Na,Jumbe Ismailly,Mkalama 
WIZARA ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi imepiga marufuku wanafunzi wa elimu ya awali katika shule za msingi nchini kukaa chini ya miti,na badala yake kila shule ihakikishe inakuwa na vyumba kwa ajili ya kusomea wanafunzi hao wa awali.

Akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Mkalama wakati wa ziara ya siku moja ya kutembelea eneo linalokaliwa na wanafunzi wa jamii ya kabila la wahadzabe baada ya kubaini kuwa wamekuwa na mwamko wa kupata elimu.

Naibu waziri wa elimu,ofisi ya Waziri mkuu,tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI),Kassimu Majaliwa alisema serikali kwa kushirikiana na Halmashauri ni lazima ihakikishe kila shule inakuwa na darasa la awali.

“Wote kwa pamoja lazima tuhakikishe kila shule inakuwa na darasa la awali,tumeshapiga marufuku wanafunzi wa elimu ya awali kukaa chini ya miti”alisisitiza Naibu waziri huyo wa Tamisemi.

Kwa mujibu wa Majaliwa moja ya mkakati wa kila Halmashauri ambao inatakiwa kufanya kila palipo shule ya msingi ni lazima pawe na darasa lililokamilika la elimu ya awali.

“Tunamtaka kila mtoto wa elimu ya awali anapokwenda shule aanze kupata Celling ya learning prosses kwa kuingia darasani na kukaa juu ya dawati,na kwa kuwa sasa tunaanza kuandaa kikamilifu walimu wa masomo ya elimu ya awali na kwa kuwa hatuna walimu wa kutosha wa kufundisha elimu ya awali,kila mwalimu anawajibika kufundisha darasa la awali”alifafanua.

Aidha Majaliwa hata hivyo alisisitiza kwamba kazi kubwa waliyonayo ni kumlea mtoto kutoka umri huo wa miaka mitano mpaka anapomaliza miaka 12 elimu yake ya msingi.

Kuhusu upungufu wa walimu,naibu waziri huyo aliweka bayana kwamba endapo kutakuwa na idadi kubwa ya walimu katika moja ya Halmashauri za Mkoa husika,katibu tawala wa Mkoa anao uwezo wa kuhamisha walimu kutoka Halmashauri moja kwenda Halmashauri nyingine ndani ya Mkoa kwa lengo la kuimarisha ikama.

Awali akisoma taarifa fupi ya maendeleo ya wilaya kwa naibu waziri kuhusu miundombinu,Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mkalama,Bravo Lyapembile alisema kuwa mahitaji ya vyumba vya madarasa ni 240,vilivyopo ni 178 na upungufu ni 62.

Hata hivyo kwa upande wa matundu ya vyoo,mkurugenzi mtendaji huyo alibainisha kwamba kati ya mahitaji ya matundu ya vyoo kwa wavulana ni 188,lakini yaliyopo ni 92 hivyo upungufu ni 96 huku kwa upande wa wasichana mahitaji ni 189,lakini yaliyopo ni 104 na upungufu ni 85.

Kwa upande wao baadhi ya watumishi wa Halmashauri,walionyesha wasiwasi wao juu ya maagizo ya naibu waziri yanayowataka wakurugenzi wa Halmashauri kulipa madeni ya likizo na uhamisho kwa watumishi wake kuwa ni jambo ambalo halitaweza kufanikiwa katika wilaya zote mpya zilizoanzishwa hivi karibuni.

Wilaya ya Mkalama ina jumla ya wanafunzi 36,152 wakiwemo wavulana 17,561 na wasichana 18,591 kuanzia darasa la kwanza hadi la saba na wanafunzi 6,808 wakiwemo wavulana 3,427 na wasichana 3,381 wa elimu ya Awali waliopo katika shule zote za msingi na hivyo kufanya jumla ya wanafunzi kuwa 42,222.

0 comments:

 
Top