Na,Jumbe Ismailly,Mkalama 
NAIBU Waziri wa Elimu,Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) amemwagiza Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mkalama kuhakikisha anawajengea matundu ya vyoo wanafunzi wa jamii ya kabila la wahadzabe wa kike wa shule ya msingi Munguli ili nao waweze kupata sehemu ya kujisaidia kwa nafasi badala ya ilivyo sasa ambapo wanachangia na wavulana.

Naibu waziri huyo,Kassimu Majaliwa alitoa agizo hilo alipokuwa akiongea na wazazi na wanafunzi wa shule ya msingi Munguli,iliyopo katika Kata ya Mwangeza,tarafa ya Kirumi kufuatia taarifa ya mkurugenzi huyo kwamba wanafunzi wa kike na wale wa kiume wanachangia matundu ya vyoo.

“Na leo nimemwambia mkurugenzi kati ya bweni na bweni kuna choo pale cha matundu mawili,ananiambia huku wavulana na kule wasichana,haiwezekani,tuamue tu lile jengo liwe la wavulana peke yao au wasichana peke yao’alibainisha naibu waziri huyo.

Alisema Majaliwa kwamba ni vyema wasichana wakajengewa matundu ya vyoo eneo mbali na wavulana ili kuwaepusha kukutana na wavulana hususani nyakati za usiku,kwani endapo utaratibu ulipo sasa utaendelea utahatarisha maisha ya wanafunzi hao wa kike watakapokuwa wakikutana usiku na wavulana chooni.

Hata hivyo Majaliwa hakusita kujizuia furaha yake kutokana na kitendo kilichofanywa na mkuu wa mkoa wa Singida,Dk.Parseko Kone cha kuifufua shule hiyo iliyojengwa katika kipindi cha utawala wa baba wa taifa,marehemu Julius Kambarage Nyerere,iliyokuwa imeanza kupoteza umaarufu wake.

Naye afisa elimu wa Halmashauri ya wilaya ya Mkalama,Mwisungi Kigosi alielezea changamoto zinazoikabili shule ya msingi Munguli kuwa ni pamoja na upungufu wa matundu ya vyoo vya wanafunzi,madawati,meza,viti,kabati,uhaba wa maji,chakula,mafuta ya kupikia,chumvi,sabuni na nguo za kubadilisha wanafunzi wa bweni.

Hata hivyo licha ya kuwepo kwa changamoto hizo,afisa huyo mwenye dhamana ya kusimamia sekta ya elimu alibainisha utatuzi wa changamoto hizo kuwa ni Miss Tanzania namba tatu ambaye pia ni Miss Singida namba moja Miss kanda ya kati,Dorothy Mollel ametoa msaada wa mablanketi 40 pamoja na vitabu.

Aidha Kigosi alisema pamoja na Miss Singida huyo kutoa msaada huo,vile vile aliahidi kutafuta wadau wa maendeleo kujenga maktaba ya kisasa itakayotumika kwa ajili ya wanafunzi hao.

Kwa upande wao baadhi ya wazazi na walezi wa wanafunzi hao,mwenyekiti wa jamii ya kabila la wahadzabe,Edward Mashimba alielezea kero zinazowakabili wananchi wa eneo hilo kuwa ni pamoja na ubovu wa barabara,mawasiliano ya simu na uvamizi katika hifadhi ya msitu waliokuwa wakiutegemea kujipatia chakula.

Wilaya ya Mkalama ina jumla ya vituo vitatu vya elimu nje ya mfumo rasmi (MEMKWA) katika shule za msingi Mwanga,Nkungi na Chemchemu huku ikiwa na shule binafsi moja inayomilikiwa na shirika la Dini la Roman Catholic yenye jumla ya wanafunzi 189,ambao kati yao wavulana ni 84 na wasichana ni 105.

0 comments:

 
Top