MWENYEKITI WA CCM,
MHESHIMIWA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE,

MAKAMU MWENYEKITI WA CCM ZANZIBAR,
MHESHIMIWA DKT. ALI MOHAMED SHEIN,

MAKAMU MWENYEKITI WA CCM TANZANIA BARA,
NDUGU PHILIP MANGULA,
KATIBU MKUU WA CCM,
NDUGU ABDULRAHMAN KINANA,
NAIBU KATIBU MKUU WA CCM ZANZIBAR,
NDUGU VUAI ALI VUAI,
WAJUMBE WA KAMATI KUU YA CCM,
WAGENI WAALIKWA,
MABIBI NA MABWANA.

Assalam Aleykum,
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa rehema na neema zake na kwa kutujaalia kukutana tena katika Mkutano wetu huu adhimu tukiwa wazima wa afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua nafasi hii kutoa shukrani zangu za dhati kwako Mheshimiwa Mwenyekiti wa CCM kwa kukiongoza Chama chetu kwa umakini, hekma, umahiri na weledi wa hali ya juu. Pia, nachukua fursa hii kumshukuru Makamu Mwenyeketi wa CCM Tanzania Bara na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar kwa bidii zenu, ushauri na utendaji wenu mzuri katika kukiendeleza na kukiimarisha Chama chetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nafasi ya kipekee napenda kuwashukuru Katibu Mkuu wa CCM na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, kwa juhudi zao kubwa za kukiendeleza na kukiimarisha Chama chetu, hali ambayo inazidi kuongeza imani kwa wananchi na kukijengea heshima kubwa chama chetu katika medali ya siasa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Napenda kuchukuwa fursa hii kuwashukuru Wajumbe wote wa Kamati kuu ya CCM kwa utekelezaji wa majukumu katika kukisimamia, kukilinda na kukiendeleza chama chetu kwa mafanikio makubwa katika maeneo yao ya kichama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mara nyengine tena nachukua fursa hii kukupongeza wewe Mwenyekiti ambae pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambae pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kuzisimamia Serikali zetu zote mbili katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita (2010-2015). Pia, nawashukuru Viongozi wote wa Serikali zetu za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wananchi wote wa Tanzania kwa ushiriki wao katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi
ya CCM ya Mwaka 2010 – 2015 kwa ufanisi na mafanikio makubwa.

UTANGULIZI

Mheshimiwa Mwenyekiti, Awamu ya Saba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa imetekeleza mipango mbali mbali ya maendeleo kwa kuzingatia maagizo na malengo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2010 hadi 2015. Malengo hayo yamewekwa katika Sekta ya Uchumi, Sekta za Uzalishaji Mali, Sekta za Miundombinu na Huduma za Kiuchumi, Sekta za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Sekta za Huduma za Kijamii pamoja na maeneo mengine ya kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetekeleza majukumu yake kwa
mafanikio makubwa. Mafanikio hayo ni pamoja na kuendelea kwa hali ya amani na utulivu hapa nchini; kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato ya ndani kutoka vianzio mbali mbali kufuatia juhudi zilizofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuziba mianya ya uvujaji wa mapato, kukua na kuimarika kwa utawala bora unaotilia mkazo suala la uwajibikaji ndani ya sekta ya umma na kuimarika kwa mshikamano wa wananchi.

HALI YA SIASA

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi cha mwaka 2010 hadi 2015 hali ya kisiasa Zanzibar kwa kiasi kikubwa imekuwa ya amani na tulivu, hakukuwa na matukio makubwa ya uvunjifu wa amani. Hali hii inatokana na wananchi wengi kuzidi kuelewa umuhimu wa kudumisha amani na utulivu pamoja na kushirikiana na Serikali kwa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla. 

Matukio muhimu ya kisiasa yalijitokeza katika kipindi hiki ni kufanyika chaguzi ndogo mbili kwa nafasi za Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na chaguzi tatu za Udiwani ambazo kwa nafasi zote hizo CCM ilishinda. Pia, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeendesha chaguzi ndogo yanafasi ya Ubunge katika Jimbo la Cham bani. Vile vile, katika kipindi hicho, nchi yetu iliadhimisha sherehe za kutimiza miaka 50 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar sherehe ambazo zilifana sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ingawaje hali ya amani na utulivu iliendelea kutawala nchini katika kipindi chote cha taarifa hii hata hivyo kulijitokeza baadhi ya matukio yaliyoashiria uvunjifu wa amani.

Matukio hayo ni pamoja na kuuawa kwa askari wa Jeshi la Polisi na
kiongozi mmoja wa kidini, kumwagiwa tindikali kwa viongozi wa dini na Serikali, na wageni wakitalii. Pia, kulitokea mripuko uliosadikiwa kuwa ni bomu na kusababisha kifo cha mtu mmoja na kujeruhi watu wengine katika eneo la Darajani. Aidha, vilijitokeza vikundi vilivyoandaa mihadhara waliyodai kuwa ya kidini na kufanya maandamano bila ya kupata kibali na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali za Serikali, mali za wananchi pamoja na nyumba za ibada. 

 Vile vile Maskani kadhaa na matawi ya CCM yalichomwa moto. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wenye hekima na busara wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Ali Mohamed Shein ilifanikiwa kudhibiti vurugu hizo kwa kuwakamata waliohusika na kuwafikisha katika vyombo vya kisheria

HALI YA KIUCHUMI

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita
(2010-2015) uchumi wa Zanzibar umeendelea kuonyesha mwenendo mzuri ambapo ukuaji wa Pato la Taifa umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka kutoka asilimia 6.4 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 7.4 mwaka 2015.

Aidha, mapato ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yameonyesha
kuongezeka kutoka TZS Bilioni 181 kwa mwaka 2010/11 hadi kufikia TZS Bilioni 330 mwaka 2014/2015 sawa na ongezeko la asilimia 82. Ongezeko hilo limetokana na kuimarika kwa Sekta ya Kilimo, Misitu na Uvuvi, Sekta Ndogo ya Uzalishaji Viwanda, Sekta ya Huduma inayojumuisha Sekta Ndogo ya Hoteli na Mikahawa, na kuongezeka kwa idadi ya watalii wanaoingia nchini. Ongezeko hilo limechangiwa kwa kiasi kutokana na juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kuziba mianya inayosababisha uvujaji wa mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya mfumko wa bei kwa upande wa Zanzibar imeshuka kutoka asilimia 6.1 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 5.6 mwaka 2014, hali hii imetokana na juhudi za Serikali katika kudhibiti mfumko huo wa bei ikiwemo kutoa ruzuku za pembejeo kwa wakulima ambako kulipelekea kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya chakula. Aidha, Serikali imetoa misamaha ya kodi kwa bidhaa muhimu za chakula kama vile sukari, unga na mchele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeanza kutekeleza ahadi ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010-2015 ya kuendeleza Maeneo Huru ya Kiuchumi ya Fumba. Katika utekelezaji wa ahadi hii, Serikali imechukuwa hatua mbali mbali ikiwa ni pamoja na kutayarisha Mpango Mkuu wa Matumizi ya Ardhi Fumba, upimaji na utayarishaji wa mchoro wa ramani ya eneo hilo. Jumla ya hekta 3,000 zimepimwa na kugaiwa kwa matumizi tofauti ambapo hekta 743 zimetengwa kwa ajili ya uwekezaji wa shughuli za kibiashara, hekta 1,310 kwa ajili ya vijiji vya asili na makaazi na hekta 946 kwa ajili ya eneo la akiba. 

Serikali imefanikiwa kukamilisha ujenzi wa njia kuu ndani ya eneo la uwekezaji Fumba yenye urefu wa kilomita 10 kwa kiwango cha lami. Aidha, Serikali imekamilisha mazungumzo na Mwekezaji wa Kampuni Mama ya Bakhressa Group juu ya kushirikiana katika uwekezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Mji wa Kisasa wa Fumba (Fumba Bay Satillite City). Kwa sasa kiwanda kikubwa cha usarifu maziwa cha Azam Dairy Milk na Zanzibar Fiber Glass tayari vimeanzishwa na vinaendelea na kazi na miradi mingine ya huduma na nyumba za makaazi imo katika hatua za awali.

Kutekelezwa kwa miradi ya aina hii katika eneo hilo la Fumba kunatarajiwa kuzalisha ajira zaidi kwa wananchi pamoja na kukuza Pato la Taifa.

SEKTA ZA UZALISHAJI MALI

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekta za Uzalishaji Mali zinajumuisha kilimo, ufugaji, uvuvi, maliasili, utalii, viwanda na biashara na Vyama Vya Ushirika.

KILIMO

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekta ya Kilimo ni mojawapo ya sekta muhimu sana kwa uchumi wa Zanzibar ambapo inatoa mchango wa moja kwa moja katika kujikimu kimaisha. Pia, sekta hii ni muhimu kwa upatikanaji wa uhakika wa chakula katika ngazi ya familia na Taifa na inasaidia kuimarisha lishe na afya za wananchi walio wengi mijini na vijijini.

Aidha, inakadiriwa kuwa zaidi ya asilimia 70 ya wananchi wa Zanzibar wanategemea Sekta ya Kilimo kwa kuwapatia ajira na kipato. Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la karafuu ndilo linalochangia kwa kiasi kikubwa katika mchango wa sekta ya kilimo katika pato la Taifa. Zao hilo pia ndilo linaloingizia nchi yetu kiasi kikubwa cha fedha za kigeni. Katika jitihada za kuliendeleza zao la karafuu, Serikali imeendelea kuongeza uzalishaji wa miche ya mikarafuu kutoka mwaka hadi mwaka. Kutokana na juhudi mbali mbali za Serikali na wakulima, uzalishaji wa karafuu umeongezeka kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na mabadiliko ya tabia nchi kunakosababisha kutokuwa na uhakika wa upatikanaji wa mvua, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa Maendeleo imeendelea kuchukua jitihada za kuimarisha kilimo cha umwagiliaji maji kinachoongeza tija na uzalishaji na kuwaongezea kipato wakulima wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuongeza kasi ya maendeleo ya kilimo, Serikali kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Kizimbani imeendelea kufanya tafiti mbali mbali za kilimo pamoja na kusambaza matokeo ya tafiti hizo kwa wakulima na wadau wengine wa kilimo. Miongoni mwa tafiti zilizofanywa ni pamoja na tafiti ya zao la mpunga, mazao ya mizizi na matunda na utafiti wa matumizi ya mbolea mpya. 

 Aidha, Serikali imenunua vifaa mbali mbali vya kilimo ikiwemo matrekta na mashine za kuvunia mpunga pamoja na kuyafanyia matengenezo matrekta ya zamani. Serikali pia imezidi kukiimarisha Chuo cha Kilimo Kizimbani ili kiweze kutoa mafunzo ya kilimo na mifugo kwa wanafunzi, wakulima pamoja na wadau wengine wa kilimo.

UFUGAJI

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetekeleza mpango wake wa kuendeleza ubora wa mifugo kwa kupata mbegu bora za mifugo zenye manufaa zaidi kwa wafugaji, kutoa elimu kwa watoa huduma za msingi, madaktari wasaidizi na wafugaji juu ya namna ya kuendeleza ufugaji bora, kukuza fursa za masoko na kuimarisha huduma za kinga na tiba kwa mifugo. Matokeo ya jitihada hizo yemepelekea kuongezeka uzalishaji wa mazao ya mifugo.

UVUVI NA MAZAO YA BAHARINI

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuendeleza Sekta ya Uvuvi, Serikali imeendelea na jitihada zake za kuwasaidia na kuwaendeleza wavuvi wadogo wadogo kwa kuwapatia zana bora na za kisasa, kuwapatia taaluma bora ya uvuvi unaozingatia uhifadhi wa mazingira ya bahari, kuwajengea miundombinu ya masoko na uhifadhi wa samaki, kuwapatia taaluma ya ufugaji wa samaki na kuwaongezea uwezo juu ya uzalishaji bora wa zao la mwani.

 Kutokana na juhudi hizi uzalishaji wa samaki umeongezeka kwa kiasi kikubwa kwa Unguja na Pemba. Aidha, katika kupambana na
uvuvi haramu na uharibifu wa mazao ya baharini, Serikali imeendelea kufanya doria na kutoa mafunzo kwa vikundi vya uvuvi, wananchi na Kamati za Uvuvi pamoja na kutoa leseni za uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uzalishaji wa zao la mwani umekuwa ukiwasaidia wananchi hasa kinamama katika kuwaongezea kipato chao. Katika kulifahamu hilo, Serikali imeendeleza tafiti juu ya zao la mwani, imetoa vifaa pamoja na kuwapatia soko la uhakika wakulima wa zao hilo.

MALIASILI

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kufahamu umuhimu wa misitu na maliasili zisizorejesheka, Serikali imeendelea na udhibiti na uhifadhi wa maliasili zikiwemo rasilimali za misitu pamoja na maliasili zisizorejesheka kwa kutoa elimu na kushajiisha jamii juu ya uhifadhi wa rasilimali hizo. Aidha, Serikali imekuwa ikichukua jitihada kubwa juu ya suala zima la ushajiishaji jamii katika muendelezo wa kupanda na kuitunza miti.

UTALII

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea na juhudi mbali mbali za kuimarisha Sekta ya Utalii kwa kuifanyia mapitio makubwa Sheria ya Utalii kwa lengo la kuzidisha kasi ya usimamiaji wa masuala ya utalii, kuanzisha Maabara ya Utalii yenye lengo la kuibua mikakati imara ya kupanua wigo katika sekta hii muhimu pamoja na kuitangaza Zanzibar kiutalii katika nchi mbali mbali. Aidha, Serikali imeendelea na mikakati yake ya kuimarisha sekta hii. Miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na uimarishaji wa miundombinu ya utalii, kuimarisha vivutio vya utalii na kukiboresha Chuo cha Maendeleo ya Utalii.

VIWANDA NA BIASHARA

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kusimamia utekelezaji wa Sera ya
Uendelezaji wa viwanda vidogo vidogo na vya kati, Serikali imefanya ukarabati mkubwa wa Kiwanda cha Sukari kilichopo Mahonda. Vile vile Serikali imeshajihisha sekta binafsi kuwekeza katika viwanda ambapo kiwanda kikubwa cha maziwa (Azam Diary Factory) kimefunguliwa rasmi na kimeanza kazi za uzalishaji na usambazaji wa maziwa ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuliendeleza zao la karafuu, Serikali imechukua hatua za kuilinda na kuipa hadhi zaidi karafuu yetu pamoja na kuitangaza Zanzibar ulimwenguni kupitia bidhaa nyengine za viungo zikiwemo mdalasini, pilipili hoho, na pilipili manga ambapo kazi hii inatekelezwa kupitia mradi wa Tasnia Malibunifu (Branding). Pia, Serikali imeunda Taasisi ya Viwango ya Zanzibar (ZBS) katika kusimamia ubora wa bidhaa zinazozalishwa na kuingizwa nchini.

VYAMA VYA USHIRIKA

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha miaka mitano Serikali
imeendelea na juhudi zake za kuimarisha na kuendeleza vyama vya
ushirika kwa kutoa mafunzo juu ya ushindani, ubunifu na ujasiriamali kwa walengwa. Aidha, Serikali katika hatua za utunzaji wa rasilimali na hesabu za ushirika imefanya ukaguzi wa hesabu za vyama vya ushirika mbalimbali kwa Unguja na Pemba.

MIUNDOMBINU YA KIUCHUMI

Mheshimiwa Mwenyekiti, miundombinu ya kiuchumi inajumuisha barabara, viwanja vya ndege, usafiri wa baharini, umeme na bandari. Kutokana na umuhimu huo Serikali imetekeleza yafuatayo kisekta.

BARABARA

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na ujenzi wa barabara za Unguja na Pemba ili ziendelee kupitika kwa wakati wote na kuwarahisishia wananchi usafiri. Jumla ya kilomita 181.7 za barabara kwa Unguja na Pemba zimekamilika. Vilevile, barabara zenye urefu wa kilomita 36.5 zilizojengwa kwa kiwango cha kifusi kwa Unguja na Pemba zimekamilika. Pia, barabara zenye urefu wa kilomita 80.5 zinaendelea kujengwa kwa kiwango cha lami zinaendelea kujengwa kwa Unguja na Pemba.

Usafiri wa Baharini

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuimarisha miundombinu ya Usafiri wa Baharini, Serikali kwa kushirikiana na Kampuni ya AZAM MARINE imejenga majengo ya kuhudumia abiria katika Bandari ya Malindi. Aidha, Serikali imekamilisha matengenezo makubwa ya gati ya Mkoani Pemba na kuondoa tatizo la kutuama kwa maji juu ya gati hiyo.

Mheshimwa Mwenyekiti, katika kuwaondolea usumbufu wa usafiri wananchi wetu na watumiaji wengine baina ya visiwa vyetu na maeneo mengine ya mwambao wa Afrika Mashariki, Serikali kupitia Shirika la meli inaendelea na ujenzi wa meli mpya yenye uwezo wa kuchukua abiria 1200 na mizigo tani 200. Meli hiyo inatengenezwa nchini Korea ya Kusini na inatarajiwa kuingia nchini mwishoni wa mwezi Julai, 2015.

Usafiri wa Anga

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuimarisha huduma za Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume, Serikali imeendelea na kazi ya kujenga uzio wenye urefu wa kilomita 11.9. Aidha, Serikali inaendelea na ujenzi wa jengo jipya la abiria lenye ukubwa wa mita za mraba 25,000. Jengo hilo litakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria 1,600,000 kwa mwaka. 

 Serikali inaendelea kufanya marekebisho na kuongeza eneo la kuegeshea ndege lenye ukubwa wa mita za mraba 37,000. Marekebisho hayo yatabadilisha mfumo wa uegeshaji wa ndege kubwa kutoka mbele ya jengo (airside) na badala yake kuegesha upande wa kusini ya jengo.

UMEME

Mheshimiwa Mwenyekiti, Nishati ya Umeme ni muhimu katika kujenga msingi wa uchumi wa kisasa wa Taifa linalojitegemea. Katika kutekeleza azma hiyo Serikali imejenga njia ya umeme inayopita chini ya bahari kutoka Ras Kiromoni Tanzania Bara hadi Fumba Unguja na inayotoka Tanga hadi Pemba. Mpango huu umetuwezesha kupata kiwango cha umeme kutoka “Megawatt” 45 na kufikia 145 kwa Unguja na kwa upande wa Pemba “Megawati” 20 zimeongozeka. Pia Serikali imeendelea na uimarishaji wa vituo vya usambaziji umeme katika maeneo mbali mbali na kutilia mkazo
usambazaji wa umeme mijini na vijijini. 

Katika kuendeleza juhudi za utafiti wa vyanzo vya nishati mbadala ya umeme ukiwemo umeme wa jua, mawimbi ya bahari, upepo na gesi asilia, Serikali imeyakagua upya na kuyafanyia uhakiki maeneo yote ambayo yalifanyiwa utafiti wa awali na kupendekezwa na wataalamu kutoka EU ili kutumika kwa ajili ya nishati mbadala kabla ya kuanza hatua ya utekelezaji. Pia, Serikali imeendelea kuliimarisha Shirika la Umeme (ZECO) ili lizidi kujiendesha kibiashara na kutoa huduma bora wananchi.

ARDHI

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeandaa Sera ya Ardhi ambayo
itasimamia matumizi bora ya ardhi kwa matumizi ya sasa na vizazi
vijavyo. Aidha, Serikali imefanya upitiaji na utayarishaji wa Mpango Mkuu wa Kitaifa wa Matumizi Bora ya Ardhi wa Zanzibar (National Land Use Plan). Vile vile, Serikali inaendelea na kazi ya usajili wa ardhi, kuwaelimisha wananchi juu matumizi bora ya ardhi pamoja na kuziimarisha na kuanzisha Mahakama za Ardhi katika kila Mkoa na kuongeza idadi ya Mahakimu kwa lengo la kupunguza migogoro ya ardhi katika maeneo yao.

MAZINGIRA

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali bado inaendelea na mikakati ya
uthibiti na uhifadhi wa mazingira kwa kuandaa, kutekeleza na kusimamia mipango mbali mbali ya uhifadhi wa mazingira katika maeneo ya ardhi, bahari na ukanda wa pwani. Aidha, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali imefanya mapitio na ukaguzi wa miradi inayohusiana na mazingira ili kupata tathmini ya athari za kimazingira. 

Vile vile Serikali imezindua kikosi kazi cha udhibiti wa uharibifu wa mazingira katika visiwa vya Zanzibar. Pia, Serikali imefanya mapitio ya Sera ya Mazingira ya mwaka 1992 na kuzindua Sera ya Mpya ya Mazingira ya mwaka 2013 ambayo inatoa miongozo kwa shughuli za uhifadhi wa mazingira.

HUDUMA ZA JAMII

ELIMU

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetoa kipaumbele kwa Sekta ya Elimu kwa sababu ndio msingi wa maendeleo ya jamii na Taifa kwa jumla. Katika kulitilia mkazo suala hilo, Serikali imechukua hatua mbali mbali katika kuboresha elimu kama ifuatavyo:-

Elimu ya Maandalizi

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuendeleza juhudi za kuongeza ushiriki wa wanafunzi katika ngazi ya maandalizi, idadi ya Skuli za Maandalizi imeongezeka hadi kufikia 270 mwaka 2015 kutoka 238 mwaka 2010 hali ambayo ongezeko la wanafunzi 29,732 mwaka 2010 na kufikia wanafunzi 38,808 mwaka 2015. Kwa upande wa Elimu ya Msingi, Serikali kwa kushirikiana na wananchi imeendelea kujenga skuli za msingi kwa sasa jumla ya skuli 370 mwaka 2015 kutoka 299 mwaka 2010. 

Aidha, Serikali imekamilisha ujenzi wa skuli 19 za sekondari Unguja na Pemba kwa asilimia 100 na tayari skuli hizo zinatumika. Pia Serikali imeongeza juhudi za kuzipatia vifaa vya kufundishia na kujifunzia skuli zote za Maandalizi, Msingi na Sekondari. Pia, Serikali inaendelea na juhudi za kuimarisha masomo ya Sayansi na Hisabati kwa kuwapatia mafunzo kazini Walimu wa masomo hayo, Walimu Wakuu, Maafisa wa Elimu wa Wilaya na Mikoa. 

Vile vile, Serikali inaendelea na jitihada katika kutoa elimu ya watu wazima, hali ambayo imepelekea kupungua kwa idadi ya wanakisomo kwa kiasi kikubwa.

Huduma za maktaba

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuimarisha huduma za maktaba, Serikali imekamilisha ujenzi wa Maktaba Kuu ya Zanzibar na kujenga Maktaba mpya kwa upande wa Pemba. Aidha, Serikali imeendelea kuzipatia vitabu na huduma nyengine za kimaktaba ili kuziwezesha kutoa huduma kwa ufanisi.

Pia Serikali kupitia Shirika la Huduma la Maktaba limeendesha mafunzo ya ukutubi kwa walimu wa skuli 44 za Unguja na 40 za Pemba ili wapate taaluma sahihi juu ya namna bora ya kutoa huduma za maktaba na kukuza maendeleo ya elimu. Aidha, Serikali imeanzisha utaratibu wa kuwa na maktaba za jamii ili ziweze kutoa huduma kwa jamii kwa ukaribu zaidi.

Elimu ya Juu

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutilia mkazo suala la elimu ya juu
nchini, Serikali imekamilisha ujenzi wa Chuo Kikuu Cha Taifa SUZA, Tunguu. Ujenzi huo umekamilika kwa majengo manne (4) na kuweka vifaa kwa ajili ya chuo hicho. Aidha, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita (2010 – 2015), Serikali imezidi kuongeza fursa za elimu ya juu kwa kutoa mikopo kwa wanafunzi wanaosoma ndani na nje ya nchi.

Vile vile, Serikali imeboresha mazingira ya wawekezaji wa Sekta Binafsi kuendelea kuekeza katika elimu ya juu. Chuo kikuu cha Zanzibar kinaendelea kutoa mafunzo mbali mbali katika Shahada ya Kwanza na Shahada ya Pili. Chuo cha Elimu Chukwani kimepandishwa hadhi na kuwa Chuo Kikuu kamili (Al-Ssumait University) na hivyo kukiwezesha kutoa shahada za juu.

Mafunzo ya Ualimu

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuimarisha mafunzo ya ualimu, Serikali imeandaa Rasimu ya Sera ya Mafunzo ya Ualimu Kazini na imefanya mapitio ya Mtaala wa Diploma ya Msingi. Mtaala huo umeingiza masomo mapya yakiwemo ya habari na mawasiliano, mafunzo ya amali, uongozi na michezo. Aidha, Serikali imeendesha mafunzo kazini kwa walimu wa Skuli za Msingi na Sekondari kwa masomo ya Sayansi na Hesabati, kompyuta na somo la Kiingereza pamoja na mbinu bora za kufundishia kwa njia ya mtandao.

Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Amali

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kutoa elimu ya amali
kupitia Vituo vya Mafunzo ya Amali vya Mkokotoni, Mwanakwerekwe na Vitongoji. Vituo hivyo vinatoa mafunzo ya fani mbali mbali za ufundi zikiwemo useremala, ushoni, uhunzi, upishi, uchoraji na uandishi wa alama, uashi, ufundi bomba, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, huduma za chakula na vinywaji, ufundi magari, umeme na ufundi wa mafriji na viyoyozi. Aidha, Serikali imeendelea kukiimarisha Chuo cha Ufundi Karume kwa ujenzi wa Madarassa na Mabweni ya wanafunzi, ukarabati wa mfumo wa maji na umeme kwa majengo yote ya chuo pamoja na
kukipatia vifaa vya mawasiliano ili kukiwezesha kwenda sambamba na ulimwengu wa sayansi na teknolojia. Vile vile, Serikali imeiendeleza na kuimarisha Skuli ya Ufundi Kengeja huko Pemba.

SEKTA YA AFYA

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita,
Serikali imejikita katika kusimamia utekelezaji wa sera na programu
mbali mbali zinazohusiana na sekta ya afya. Huduma za Kinga na Tiba: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuendeleza huduma ya kinga na tiba, Serikali imefanya utafiti juu ya kuangalia kiwango cha sababu hatarishi zinazopelekea kupata maradhi yasiyo ya kuambukiza. Matokea ya utafiti huo yameonesha idadi kubwa ya jamii inasumbuliwa na tatizo la uzito mkubwa (Obesity). 

 Serikali kwa kushirikiana na Jumuiya ya Watu wanaoishi na Kisukari, imeshajiisha jamii kuanzisha vikundi vya mazoezi katika Wilaya zote za Unguja na Pemba. Aidha, Serikali inaendelea kuchukua juhudi mbali mbali za kukuza uelewa kwa jamii juu ya kujikinga na maradhi ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza.

Vilevile, Serikali inaendelea kutoa huduma za tiba kwa magonjwa mbali mbali yakiwemo maradhi ya moyo, kisukari na mengineyo kwa wananchi wake kupitia hospitali na vituo vya afya kwa kipindi chote cha miaka mitano iliyopita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na kampeni za kupunguza na kudhibiti malaria Zanzibar. Katika Mpango huo ujulikanao kama “Maliza Malaria Zanzibar”, Serikali imefanikiwa kupunguza ugonjwa wa Malaria katika jamii kutoka asilimia 0.06 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 0.03 mwaka 2013. Katika kupambana na ugonjwa wa UKIMWI, Serikali imeimarisha huduma za tiba na huduma za kuzuia maambukizi ya mama kwenda kwa mtoto. 

Aidha, Serikali imeimarisha vituo vya ushauri nasaha na upimaji wa VVU kwa kuvipatia nyenzo za kufanyia uchunguzi. Vile vile, Serikali imeendelea kutoa elimu na tiba kwa maradhi nyemelezi kama vile kifua kikuu na ukoma ili kupunguza maambukizi zaidi.

Huduma bora za Afya kwa wananchi wote

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha kuwa hospitali zetu zote zinatoa huduma bora za afya kwa wananchi wetu, Serikali inaendelea na mipango yake ya kuzipandisha daraja hospitali zake za Unguja na Pemba.

Katika kutekeleza mkakati huu, Serikali imeziongezea majengo pamoja na kuzipatia vifaa vya kisasa Hospitali ya Mnazimmoja ili ifikie hadhi ya Hospitali ya Rufaa, hospitali ya Abdallah Mzee Mkoani ili ifikie hadhi ya hospitali ya Mkoa na Hospitali za Wete, Kivunge na Makunduchi ili zifikie hadhi ya Hospitali za Wilaya. Aidha, Serikali imeendelea kuviendeleza vituo vya afya vikiwemo vya daraja la kwanza na daraja la pili ambavyo vinatoa huduma za ziada kama vile huduma za kuzalisha, maabara na huduma za meno. Vile vile, Serikali imeifanyia mapitio Sera ya Afya ya mwaka 1999 na kuwa na Sera mpya ya mwaka 2011 pamoja na Sheria ya Afya ya Jamii ambazo zinakwenda sambamba na mahitaji pamoja na mikataba ya kitaifa, kikanda na kimataifa katika utoaji wa huduma za afya nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha upatikanaji wa dawa muhimu katika vituo vya afya unakuwa wa kuridhisha kwa wananchi, Serikali inaendelea kutoa huduma za dawa bila ya malipo katika hospitali zote na vituo vya afya. Vituo vyote hivi vinafaidika na upatikanaji wa dawa chini ya mpango maalum ujulikanao kama “Zanzibar Integrated Logistic System”. Aidha, Serikali imejenga Bohari Kuu ya Madawa iliyopo Maruhubi ambayo itarahisisha kupata na kutoa taarifa za hali ya upatikanaji wa dawa kutoka hospitali na vituo vya afya mbali mbali nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja wapo katika jambo muhimu la upatikanaji wa huduma ya afya kwa wananchi ni kuwa na madaktari na watoa huduma wenye uwezo mzuri wa kazi hiyo. Katika kuhakikisha kuwa azma hii inafikiwa, Serikali inaendelea kuwajengea uwezo madaktari na watoa huduma wa hospitali na vituo vya afya kwa kuwapeleka masomoni katika vyuo mbali mbali vya ndani na nje ya nchi. Hatua hii imeweza kutupatia madaktari na watoa huduma wenye ufanisi zaidi kwa wananchi wetu. 

Aidha, Chuo cha Taaluma cha Sayansi za Afya kinaendelea kutoa taaluma za afya kwa kiwango cha Stashahada katika fani mbali mbali. Vile vile, Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Cuba imewasomesha wanafunzi 38 wa kada ya Udaktari, ambao tayari wamemaliza masomo yao, hivyo kupata madaktari wengine wazalendo 38 idadi hiyo imewezesha madaktari wote wanaotoa huduma Zanzibar kufikia 142, kati ya hawa madaktari 40 ni madaktari wa kigeni kutoka Cuba na China hali ambayo imepelekea kwa sasa kuwa na uwiyano wa daktari mmoja kuhudumia wastani wa wagonjwa 9,708.

Huduma Za Tiba Asili

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kusimamia matumizi sahihi ya Tiba Asili, Serikali kwa kushirikiana na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala imeelimisha jamii kupitia vyombo mbali mbali vya habari, kutumia vipeperushi pamoja na kufanya mikutano. Pia, Baraza limefanikiwa kutengeneza Kanuni (regulations) za Tiba Asili na kutoa elimu kwa waganga. 

Sambamba na hayo, Baraza limeweza kusajili waganga, waganga wasaidizi, kliniki za tiba asili na tiba mbadala, viringe au sehemu wanazofanyia na maduka ya dawa za asili baada ya kutimiza masharti ya sheria za Baraza. Aidha, Serikali imefanya uchunguzi wa sampuli za dawa asilia chini ya usimamizi wa Maabara ya Bodi ya Chakula na Madawa. 

Vile vile, katika kuhakikisha Baraza la Tiba Asili linafanya kazi zake vizuri na ipasavyo limejenga uhusiano mzuri kati ya madaktari wa kisasa (Biomedical Practitioners) na waganga wa asili (Traditional Healers).

MAJI

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hatua za kuendeleza upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi, Serikali imeendelea na uchimbaji wa visima na ulazaji wa mabomba makubwa katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba ambapo utekelezaji wa hatua hii umefikia asilimia 96.15 kwa Unguja na asilimia 96.26 kwa Pemba. 

 Pia Serikali imesambaza pampu mpya katika maeneo mbali mbali ya mijini na vijini ambapo kwa sasa mradi huu umefikia asilimia 94 ya utekelezaji. Aidha, mradi wa usambazaji maji safi na salama katika Mkoa wa Mjini Magharibi uliojumuisha ujenzi wa matangi mawili umekamilika.

MAKAAZI

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kuzingatia agizo la Ilani ya
Uchaguzi ya CCM (2010-2015) imeendelea kusimamia utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Nyumba na Sheria ya Shirika la Nyumba la Zanzibar ya mwaka 2014 imeshapitishwa na Baraza la Wawakilishi. Aidha, Serikali imekamilisha ujenzi wa Nyumba ya Maendeleo Bambi (Mpapa) ambapo fleti 24 zimekabidhiwa kwa wananchi wakati wa Sherehe za Maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar. 

 Vile vile Serikali inaendeleza Mji Mkongwe wa Zanzibar ambao ni hazina kubwa na kivutio cha historia ya Zanzibar. Hivyo basi, Serikali kwa kushirikiana na watu binafsi inaendelea kuulinda, kuuhifadhi na kutumika kama kivutio cha utalii na kubakisha dhana ya urithi wa Dunia.

MAENEO MENGINE YA KIPAUMBELE

Utamaduni na Michezo

Mheshimiwa Mwenyekiti, utamaduni ni moja kati ya mambo muhimu katika Taifa lolote duniani, kwa kuzingatia hilo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeifanyia mapitio Sera ya Utamaduni ili iendane na wakati kwa kuihusisha Sekta ya Utalii na Utamaduni. Aidha, katika kuufanya utamaduni uwe na tija zaidi, Serikali imekamilisha mchoro wa ramani ya utamaduni katika Shehia za Unguja na Pemba. Pia, Serikali imekamilisha utafiti wa Urithi wa Utamaduni Usioshikika katika mikoa yote ya Unguja na Pemba na hatimaye kuhifadhiwa na kutangazwa kimataifa kwa kuingizwa katika orodha ya “UNESCO” ya Utamaduni uliohifadhiwa. 

 Vile vile, Serikali imechukua hatua za kuzikagua kazi za sanaa kwa lengo la kulinda na kuhifadhi mila na silka za Wazanzibari. Pia, imeandaa makamusi ya lahaja ya Kipemba, Kimakunduchi na Kitumbatu kwa lengo la kuendeleza lahaja hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuendeleza michezo kwa faida ya vijana wetu na Taifa kwa ujumla, Serikali imeifanyia mapitio Sera ya Michezo ili iwe muongozo kwa shughuli zote za michezo nchini. 

Aidha, Serikali imeufanyia matengenezo na marekebisho makubwa uwanja wa Gomabani Pemba ili kuuwezesha uwanja huo kukidhi haja ya mashindano ya kimataifa ya mpira wa miguu. Vile vile, Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Japan imejenga ukumbi wa Zanzibar Budocan ndani ya Uwanja wa Amaan na uwanja huo tayari umeanza kutumika kwa michezo ya judo, karati na michezo mingine ya ndani inayolingana na hiyo. 

Sambamba na hayo Serikali ya imekamilisha mradi wa ujenzi wa studio ya kisasa ya kurikodia nyimbo na michezo ya kuigiza kwenye jengo la zamani la Utangazaji la Sauti ya Tanzania Zanzibar baada ya jengo hilo kufanyiwa matengezo makubwa. Tayari Serikali imenunua na kufunga vifaa vipya kwa ajili ya studio hiyo ambavyo vimegharimu jumla ya shilingi 291,534,000.

Vyombo vya habari:

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha wananchi wetu wanapata habari kwa wakati na zenye uhakika, Serikali imetunga Sheria Namba 4 ya mwaka 2013 ya kuunda Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC), Sheria hiyo tayari imepitishwa na Baraza la Wawakilishi na imeanza kufanya kazi. 

 Sambamba na hilo Serikali imeandaa na kusimamia utekelezaji wa Sheria ya vyombo vya habari, kanuni na miongozo kwa lengo la kuleta ufanisi katika mageuzi ya mfumo wa utangazaji kutoka Analogi kwenda Digitali. Aidha, Serikali imeweza kufanya mageuzi makubwa katika vyombo vya habari kwa kuvipa uhuru na haki ya kuhoji, kutafuta, kupokea na kuchapisha habari na maoni bila ya woga. 

Vile vile kwa lengo la kupanua misingi ya demokrasia ya habari, Serikali imeshajiisha wawekezaji kuwekeza katika Sekta ya habari na tayari vituo vya Redio vinne (4) na Televisheni vitano (5) vimeazishwa katika kipindi cha 2010-2015.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia mafanikio makubwa ya vyombo vya habari vya Serikali, Shirika la Magazeti la Zanzibar limeweza kuongeza maeneo ya usambazaji kwa Zanzibar na Tanzania Bara mjini na vijijini. Pia Serikali imekuwa ikitoa miongozo mbali mbali kwa vyombo vya habari kuzingatia maadili ya uandishi wa habari na pia kuheshimu na kulinda maslahi na uhuru wa raia wa kuishi pamoja na haki za faragha. 

Vile vile, Tume ya Utangazaji imeanzisha mfumo wa ufuatiliaji vipindi (Monitoring System) ambapo hivi sasa vipindi vyote vinarikodiwa, kuhifadhiwa na kufuatiliwa. Aidha, katika kipindi cha 2010 hadi 2014, waandishi 42 wameweza kupatiwa mafunzo katika ngazi tofauti zikiwezo Stashahada, Shahada ya Kwanza na Shahada ya Uzamili. Vile vile, taaluma mpya ya teknolojia ya digitali imetolewa kwa mafundi, watayarishaji vipindi na viongozi wa vituo vya utangazaji vya Serikali na Binafsi vilivyopo Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeviimarisha Vyombo vya Habari vya Zanzibar kwa kuvinunulia vifaa mbali mbali vya kisasa vinavyotumia teknolojia ya digitali. Aidha, Serikali imeweza kuimarisha kazi za utangazaji kwa kuhamisha mnara wa masafa ya kati (medium waves) kutoka Chumbuni kwenda Bungi. Pia, Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China imefanya ukarabati wa mnara wa mawimbi mafupi (short wave).

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza agizo la Ilani ya Uchaguzi ya CCM (2010-2015) ya uendelezaji wa taaluma ya habari, Serikali imekiimarisha Chuo cha Uandishi wa Habari kwa kuweka vifaa pamoja na kuajiri walimu wenye ujuzi ili kuweza kutoa wahitimu wenye uwezo mzuri wa tasnia ya habari. Vile vile, Chuo kimeweza kutengeneza nyaraka mbali mbali za kitaalamu ikiwemo Kitabu cha Miongozo wa Shughuli za Chuo (Prospectus), Mpango Mkakati (Strategic Plan) na Vipeperushi.

Pia, Chuo kimeweza kuanzisha mafunzo ya lugha ya Kichina kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China. Sambamba na hayo, Chuo kimekuwa na ushirikiano wa karibu na Redio ya Kimataifa ya Deutsche Welle (DW) ya Ujerumani ambayo imekuwa ikisaidia kuwajengea uwezo walimu na wanafunzi kwa kuwapatia mafunzo mbali mbali.

Majanga na huduma za uokozi

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kushughulikia masuala ya majanga na maafa, Serikali imeandaa Sera ya kukabiliana na maafa, na Mpango wa Dharura wa Kujiandaa na Kukabilana na Maafa. Vile vile, Serikali imeandaa Muongozo wa Ufuatiliaji na Tathimini pamoja na Mkakati wa Mawasiliano wakati wa Maafa. Aidha, elimu ya kukabiliana na maafa kwa ajili ya kujenga uelewa kwa jamii juu ya majanga na maafa imetolewa katika ngazi ya Shehia, Wilaya na Taifa. Kutokana na elimu hii Kamati za maafa za Shehia zimeundwa katika Shehia za Unguja na Pemba. 

Aidha, Serikali imeweza kukiimarisha Kikosi Maalum cha Uokozi na Uzamiaji cha (ZARDEC) kwa kuwashirikisha katika shughuli mbali mbali za kukabiliana na maafa pamoja na kuhamasisha vikosi vyengine vidogo vidogo kuanzisha Jumuiya za pamoja ili kurahisisha shughuli za uokozi pindi maafa yanapotokea.

Madawa ya kulevya

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na changamoto za Madawa ya kulevya hapa Zanzibar, Serikali kupitia Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya imeweza kuandaa mpango maalum (Road Map) wa utekelezaji wa Sheria ya Dawa za Kulevya. 

Serikali imeanzisha vikao vya Kamati ya Kitaaluma ya Kupambana na Dawa za Kulevya na kuandaa Sera ya Dawa za Kulevya na kufanya mikutano na vyombo vya kusimamia sheria (Law Enforcement Agency- LEA) ili kukuza mashirikiano na vyombo hivyo kwa kudhibiti mapambano ya Dawa za Kulevya. Aidha, Serikali imetoa taaluma juu ya madawa ya kulevya katika maeneo ya kazi, maskulini, Shehia na makundi mbali mbali Unguja na Pemba. 

Pia Serikali imetayarisha muongozo wa nyumba za makaazi ya vijana walioacha matumizi ya Dawa za Kulevya (Sober House).

Demokrasia na Utawala Bora

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kusimamia demokrasia na utawala bora nchini, Serikali imeandaa Sera ya Utawala Bora pamoja na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa lengo la kutoa miongozo ya utekelezaji wa demokrasia na utawala bora nchini. Aidha, Serikali imetoa elimu ya uraia kwa wananchi juu ya Sera ya Utawala Bora, Rushwa na Haki za Binaadamu kupitia vyombo vya habari, ziara za vijijini pamoja na kutumia vikundi vya sanaa za maonesho. Pia, Sheria na Kanuni za kuzuia rushwa na uhujumu uchumi zimetayarishwa na kuanza kutumika. Sambamba na hilo, Serikali imeiimarisha Mamlaka ya Kuzuia Rushwa kwa kuwasomesha na kuwapatia mafunzo kwa vitendo watendaji wa Mamlaka hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kusimamia uwajibikaji na utawala bora kwa watendaji wa Serikali, Serikali imeimarisha Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa ujenzi wa majengo ya kisasa na uwekaji wa vifaa vya kisasa vya utunzaji kumbumbu wa kazi za ukaguzi pamoja na kuwapatia mafunzo ya muda mfupi na mrefu wafanyakazi wake katika fani za ukaguzi wa thamani (Value for Money Auditing) kwa lengo la kuiwezesha Ofisi hiyo kuimarisha kazi za ukaguzi na kutoa ripoti za ukaguzi zilizokuwa na viwango vinavyokubalika Kimataifa na kwa wakati muafaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kudumisha Muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kama ilivyoelekezwa katika Katiba ya Zanzibar kutokana na mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar ya 1984 Toleo la 2010. Aidha, Serikali imeendelea kuzingatia na kudumisha misingi ya kidemokrasia na utawala bora kwa kuhakikisha kuwa mihimili mikuu mitatu (Mahakama, Serikali, na Baraza la Wawakilishi) ya demokrasia na utawala bora inafanya kazi zake kwa uhuru bila ya kuingilia na chombo chengine. Vile vile, Serikali imefanya Mikutano na Vikao vyake vyote vya kisheria kwa lengo la kujadili Nyaraka kadhaa zikiwemo za Sheria, Sera pamoja na kupokea na kujadili taarifa mbali mbali.

 Aidha, mikutano mbali mbali kati ya Mheshimiwa Rais na Viongozi wa Wizara za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kujadili utekelezaji wa malengo ya bajeti imefanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuendeleza elimu hiyo ya muundo mpya wa Serikali yetu, Serikali imetoa elimu juu ya Mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Maafisa Wadhamini, Maafisa Tawala wa Mikoa na Wilaya pamoja na Wawakilishi wa Jumuiya za Kiraia Unguja na Pemba. Aidha, Serikali imetoa vipeperushi juu ya mfumo huo kwa ajili ya kutumika katika kutoa elimu hiyo kwa makundi mbali mbali ya kijamii. Pia, Viashiria vya Kitaifa vya Utawala Bora vimeandaliwa na kutumika kwa ajili ya kusimamia uwajibikaji na ufanisi katika utendaji wa Shughuli za Serikali.

OFISI YA MKURUGENZI WA MASHTAKA

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeanzisha Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar kwa mujibu wa Sheria ya Kuanzishwa kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Nam. 2/2010. Aidha, kitabu cha Muongozo wa Uendeshaji Mashtaka kimetayarishwa na kutumika. Vile vile, Serikali imejenga jengo jipya lenye Maktaba ya sheria ya kisasa yenye vitabu mbali mbali vya sheria ambapo Wafanyakazi na Wanasheria wa Serikali kutoka Taasisi mbali mbali pamoja na wanafunzi wa Sheria wanaitumia Maktaba hiyo. 

Aidha, Serikali imeendelea kuimarisha Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kwa kuwajengea nyumba za makaazi waendesha Mashtaka, kujenga kituo cha Mafunzo ya Sheria, kufanya matengenezo ya Kitengo cha Uendeshaji wa Mashtaka na kuwapatia fursa ya kujiendeleza kielimu watendaji wake.

Kuimarisha Kiwanda cha Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Saba inaendelea na mpango wake wa kukifufua Kiwanda cha Upigaji Chapa na Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali ili kuinua kiwango cha uzalishaji pamoja na kuongeza ubora wa huduma na bidhaa zinazozalishwa katika kiwanda hicho. 

Awamu ya Kwanza ya Mradi/Mpango huu tayari imeshatekelezwa ambapo shughuli zilizofanywa ni pamoja na kuyafanyia matengenezo makubwa majengo mawili ya kilichokuwa Kiwanda cha Sigara, Maruhubi kwa ajili ya kuweza kutumika kuwa Kiwanda cha Idara ya Upigaji Chapa na Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali. 

Aidha, Serikali imenunua na kufunga mashine za kisasa za upigaji chapa (Digital Printing Machines) na kutoa mafunzo ya muda mfupi ya utumiaji wa mashine hizo kwa watendaji. Kutokana na matengenezo hayo na uwekaji wa mashine kwa Awamu ya Kwanza, Kiwanda cha Upigaji Chapa na Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali hivi sasa kinatoa machapisho mbali mbali ya Serikali na sekta binafsi kwa kiwango bora na kwa wakati.

SERIKALI ZA MITAA NA IDARA MAALUM

Serikali za mitaa: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuendelea kuziimarisha Serikali za Mitaa, Serikali imefanikiwa kuandaa Sera ya Serikali za Mitaa na kufanikisha kufanya mapitio ya Sheria mbili (Sheria Nam.1 ya 1998 ya Tawala za Mikoa na Sheria Nam. 3 na 4 ya Baraza la Manispaa) na kuwa na Sheria Mpya Namba 8 ya mwaka 2014 ya Tawala za Mikoa na Sheria Namba 7 ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa ya mwaka 2015. 

Aidha, Serikali imewajengea uwezo wafanyakazi wa Serikali za Mitaa kwa kuwapa mafunzo ya muda mrefu na mfupi pamoja na ziara za kimasomo na kubadilishana uzoefu ndani na nje ya nchi. Pia, elimu juu ya kuanzisha mfumo madhubuti wa ukusanyaji na utunzaji wa mapato ya Serikali za Mitaa (Data base System) katika Taasisi za Halmashauri zote za Unguja na Pemba imetolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuboresha upatikanaji wa huduma za jamii katika miji ya Zanzibar kupitia Mradi wa Huduma za Jamii Mjini (Zanzibar Urban Service Project). Kupitia mradi huu uwezo wa kitaasisi wa Baraza la Manispaa Zanzibar na Mabaraza ya Miji ya Pemba umeimarishwa kwa kufanya ukarabati wa majengo, kutoa mafunzo kwa wafanyakazi na ununuzi wa vifaa vya ofisi yakiwemo magari na vifaa vya usafi. 

Aidha, Serikali imefanikiwa kuweka mazingira bora ya kazi kwa kujenga Ofisi za kisasa zinazokidhi mahitaji kwa Taasisi za Halmashauri za Unguja na Pemba. Pia katika kutoa huduma kwa wananchi Serikali imekuwa karibu na jamii katika kusaidia miradi ya maendeleo kwa kuwahamasisha wananchi kuunda Kamati za Maendeleo za Shehia na Majimbo ili kusimamia miradi ya maendeleo.

Idara/vikosi Maalum vya SMZ

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jitihada za kuviimarisha vikosi vya
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Serikali imetoa mafunzo ndani na nje ya nchi kwa wapiganaji wa vikosi hivyo katika fani mbali mbali. Pia Serikali imefanya matengenezo ya majengo, utoaji wa vifaa na ukarabati wa miundombinu ya maji na umeme kwa kambi zote za Unguja na Pemba ili kuleta ufanisi zaidi wa utendaji kazi kwa vikosi hivyo.

MFUKO WA HIFADHI YA JAMII

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii, Serikali imekamilisha uandaaji wa Sera ya Hifadhi ya Jamii na kuanza utekelezaji wake. Lengo la Sera hiyo ni kujenga mfumo wa hifadhi ya jamii unaolenga kutoa huduma bora za hifadhi kwa watu wote, hasa maskini na wanaoishi katika mazingira magumu zaidi. 

Aidha, Serikali kupitia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii imeanzisha Mfumo wa uchangiaji wa hiari (Zanzibar Voluntary Social Security Scheme) ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanafikiwa na kunufaika na matunda ya hifadhi ya jamii yanayotolewa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar pia umeweza kuwekeza katika miradi mbali mbali ya maendeleo, miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa viwanja vya kufurahishia watoto Kariakoo kwa Unguja na Tibirinzi kwa Pemba, ujenzi wa Mnara wa kumbukumbu ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar na ujenzi wa nyumba za makaazi. 

Aidha, Mfuko umeweza kutoa mikopo kwa Taasisi mbali mbali zikiwemo za Serikali na binafsi ikiwa ni moja ya njia ya kuwekeza fedha zinazotokana na michango ya wanachama wa Mfuko kama inavyoelezwa katika Sheria ya Mfuko ikiongozwa na Sera ya Uwekezaji ya Mfuko.

KUYAENDELEZA MAKUNDI MBALI MBALI

Watoto: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika juhudi za kuimarisha maslahi ya watoto wetu, Serikali imeandaa Sheria ya Mtoto ya 2011 na kutengeneza Kanuni 7 za kusimamia utekelezaji wa Sheria hiyo pamoja na uandaaji wa Sera na Mikakati mbali mbali yanayohusiana na hifadhi na maendeleo ya mtoto ambayo yanahusisha masuala ya hifadhi ya mtoto, usajili wa vituo na makaazi ya kulelea watoto, ukaazi na ulezi wa kambo pamoja na kinga maalum kuhusu hifadhi, ridhaa ya kupima Ukimwi na matibabu. 

Vile vile, Serikali inaendelea kuimarisha Mfumo wa hifadhi ya mtoto ikiwemo uanzishwaji wa mahakama za watoto. Aidha, Serikali imesimamia uundwaji wa Mabaraza ya Watoto nchini kwa lengo la kuwakutanisha watoto kuzungumza masuala yanayowahusu pamoja na changamoto zinazowakabili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuendeleza malezi bora ya watoto,
Serikali imekamilisha ujenzi wa nyumba ya kulelea watoto Mazizini na tayari watoto wanalelewa katika nyumba hiyo. Serikali pia, imeandaa na kuisambaza miongozo ya uanzishaji na uendeshaji wa nyumba za kulelea watoto kwa taasisi binafsi kwa lengo la kuimarisha malezi ya watoto katika vituo hivyo. 

Aidha, Serikali imefanya zoezi la kuvitambua vituo vya kulelea watoto na kusimamia utekelezaji wake. Vile vile, Serikali inaendelea na usajili wa kuwatambua watoto walio katika mazingira magumu kwa Unguja na Pemba.

Wanawake

Mheshimiwa Mwenyekiti, Katika utekelezaji wa Sera ya Hifadhi na
Maendeleo ya Wanawake ya mwaka 2001, Serikali imeweza kuwajengea uwezo na uthubutu wanawake wa kutumia fursa za kujiendeleza kiuchumi, kijamii na kisiasa. Wanawake wengi hivi sasa wameweza kumiliki mitaji na kufanya biashara kubwa na ndogo zinazoendesha maisha yao, familia zao na kuchangia uchumi wa taifa. 

Hali hii imetokana na Serikali kuvipatia mafunzo, kuvihamasisha, kuvishauri na kuvitembelea vikundi vya wanawake vya uzalishaji mali, wajasiriamali na SACCOS. Aidha, wanawake wameweza kujitokeza kugombea nafasi mbali mbali za uongozi ambapo idadi yao imeongezeka katika ngazi ya utoaji wa maamuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kupambana na vitendo vya udhalilishaji, Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Action AID imeanzisha nyumba salama kwa ajili ya kuwahifadhi na kuwahudumia waathirika wa vitendo vya udhalilishaji. 

Pia, Serikali imezijengea uwezo Kamati za Kupambana na Ukatili na Udhalilishaji wa Kijinsia kutoka ngazi ya Taifa hadi Shehia, kuunda mtandao wa kupambana na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia, kuandaa miongozo ya kufundishia na kushirikiana na viongozi wa dini katika mapambano hayo. 

Aidha, Serikali imefanya uchambuzi wa sheria na kanuni zinazohusiana na udhibiti wa vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia, ambapo imeweza kubaini mapungufu mbali mbali na baadhi ya mapungufu hayo tayari yameanza kufanyiwa kazi.

Vijana:

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa lengo la kuwaendeleza vijana, vikundi vya vijana vimefanyiwa tathmini ya mahitaji na changamoto zao ili kutafuta njia ya namna ya kuviendeleza vikundi hivyo. Pia, Serikali imekamilisha uandaaji wa Sheria na Kanuni ya kuanzisha Baraza la Vijana Zanzibar lenye lengo la kuwashirikisha vijana katika ngazi mbali mbali za maamuzi. Aidha, Baraza hilo tayari limeshaundwa na Katibu wa Baraza la Vijana tayari ameshateuliwa na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Aidha, Serikali imezindua mfuko wa uwezeshaji wananchi kiuchumi kwa kuiunganisha Mfuko wa Kujitegemea, Mfuko wa AK/JK na Mfuko wa Vijana ili kuweza kukabiliana na tatizo la ajira na kuinua uchumi wa Zanzibar. Vile vile, kwa mashirikiano na Taasisi mbali mbali za Serikali na Binafsi, Serikali imeendelea kuishughulikia changamoto ya upatikanaji wa ajira hasa kwa vijana nchini kwa kuwaorodhesha watafuta kazi kupitia Kituo cha Kutoa Taarifa za Soko la Ajira ili kuweza kuwaunganisha na waajiri. Jumla ya vijana 2,473 wameorodheshwa, ambapo vijana 1,978 wamefanikiwa kuajiriwa ndani na nje ya nchi kupitia Kituo hicho.

Wazee

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kutoa misaada ya kijamii kwa wazee wasiojiweza pamoja na kutoa posho la kujikimu wazee wenye watoto wanaoishi katika mazingira magumu zaidi. Vile vile Serikali inaendelea na kuihamasisha jamii kuendeleza utamaduni wa kuwaheshimu, kuwaenzi na kuwatunza wazee wetu. Kila ifikapo siku ya tarehe 01 Oktoba ya kila mwaka Serikali inasimamia na kuadhimsha siku ya wazee Duniani kwa lengo la kutathmini mafanikio na changamoto zilijitokeza katika jitihada za kuwatunza, kuwaheshimu na kuwaenzi wazee hao ikiwa ni pamoja na kuihamasiha jamii pamoja na wadau wengine kuongeza juhudi za kuendeleza mikakati hiyo nchini.

Watu Wenye Ulemavu

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuwa na takwimu sahihi za Watu Wenye Ulemavu na aina ya ulemavu walionao pamoja na kurahisisha upangaji wa Sera, Mikakati ya Mipango mbali mbali hapa nchini, Serikali imefanya usajili katika Wilaya zote za Unguja na Pemba katika ngazi ya Shehia.

Vile vile Serikali imeendelea kutoa elimu inayohusu mikataba, haki,
fursa na wajibu wa Watu Wenye Ulemavu katika Mikoa ya Unguja na Pemba. Serikali imetoa ruzuku na visaidizi kwa Jumuiya za Watu Wenye Ulemavu ili ziweze kutimiza malengo yao.

Wafanyakazi

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa wafanyakazi Serikali imefanya mapitio ya Sheria za Kazi, imetayarisha na kusambaza Kanuni za Sheria ya Ajira Nambari 11 ya mwaka 2005 na Kanuni za Utumishi wa Umma kwa wahusika wote. Kanuni hizo zinahusu mambo mbali mbali yakiwemo maslahi ya wafanyakazi katika sekta binafsi, usajili na utendaji kazi wa Vyama vya wafanyakazi, mikataba, likizo bila ya malipo na makundi maalum ya wafanyakazi.

SEKTA YA SHERIA

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuimarisha sekta ya sheria, Ilani ya CCM mwaka 2010-2015 imeagiza Serikali kuimarisha Mahakama kwa kujenga majengo mapya, kuzipatia vifaa vya kisasa, kujenga nyumba za Mahakimu Unguja na Pemba na kufanya marekebisho ya Sheria na Kanuni za Utendajikazi wa Mahakama. Katika kulitekeleza agizo hilo, Serikali imefanya matengenezo makubwa ya majengo ya Mahakama na kuziwekea vitendea kazi kwa Unguja na Pemba. 

Aidha, Serikali imeanzisha Kitengo kinachohusiana na masuala ya Mikataba, ambacho kina wataalamu wanaoshughulikia masuala yote ya mikataba ya Serikali. Pia, Serikali imewapatia mafunzo maafisa wa Sheria kutoka Taasisi mbali mbali juu ya uandishi wa sheria, utatuzi wa migogoro, ufungaji na uingiaji wa mikataba ya kitaifa na kimataifa. Mafunzo hayo yamedhaminiwa na Serikali kwa mashirikiano na UNDP kupitia Mradi wa Mageuzi katika Sekta ya Sheria (Zanzibar legal Sector Reform Program).

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kupunguza mrundikano wa kesi Mahakamani, Serikali imeajiri Mahakimu wapya na imeanzisha Kamati ya kusukuma kesi kwa kuwashirikisha wadau wote wa masuala ya kesi. Vile vile, Mahakama kupitia Mradi wa Mageuzi ya Sekta ya Sheria inaendelea na utaratibu wa kuanzisha mfumo wa kisasa wa usimamizi wa uendeshaji kesi (Case Management System).

Aidha, Serikali kupitia Programu ya Mabadiliko katika Sekta ya Sheria, imewapatia mafunzo Majaji, Mahakimu na waendesha mashtaka ili kuwazidishia ujuzi katika utendaji wa kazi zao za kila siku. 

 Aidha, Serikali imepeleka huduma za Mahakama karibu na wananchi kwa kuendesha vipindi vya redio na televisheni, mikutano ya hadhara katika Shehia na maskuli na kutoa na kusambaza kwa wananchi matoleo mbali mbali ya Jarida la Mahakama la Shahidi kwa ajili ya kuelimisha wananchi kuhusu huduma na masuala ya mahakama na jinai.

CHANGAMOTO ZILIZOATHIRI UTEKELEZAJI WA ILANI

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 hadi 2015, kulijitokeza baadhi ya changamoto ambazo Serikali ililazimika kutumia rasilimali zake chache ili kukabiliana nazo. Changamoto hizo ni pamoja na kutokea kwa vitendo au matukio yaliyoashiria uvunjifu wa amani, kutokea kwa maafa mbali mbali, ikiwemo kuzama kwa Meli ya Spice Islander huko eneo la bahari ya Nungwi na Meli ya MV Skagit katika maeneo ya Chumbe ambapo zaidi ya watu 1,600 walipoteza maisha.

Changamoto nyengine ni kutokea kwa upepo mkali katika maeneo mbali mbali ya visiwa vya Unguja na Pemba na kuleta uharibifu wa makaazi ya watu na mazao. Majanga haya yalipelekea kupoteza kwa nguvu kazi pamoja na matumizi makubwa kwa Serikali ambayo hayakutarajiwa. 

Aidha, Mfumko wa bei za vyakula uliotokana na tatizo la kupanda bei za mafuta na chakula katika soko la dunia, hasa katika miaka ya 2010 na 2011. Wananchi wengi hasa wenye kipato cha chini waliathirika na tatizo hilo kwa kushindwa kununua chakula na mahitaji yao mengine ya msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbali mbali walikabiliana na majanga hayo kwa pamoja, ikiwemo huduma za uokozi na huduma za kibinaadamu na kutoa pole kwa waathirika. Kwa upande wa mfumko wa bei, Serikali ilihamasisha wananchi hasa wakulima kuongeza bidii katika shughuli za kilimo na uzalishaji mali ili kuweza kupata chakula cha uhakika na kujiongezea kipato pamoja kutoa ruzuku katika pembejeo na matrekta katika kilimo na ushuru wa bidhaa za chakula zinazoingizwa nchini ili kudhibiti mfumko wa bei.

HITIMISHO:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla katika kipindi cha miaka mitano iliyopita (2010 - 2015), Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilitekeleza maagizo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa mafanikio makubwa ya wastani wa kiwango cha asilimia 90. Mafanikio haya kwa kiasi kikubwa yametokana na mashirikiano na mshikamano kati ya wananchi na viongozi katika ngazi mbali mbali katika jamii yetu kuanzia ngazi ya Shehia, Wilaya, Mkoa hadi Taifa. Kutokana na mafanikio yaliyopatikana ni dhahiri kwamba wananchi wameongeza imani ya Chama cha Mapinduzi na watakichagua tena kuongoza Serikali zote mbili (2) kwa kishindokikubwa katika Uchaguzi utakaofanyika mwezi Oktoba, 2015.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kutoa shukrani zangu kwa Sekta Binafsi, Asasi za Kiraia, Washirika wa Maendeleo na nchi marafiki kwa ushirikiano na mahusiano yao yaliyoiwezesha Serikali kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa sana. Tunaomba mashirikiano hayo yaendelee ili kuleta maendeleo ya kudumu katika nchi yetu na kuwaondoshea wananchi wetu umasikini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mara nyengine tena napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwako, kwa Wajumbe wote wa Kamati Kuu ya CCM pamoja na waalikwa wote. Nawashukuru wote kwa kunisikiliza kwa makini.
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.
Naomba kuwasilisha.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI

0 comments:

 
Top