sekta ya utalii ni mchangiaji mkubwa kwa uchumi wa Tanzania. Toleo la sasa la Hali ya Uchumi wa Tanzania linalochapishwa na Benki ya Dunia linadai kwamba sekta hii inaweza kukua na kujenga ajira nyingi zaidi, hususani katika ajira zinazolipa vizuri, pia inaweza kuunganisha biashara na wana jamii wa maeneo husika. Ili kuweza kutumia fursa hii, serikali inapaswa kupitia upya wajibu wake kwa kurahisisha mfumo wa kodi na ushuru, na kufanya mgawanyo wa mapato kuwa wazi zaidi.

“Hapana shaka kwamba Tanzania ni mahali pazuri kadri utalii wake unavyohusika,” anasema Philippe Dongier, Mkurugenzi wa Benki ya Dunia kwa nchi za Tanzania, Burundi na Uganda. “Tanzania ina maliasili nyingi ambazo zinaweza kuendeleza sekta hii, na inafahamika vyema kimataifa pamoja na karibu kila mwaka huandikwa katika gazeti la New York Times. Nchi hii ilipokea wageni milioni moja mwaka 2013, ambao waliliingizia taifa Dola za Marekani bilioni 1.5 katika fedha za kigeni, kiasi ambacho ni kikubwa kwa hali yoyote ile. Lakini kuna uwezekano wa kukua zaidi, kama ambavyo pia imesisitizwa na Serikali; na baadhi ya maboresho yanayohitajika ni ya haraka sana kwani hali kubaki kama ilivyo ni gharama kwa nchi.”

Utalii huajiri moja kwa moja takribani Watanzania nusu milioni na huchangia karibu asilimia 20 ya bidhaa zinazouzwa nje. Huwakilisha takribani asilimia 3.4 ya Pato Ghafi la Taifa la Tanzania (GDP), lakini kiwango hiki kinaweza kufikia makadirio ya asilimia 10 unapochukulia mchango wake ambao si wa moja kwa moja katika sekta nyingine kama vile kilimo na uchukuzi. 
 
Kutokana na hali hii, sekta hii inachukuliwa kuwa ni ya kipaumbele chini ya ajenda ya maendeleo ya Rais Jakaya Kikwete, lakini pia na ile ya Baraza la Taifa la Biashara. Sekta ina lengo la kuongeza mapato yatokanayo na utalii mara nane ifikapo mwaka 2025, au kuongeza kiwango cha ukuaji wa sekta maradufu kwa kila mwaka kama inavyoonekana katika miaka ya hivi karibuni. “Lengo hili kwa hakika linafikika lakini ni pale tu iwapo kutakuwa na mabadiliko katika sera na mitazamo miongoni mwa wadau wote,” anasema Jacques Morisset, Mchumi Mkuu wa Benki ya Dunia kwa nchi za Tanzania, Burundi, na Uganda, aliyeandika ripoti hii.

Ili kuongeza manufaa ya sekta hii kwa uchumi na watu, toleo hili la Hali ya Uchumi linapendekeza mielekeo mitatu ya kimkakati:

Mwelekeo wa kwanza ni kupanua shughuli za utalii kuwa anuwai tofauti na msisitizo wa sasa ambao unatoa umuhimu kwa utalii wa gharama kubwa katika kanda ya kaskazini kuzunguka Arusha na Zanzibar ambako hadi asilimia 90 ya shughuli za utalii ndiko ziliko kwa sasa. Ripoti inapendekeza kuchangamkia fursa nyingine, hususani maeneo ya Kusini, na kutayarisha shughuli ambazo zitawavutia watalii wenye bajeti za chini na kati, ikijumuisha watalii wa ndani na kutoka katika kanda.

Mwelekeo wa pili ni kuongeza juhudi za kuwaunganisha wana jamii wa maeneo husika na wafanyabiashara wadogo wa utalii katika shughuli za utalii, kupitia michakato ya kugawana faida. Wakati tayari juhudi hizi zipo nchini Tanzania, ni kwa kiwango cha chini na hazijaleta mabadiliko katika jamii. Ripoti inazungumzia utendaji bora ambapo programu za mafunzo na kuunganisha jamii hutayarishwa kwa pamoja baina ya sekta za umma na binafsi, hii imeleta viwango vya juu vya ubora wakati huo huo ikiongeza ushiriki wa jamii ya wafanyabiashara na wafanyakazi wa maeneo hayo katika shughuli za utalii.

Mwelekeo wa tatu unataka pafanyike mapitio ya mfumo wa sasa wa kodi na ushuru ambao ni mgumu kuuelewa, mapitio hayo pia yaguse matumizi yasiyo wazi ya mapato yaliyokusanywa kutoka utalii. Ripoti ya Hali ya Uchumi inapendekeza kwamba mfumo wa kodi na ushuru ufanywe kuwa rahisi na kutekelezwa kwa usawa zaidi kwa lengo la kupunguza gharama za uendeshaji wa biashara na kuziba mianya ambayo inatoa nafasi kufanya malipo haramu. Aidha, mgawanyo wa mapato urasimishwe ili iwe rahisi kufuatilia na kuongeza manufaa kwa wananchi walio wengi. Serikali pia lazima iongeze usimamizi wa maliasili kupitia matumizi ya busara ya motisha na vikwazo ili kulinda wanyama walio katika hatari ya kutoweka pia na matumizi bora ya ardhi na maji.

Mbali na mjadala wa Utalii wa Tanzania kama mada maalum ya toleo hili la Hali ya Uchumi wa Tanzania, chapisho hili pia linachambua hali ya uchumi. Tathmini mpya ya hivi karibuni ya Pato Ghafi la Taifa (GDP) na utafiti wa bajeti ya kaya ya hivi karibuni imekosoa mtazamo tuliouzoea wa uchumi wa Tanzania. Kipato cha wastani kwa mwananchi wa Tanzania ni Dola za Marekani 950, kiwango kilicho karibu zaidi kuliko mwanzo kwa nchi kufikia hadhi ya kipato cha kati, na kiwango cha umasikini kimepungua kutoka asilimia 33 mwaka 2007 hadi asilimia 28 mwaka 2012. Wakati huo huo uchumi ukiendelea kupanuka kwa takribani asilimia 7 mwaka 2014, na mfumuko wa bei ukidhibitiwa katika wastani wa asilimia 5.

“Udhaifu mkubwa katika usimamizi wa uchumi mkuu wa Tanzania unabakia kuwa ni sera yake ya fedha, na ni muhimu Serikali ikarekebisha hali hii,” anasema Morisset.

Hatua za haraka zinahitajika kuchukuliwa ili kushughulikia hatari za kifedha zinazoikabili bajeti ya Serikali kwa sasa kutokana na kutokufikia malengo yake ya mapato, madeni ya mifuko ya pensheni na makandarasi, na wabia wa maendeleo kuendelea kugoma kutoa msaada wa bajeti kumesababisha Serikali kuendelea kukopa kutoka soko la fedha la ndani. Ijapokuwa Serikali inaonekana iko tayari kuchukua hatua stahiki kushughulikia hatari hizi, ripoti inaonya kwamba hakuna nafasi ya kubweteka wakati nchi inajiandaa kwa kura za maoni mwezi Aprili 2015 kuhusu katiba iliyopendekezwa na uchaguzi mkuu mwezi Oktoba, 2015.

0 comments:

 
Top