Uwekezaji katika maeneo maalumu ya kilimo nchini Tanzania ulichangia kuongeza kwa mavuno katika mazao kama vile mpunga, mahindi, au nyanya kwa kiwango cha kati ya asilimia 60 hadi 120 kule ambako umwagiliaji na huduma za ugani zilitolewa kwa kiwango cha kutosha, mpango mpya wa nchi wa tathmini ulioendeshwa na Ofisi Huru ya Tathmini ya Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), uliowasilishwa leo jijini Dar es Salaam, umeonyesha.

Msaada wa Mfuko wa IFAD nchini Tanzania ni wa pili kwa ukubwa (kwa maana ya kiasi cha utoaji mikopo) katika ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika, baada ya Ethiopia. Tangu IFAD inaanza shughuli zake nchini mwaka 1978, imetoa fedha kwa miradi ya uwekezaji inayotumia mikopo ipatayo 14 yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 360, na Mfuko umehamasisha msaada wenye thamani inayozidi Dola za Marekani milioni 700 kwa miradi ya maendeleo ya kilimo. Serikali imeshiriki katika utoaji fedha kwa kiwango cha Dola za Marekani milioni 72, au asilimia 10 ya gharama nzima. Michango ya nyongeza ilitolewa na wafadhili wengine, hasa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Benki ya Dunia na serikali za Ubelgiji, Japani na Ayalandi.

Tathmini ilipendekeza kwamba msaada wa IFAD katika awamu inayofuatia katika Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo – ambayo ni programu ya serikali inayolenga kuongeza uwezo wa wakulima kupata na kutumia maarifa ya kilimo, teknolojia, mifumo ya masoko na miundombinu, Bara na Zanzibar.
“Kwa upande wa Unguja na Pemba peke yake, msaada wa IFAD kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo umesaidia zaidi ya wakulima 35,000, ambapo asilimia 62 ni wanawake,” alisema Nadine Gbossa, Mkuu wa Ofisi ya Kanda ya IFAD ya Nairobi. “Programu hii inaweka mkazo katika shughuli za ugani, kwa kutumia njia ya ubunifu ya Farmer Field School. Serikali imechukua njia hii kama sehemu ya sera na mikakati yake , na sasa inaiingiza katika programu zake. Haya ni mafanikio makubwa kwa IFAD kama mshirika.”

Ripoti ya tathmini ilionyesha jinisi IFAD na washirika wengine wa maendeleo walivyo muhimu katika kusaidia sera ya Tanzania ya upelekaji madaraka mikoani, jambo ambalo linalenga kupeleka utoaji uamuzi katika kupanga na kutekeleza miradi kwa mamlaka za serikali za mitaa. Hata hivyo, tathmini hiyo ilikuta maendeleo kidogo katika kusaidia upatikanaji wa masoko ya mazao ya kilimo na suala la kuongeza thamani kwenye mazao.

Ripoti huru ya tathmini—ya pili ya aina yake nchini Tanzania—itatoa mwanga kwa mkakati unaofuata wa IFAD nchini mwishoni mwa 2015. “Mkakati unaofuata wa IFAD nchini ni fursa ya kuendeleza matokeo ya shughuli za ugani katika kilimo na kuweka mkazo katika utafutaji masoko na uongezaji thamani kwa mazao ya kilimo, na vilevile kuimarisha shughuli zisizo za utaoaji mikopo, zikiwemo usimamizi wa maarifa, mazungumzo kuhusu sera na kujenga ushirikiano,” alisema Oscar A. Garcia, Mkurugenzi wa Ofisi Huru ya Tathmini. "Zaidi ya hayo, kuna nafasi ya kupanua ushirikishwaji wa sekta binafsi na kutafiti uratibu zaidi wa msaada kwenye kuongeza thamani kwa kushirikiana na washirika wengine wa maendeleo nchini Tanzania,” aliongeza.
Ripoti kamili ya tathmini inatarajiwa kutolewa mwezi Aprili, 2015.

0 comments:

 
Top