wa Jimbo la Kitope kwa takriban miaka kumi sasa tokea mwaka 2005 amefanya mengi ya Maendeleo ndani ya uongozi wake katika kuwahudumia wananchi wa Jimbo hilo.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top