Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba jukumu la Wazazi na Walezi Nchini bado litaendelea kubakia pale pale katika kuhakikisha kwamba wanasimamia vyema watoto wao kupata Elimu kadri ya uwezo wa watoto hao utakavyowaruhusu.

Alisema ile tabia ya kuwaharakisha watoto wao katika maisha yao hasa wale wa kike kuwaozesha mapema waelewe kwamba wanawadumaza katika kupata wataalamu na viongozi bora wa hapo baadaye.

Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza hayo wakati wa hafla fupi ya kukabidhi vifaa mbali mbali vya ujenzi kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa jengo jipya la Skuli ya Msingi ya Kinduni iliyomo ndani ya Jimbo la Kitope Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Vifaa hivyo ambavyo ni pamoja na Matofali, Nondo, Saruji, Mchanga na Kokoto vitasaidia nguvu za Wananchi wa Kijiji cha Kinduni walioamua kukabiliana na ufinyu na nafasi za Madarasa kwa watoto wa Kijiji hicho na vile vya jirani.

Balozi Seif alisema kundi kubwa la watoto kwa kushirikiana na wazazi wao walioamua kutafuta elimu kwa njia zote ndilo litakalofanikiwa kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya Teknolojia katika karne ijayo.

“ Karne ijayo ni ngumu sana na watakayoiwahi watalazimika kuwa na taaluma ya kutosha. Hivyo watoto wanapaswa kuacha mchezo na kuitafuta elimu kwa gharama yoyote ile ”. Alisisitiza Balozi Seif.

Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope amewapongeza Walimu wa Skuli ya Kinduni kwa juhudi wanazochukuwa katika kuwapatia elimu wanafunzi wao na kufanikiwa kupasisha wanafunzi wengi waliyoipatia sifa skuli hiyo kushika nafasi ya Tatu Kitaifa kwa wanafunzi walioingia Mchepuo.

Aliwaahidi walimu, wanafunzi na Wazazi wa Kinduni kwamba Uongozi wa Jimbo hilo utajitahidi katika kusimamia ujenzi wa jengo jipya na limalizike kwa wakati ili kukabidhiwa Wizara ya Elimu kwa hatua ya ukamilishaji.

“ Mimi Kama Kiongozi wenu Napata faraka na matumaini kuona hakuna Mtoto ye yote anayekaa chini kwenye Skuli yenu wakati anapoendelea na masomo yake ya kila siku ”. Alisisitiza Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope.

Akizungumzia changamoto zinazoikabili skuli hiyo likiwemo upungufu wa walimu Balozi Seif alisema suala hilo analichukuwa kwa hatua ya kuzungumza na Uongozi wa Wizara ya Elimu ili kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Aliahidi pia kwamba juhudi za makusudi zitachukuliwa na Uongozi wa Jimbo hilo katika kuipatia vifaa vya Maabara na Maktaba Skuli hiyo ili wanafunzi wake kuwa tayari wakati itakapanzishwa skuli ya Sekondari.

Akitoa Taarifa fupi ya Skuli ya Msingi Kinduni Mwalimu Mkuu wa Skuli hiyo Bibi Miza Omar Moh’d alisema mchango wa Mbunge wa Jimbo la Kitope kwa Skuli hiyo iliyoanzishwa mwaka 2009 unaendelea kuleta faraja kwa wazazi, walimu na wanafunzi wa skuli hiyo.

Mwalimu Miza alisema licha ya changamoto ya upungufu wa walimu, ukosefu wa huduma za maji safi na salama, maabara na Maktaba lakini lengo la Kamati ya Uongozi ya Skuli hiyo ni kuona Kijiji cha Kinduni kinakuwa na Skuli ya Sekondari.

Akitoa nasaha zake Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “B” Nd. Haji Makungu Mgongo alisema kutokana na mazingira bora yanayoendelea kuwekwa na Kamati ya Skuli ya Kinduni hakuna sababu yoyote kwa mwanafunzi wa Skuli hiyo asisome kwa Bidii.

Nd. Mgongo alisema wazazi na walezi lazima wahakikishe kwamba watoto wao wanapatiwa elimu kwa lazima kwani ndio njia pekee itakayowafungulia njia bora za maisha yao ya baadae.

Katika Kuunga mkono jitihada za walimu, wazazi ,a Kamati ya Skuli ya Kinduni Mke wa Mbunge wa Jimbo la Kitope Mama Asha Suleiman Iddi alichangia shilingi Milioni Moja katika kusaidia uendelezaji wa jengo jipya la skuli hiyo.

Mama Asha pia akaahidi muda mfupi ujao kupeleka mafundi kwa ajili ya uchimaji wa kisima kitakachosaidia kuondosha kero linalowakabili wanafunzi wa Skuli hiyo la kupata huduma za maji safi na salama.

Wakati huo huo Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi alifika Kijiji cha Mgambo kumfariji Bwana Ame Khamis Chumu ambae hivi karibuni duka lake lilipatwa na maafa ya kuungua moto.

Bwana Ame alimueleza Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope kwamba moto huo umesbabisha kuungua kwa bidhaa zake zote zilizomo ndani ya duka hilo jambo ambalo limempa hasara za zaidi ya shilingi laki nane.

Balozi Seif ambae alimkabidhi baadhi ya vifaa na vyakula ili visaidie kukidhi mahitaji yake ya lazima alimuomba Mfanyabiashara huyo kufanya tathmini ya hasara hiyo na yeye ataangalia uwezekano wa kiusaidia matengenezo ya mlango wa duka hilo.

Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope pia akapata fursa ya kumpa pole Bibi Asha Ali Foum wa Kijiji cha Pangeni ambaye Paa la Banda analoishi liliwaka moto ambao hadi sasa bado chanzo halisi kimebakia kuwa na Utata.

Bibi Asha alisema moto huo uliibuka wakati harakati za mapishi zimeshakamilika na moto uliopo jikoni mwa Banda hiLo kuzimwa kabisa jambo ambalo limewapa fadhaa kutokana nakuibuka kwa moto huo uliounguza nguo na vifaa vyote vilivyokuwemo ndani humo.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top