Benki ya kuhudumia wateja wadogo wadogo Tanzania { NMB } imeahidi kuendelea kutoa huduma za Kijamii katika maeneo mbali mbali Nchini Tanzania ili lengo la kuanzishwa kwake liweze kufikiwa kwa ufanisi.

Meneja Mkuu wa Idara inayoshughulikia masuala ya fedha ya Benki Hiyo Bwana Waziri Banabas alitoa ahadi hiyo wakati Uongozi wa Benki hiyo Tawi la Zanzibar ulipowaandalia futari ya pamoja baadhi ya wateja wake, Viongozi wa Taasisi tofauti Nchini pamoja na Wananchi.

Futari hiyo ya pamoja iliyoandaliwa ndani ya kumi la kwanza la rehema la Mwezi Mtukufu wa ramadhani imefanyika mara baada ya sala Magharibi kwa washiriki hao iliyofanyika katika Hoteli ya Zanzibar Ocean View Kilimani Mjini Zanzibar.

Meneja Mkuu huyo wa Idara inayoshughulikia masuala ya fedha ya Benki ya NMB Bwana Waziri Banabas alisema faida ya fedha zinazokusanywa na Benki hiyo kwa mujibu wa taratibu iliyojipangia hutolewa katika kusaidia sekta za afya pamoja na elimu.

Bwana Banabas alifahamisha kwamba kutokana na kukua kwa uchumi wa Zanzibar na wananchi wake kuhitaji huduma za Kibenki Uongozi wa NMB una mpango wa kuongeza Matawi pamoja na ATM ili kukidhi mahitaji ya wananchi hao.

Alisema Benki ya NMB Hivi sasa ina jumla ya Matawi 17 katika maeneo mbali mbali nchini Tanzania ambapo mawili kati ya hayo yapo kwa upande wa Zanzibar kiwango ambacho kinastahiki kuongezwa.

Akigusia changamoto za uhaba wa vifaa vya maabara katika Maskuli mengi hapa Zanzibar Meneja Mkuu huyo wa Idara inayoshughulikia masuala ya fedha ya Benki ya NMB Bwana Waziri Banabas alisema Uongozi wake utazingatia kwa kina tatizo hilo.

Alielezea matumaini yake kuona kwamba Benki ya NMB italipa kiapaumbele suala hilo kwa nia ya kulitafutia mbinu na ufumbuzi wa kudumu kwa lengo la kuwaondoshea usumbufu wa changamoto zinazowakabili wanafunzi wa Zanzibar.

Bwana Waziri Banabas amewapongeza Wananchi na wateja wote Nchini Tanzania waliosaidia kuifanya Benki ya NMB kuwa ya kwanza Tanzania kwa kukusanya shilingi Bilioni 156 mwaka uliopita.

Akitoa shukrani kwa niaba ya washiriki wa futari hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliupongeza Uongozi wa Benki ya NMB Kwa kujipangia utaratibu wa kusaidia huduma za kijamii licha ya jukumu lao la kukusanya mapato.

Balozi Seif alisema Benki ya NMB imeanzishwa maalum ili kuwapa nguvu Wananchi wa kipato cha chini kuapata mikopo ya kuwawezesha kiuchumi ili waendeshe maisha yao ya kila siku kwa matumaini makubwa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwataka Wananchi wote kuitumia Benki hiyo ya NMB katika shughuli zao za ujasiri amali ambazo ndio njia pekee itakayowakomboa kutokana na ukali wa maisha.

Alisema NMB yeye binafsi imemuwezesha kujenga mapenzi na upendo kwa Wananchi wa Jimbo lake la Kitope mara tuu baada ya kuchaguliwa kuwa Mbunge wao wa Jimbo hilo Mwaka 2005 kwa kupata mkopo mkubwa aliouelekeza katika kuanzisha miradi ya maendeleo ya Wananchi Jimboni humo.

Uongozi wa Benki ya NMB tayari umeshafutarisha Wateja na Viongozi wa Kisiwa cha Pemba na kuahidi kuendeleza utamaduni huo kila mwaka ili kuwapa fursa wateja wake kukaa pamoja na kubadilishana mawazo na fikra zitakazosaidia kuongeza ufanisi wa Benki hiyo.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top