Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema wakati harakati za uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 zimeanza kwa vyama vya siasa kutafuta wagombea wa nafasi mbali mbali za uongozi Viongozi pamoja na wananchi wanaweza kuchaguana bila ya kutukanana,kugombana nakuepuka kuhamasishana katika kufanya vurugu zinazoweza kuvuruga zoaezi zima la uchaguzi huo.

Alisema mafanikio yaliyopatikana kwa muda mrefu yanategemea kudumu kwa hali ya amani na utulivu kwa vile kila mwana jamii na mwananchi ana haki na wajibu wa kusimamia maendeleo hayo.

Akiufunga Mkutano wa 20 wa Baraza la Wawakilishi uliokuwa ukijadili Bajeti ya Serikali ya mwaka 2015/2016 katika ukumbi wa Baraza hilo Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar Balozi Seif alielezea matumaini yake kwamba wananchi wataendelea kuiamini na kuiunga mkono Serikali yao inayoongozwa na Rais kutoka CCM.

Alitanabahisha kwamba Serikali itahakikisha ulinzi na usalama unaimarika na haitokuwa tayari kumvumilia mtu au kikundi chochote kitakachovunja sheria na kuihatarisha amani na utulivu wa nchi.

Balozi Seif Ali Iddi alionya kwamba watu wasifikirie hata siku moja kwamba vikundi vinavyojitayarisha au kutayarishwa na wachochezi kufanya vitendo vya kuhatarisha amani ya nchi vinaikomoa Serikali, bali vielewe kwamba vinajikomoa vyenyewe.

Akizungumza bila ya uwepo wa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka Chama cha Wananachi { CUF } ndani ya kikao hicho Balozi Seif aliwaeleza wananchi kwamba yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana ndani ya Kipindi cha Kwanza cha Awamu ya Saba katika Sekta mbali mbali ikiwemo Afya, Elimu, Utalii, Maji, Miundombinu na Mawasiliano,Sekta za Uzalishaji viwandani, kilimo, mifugo na uvuvi.

Alisema mafanikio hayo ya kupigiwa mfano yametokana na utekelezaji sahihi wa Ilani ya CCM ya mwaka 2010 – 2015 chini ya usimamizi wa Rais wa Zanzibar ambae pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein ambapo hakuna shaka kwa mafanikio hayo Wananchi walio wengi watamrejesha tena kuiongoza Zanzibar iliyoamua kuwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye mfumo wa Umoja wa Kitaifa.

Balozi Seif alisema katika kipindi cha miaka mitano (2010 – 2015), Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetoa fidia ya jumla ya Shs. 7,129,591,148 za kuendeleza kilimo, kwa ajili ya ununuzi wa mbolea, madawa, mbegu na kutoa huduma za matrekta kwa wakulima.

Alisema hadi kufikia asilimia 5.6 mwaka 2014 hali inayotokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa ndani unaotokana na juhudi zilizochukuliwa na Serikali katika kuwapatia ruzuku za pembejeo wakulima hapa Nchini. 

Balozi Seif alieleza kwamba Kilimo bado kinaendelea kuwa muhimili Mkuu wa Uchumi wa Taifa kwa kutoa ajira kwa wananchi walio wengi na ndio maana Serikali ikalazimika kutekeleza mipango na miradi mbali mbali ya kilimo.

Akigusia sekta ya utalii inayoendelea kuimarika na kuwa tegemeo la kuongeza pato la Taifa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema idadi ya watalii walioingia Nchini imeendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka na kufikia watalii Laki 274,619 mwaka 215.

Alisema ongezeko hilo linatokana na kuimarika kwa miundombinu ya utalii pamoja na hali ya kudumisha amani na amewahakikishia watalii usalama wao kwa kipindi chote ambnacho watakuweo hapa Nchini.

Alifahamisha kwamba katika kuimarisha zaidi sekta ya Utalii Serikali imeamua kuibadilisha mandhari ya Hoteli ya Bwawani ambayo ina Historia kubwa baada ya kuatikana kwa mwekezaji ambae yuko tayari kuibadilisha hali hiyo.

Balozi Seif alisema Mazungumzo baina ya Serikali ya Mainduzi ya Zanzibar na Mwekezaji aliyechaguliwa kuendesha mradi huo yamefikia hatua nzuri na kinachobakia kwa sasa ni Serikali kumkabidhi mradi huo mwekezji husika na kufungaq naye mkataba.

Kuhusu Sekta ya miundombinu ya mawasiliano ya Bara bara Mtendaji Mkuu huyo wa Serikali alisema Serikali imejenga bara bara mpya kwa kiwango cha lami zenye urefu wa kilomita mia 243.85 na Bara bara nyengine zenye urefu wa kilomita 39.3 zimejengwa kwa kiwango cha kifusi na zile zenye urefu wa Kilomita 656 zimefanyiwa matengenezo mbali mbali.

Alisema miundombinu hiyo kwa kiasi kikubwa itasaidia kuimarisha uchumi wa Taifa na kutoa wito kwa wananchi pamoja na watumiaji wa bara bara hizo kuzitunza kwa faida yao na vizazi vijavyo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaasa wale watu wenye tabia ya kuzichoma bara bara hizo kwa makusudi kutokana na ushabiki wa kisiasa ni vyema wakaacha tabia hiyo yenye kuigharimu fedha nyingi Serikali Kuu katika kuzitengeneza upya.

Balozi Seif aliwashukuru na kuwapongeza Wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi kwa michango,mapendekezo na ushauri walioutoa wakati wa kuzijadili Hotuba za Bajeti zilizowasilishwa kwenye Baraza hilo la WEawakilishi Zanzibar.

Alisema katika Mikutano yote ya Baraza la Wawakilishi, Mkutano wa mwaka huu ulikuwa wa kupigiwa mfano kwa kupitishwa bajeti zote kwa urahisi na bila ya pingamizi zozote.

Balozi Seif alieleza kwamba upitishwaji wa Bajeti hizo ulikuwa rahisi kutokana na sababu ya kutumia mfumo mpya wa Bajeti uitwao Program Based Bujet { PBB } uliosaidia kupunguza vikwazo kutoka kwa Wajumbe wakati wa Kamati.

Baraza hilo la Wawakilishi la Nane tokea kuasisiwa kwake hadi sasa limeshafanya jumla ya Mikutano 20 katyika Mikutano ambayo jumla ya maswali ya msingi 1,630 na yale ya nyongeza elfu 3,277 yameulizwa kwa Serikali na kujibiwa.

Baraza hilo pia limefanikiwa kujadili na kupitisha miswada ya sheria ipatayo 63 na hatimae kutungwa kwa sheria kutokana na miswada hiyo pamoja na kuidhinisha Bajeti ya Serikali na Mawizara mara Tano hadi kipindi hichi Bajeti ambazo zimesaidia kufanikisha kupatikana kwa maendeleo makubwa hapa nchini.

Othman Khamis Ame
Ofisiya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top