Na,Jumbe Ismailly-Mkalama
WANANCHI wa Kijiji cha Ibaga,tarafa ya Kirumi,wilaya ya Mkalama,Mkoani Singida wanatarajia kutumia jumla ya shilingi 88,703,000/= kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa zahanati ya Kijiji hicho iliyoanza kujengwa mwaka 2013.
Hayo yamesemwa na afisa mtendaji wa Kijiji cha Ibaga,Bwana Hassani Kiyungi wakati akitoa ufafanuzi juu ya gharama zinazotarajiwa kutumika kukamilisha ujenzi wa zahanati hiyo inayosubiriwa na wakazi 5,190 wanaoishi katika kaya 865.
Aidha afisa mtendaji huyo amefafanua kwamba mpaka sasa mradi wa ujenzi wa zahanati hiyo umegharimu jumla ya shilingi 24,704,000/=,ambazo kati ya kiasi hicho cha fedha,nguvukazi ya wananchi zimeokoa shilingi 15,650,000/=,serikali kuu shilingi (CBD) 5,000,000/= na michango ya wananchi ni 4,054,000/=.
Kwa mujibu wa mtendaji huyo ili waweze kukamilisha ujenzi wa mradi huo mpaka sasa bado zinahitajika jumla ya shilingi 63,999,000/= na kwamba kwa maana hiyo kulingana na hali ya hewa iliyowakumba wananchi,alitumia fursa hiyo kuiomba serikali kuu iwasaidie kukamilisha mradi huo ili kunusuru afya za wananchi wa Kijiji cha Ibaga.
Hata hivyo mlinzi huyo wa amani wa Kijiji ameweka bayana kwamba zahanati hiyo itakapokamilika itawasaidia wananchi kupata huduma za afya ya matibabu kwa karibu,kwani mpaka sasa wananchi hufuata huduma katika Kituo cha afya kilichopo Kijiji cha Mkalama na wengine Kijiji cha Ilongo umbali wa kilomita tano kutoka hapo.
Aidha afisa mtendaji huyo hata hivyo amebainisha pia kwamba wananchi wengine wa Kijiji hicho hufuata huduma za afya katika Hospitali ya Misheni Haydomu,wilayani Mbulu,Mkoani Manyara,Hospitali ya misheni Nkungi,wilayani Mkalama na wengine wilayani Iramba.
Amefafanua kuwa mara zahanati hiyo itakapokamilika itawasaidia akina mama wajawazito kupatiwa huduma kwa ukaribu na maeneo wanayoishi na hivyo kutekeleza lengo la Wizara ya afya na Ustawi wa jamii la kusogeza huduma za afya umbali usiozidi kilomita nne kutoka kwenye makazi yao.
0 comments:
Post a Comment