Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameipongeza Serikali ya Watu wa Marekani kupitia Shirika lake la Misaada ya Maendeleo la Us aid kwa jitihada zake za kuisaidia Zanzibar katika mipango yake ya kutafuta mbinu za kuwa tayari kwa kukabilana na maafa wakati wowote yatapotokezea.

Alisema Zanzibar imekuwa na historia pana ya majanga mbali mbali yaliyowahi kuikumba na kusababisha maafa makubwa yatayoendelea kukumbukwa na vizazi vya sasa na vile vijavyo.

Balozi Seif alitoa pongezi hizo wakati akifungua rasmi mafunzo ya siku tano kuhusu zoezi la kukabiliana na maafa Zanzibar yanayofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mazizini nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Alisema Marekani imekuwa mshirika mkubwa katika kusaidia harakati mbali mbali za maendeleo ya miundo mbinu ya mawasiliano ya Bara bara, huduma za Afya na ustawi wa Jamii wa Zanzibar jambo ambalo limekuwa likileta faraja kwa Wananchi walio wengi hapa Nchini.

Balozi Seif alifahamisha kwamba juhudi za Zanzibar katika kujiweka tayari kukabiliana na maafa yoyote yatakayoweza kutokea zimekuja kufuatia majanga tofauti yaliyowahi kutokea kama maradhi ya Kolera, ajali za vyombo vya usafiri wa Baharini na majanga ya moto ambayo yamesababisha vifo vya watu kadhaa.

“ Zanzibar imeshuhudia maradhi ya kolera karibu miaka 20 iliyopita na kukumbwa na ajali za usafiri wa Baharini miaka michache iliyopita na kulazimika kuchukuwa jitihada za tahadhari katika kukabiliana nayo endapo yatatokezea tena “. Alisema Balozi Seif.

Alifahamisha kwamba Zanzibar ikiwa miongoni mwa Mataifa machanga Duniani inawajibika kuimarisha Idara yake ya Maafa kwa kushirikiana na taasisi za ulinzi, Afya na Mawasiliano ili kuona huduma za kukabiliana na maafa Nchini zinapatikana kwa ubora unaokusudiwa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kuwa ile nia ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kujenga vituo vya mafunzo na uokozi wakati yanapotokea maafa katika eneo la Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja na Chake chake kwa Pemba bado iko pale pale.

Alisema kilichokwamisha utekelezaji wa mpango huo kwa sasa ni upatikanaji wa vifaa na fedha licha ya juhudi kadha zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali kuu katika kuomba misaada ya kiufundi kwa Taasisi za Kimataifa zilizobobea katika taaluma hiyo muhimu.

Balozi Seif alieleza kuwa katika kuimarisha huduma za kukabiliana na maafa Nchini Mswada wa Sheria ya Kuanzisha Sheria ya Kupunguza na Kukabiliana na Maafa Zanzibar uliwasilishwa na kujadiliwa na Baraza la Wawakilishi Zanzibar hivi karibu na hatimae kupitishwa katika Mkutano wa 18 wa Baraza hilo.

Alisema Mswada huo ulikusudiwa kuweka sheria mpya inayoweka mfumo wa kisheria katika shughuli za kukabiliana na maafa na mambo ambayo yataondosha mapungufu yanayoonekana katika sheria iliyopo hivi sasa.

Balozi Seif alisisitiza kwamba Sheria hiyo mpya itawiana na Sera ya Kukabiliana na Maafa ya mwaka 2011 pamoja na Makubaliano na Mikataba ya Kikanda na Kimataifa inayohusiana na masuala ya kukabiliana na maafa iliyoridhiwa na nchi yetu.

Mapema Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Ahmad Kassim alisema lengo la zoezi hili la kukabiliana na maafa Zanzibar ni kujenga nguvu za pamoja kati ya Taasisi za Umma, binafsi zikiungwa mkono na washirika wa maendeleo .

Nd. Ahmad alisema kwa vile majanga yanapotokea yanakumba kila kilichoko mbele yake ushirikiano wa karibu unahitajika kwa pande zote zinazohusika ili kujiweka tayari kukabiliana na majanga yoyote yanapotokezea.

Wakitoa salamu za Taasisi zao za kimataifa zinazoshiriki zoezi hilo Mwakilishi wa Shirika linalosimamia huduma za Kibinaadamu na Afya la Usafricom Kamanda Philip Knightsheen na Mwakilishi wa shirika la Misaada la Marekani Us Aid Bibi Anna Senga walisema suala la ulinzi wa maisha ya Mwanadaamu linamuhusu kila mwana jamii.

Walisema licha ya kwamba nguvu kubwa imewekwa kwa vikosi vya ulinzi na uokozi kukabiliana na maafa yanapotokea, lakini bado jukumu hilo litaendelea kusimamiwa kwa pamoja na taasisi zote za umma,binafsi kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo.

Wawakilishi wa taasisi hizo za Kimataifa walisema kwamba Nchi za Malawi, Msumbiji na Senegal zinazokuwa zikikabiliana na mafuriko ya mara kwa mara zimekuwa zikipata msaada ya kibinaadamu kwa lengo la kuwapa matumaini wananchi wake wanaokumbwa na kadhia hiyo.

Waliahidi kwamba Taasisi na mashirika ya maendeleo ya Kimataifa wakiyatolea mfano yale ya Unicef, WHO,Usafricom,CDHAM na mengine ya kujitolea yataendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kukabiliana na majanga na maafa wakati yanapotokea.

Akimkaribisha mgeni rasmi kufungua zoezi hilo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Moh’d Aboud Moh’d alizishukuru Taasisi inayohudumia masuala ya Kibinaadamu na Afya { USAFRICOM } na ile ya kujikinga na Majanga ya Kibinaadamu { CDHAM } kupitia Serikali ya Marekani kwa kukubali kugharamia mafunzo ya zoezi hilo.

Waziri Aboud alisema msaada wa Taasisi hizo utasaidia kuwawezesha washiriki wa mafunzo hayo kutoka Mataifa mbali mbali rafiki kupata taaluma pana itayoweza kuwasaidia katika kutekeleza majukumu yao kwenye taasisi wanazotokea.

Mafunzo hayo ya siku tano kuhusu zoezi la kukabiliana na maafa Zanzibar yanayofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Zanzibar Beach Resort yameshirikisha wawakilishi wa Taasisi za ulinzi, maafa, Utawala, pamoja na wataalamu wa Afya kutoka nchi mbali mbali Duniani.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top