Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi amewaasa wana CCM Nchini kutafakari kwa makini wimbi la Wanachama walioanza harakati za kuomba kuteuliwa kuwa wagombea wa nafasi za Uongozi kabla ya wakati maalum ulipangwa na chama kwa mujibu wa katiba na miongozo iliyowekwa.

Alisema CCM itamteua mwanachama mwenye sifa zinazozingatia maadili na miongozo ya Chama kugombea nafasi ya Uongozi baada ya wanachama hao kuwachambua wahusika hao katika vikao vitakavyowahusu kwenye maeneo yao.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa nasaha hizo wakati wa hafla fupi ya kulizindua jengo la Ofisi ya Tawi jipya la CCM la Kijiji cha Ghana shughuli aliyoifanya sambamba na Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Taifa Mzee Ali Hassan Mwinyi ndani ya Jimbo la Uzini Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusni Unguja.

Ujenzi wa Tawi hilo la CCM uliofanywa na Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mh. Moh’d Raza Hassanali umekuja kufuatia lile la mwanzo lililojengwa na Mbunge wa Jimbo hilo Mh. Moh’d Seif Khatib mwaka 2000 kupata athari wakati wa ujenzi wa bara bara.

Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema licha ya kwamba Chama cha Mapinduzi kina utajiri mkubwa wa Viongozi wa kuongoza Dola ya Tanzania lakini bado wanachama na wananchi wanapaswa kuwa makini kuwapima viongozi wanaokusudia kuwachagua ili wawaongoze.

Alieleza kwamba zipo nchi kadhaa Duniani ambazo wananchi wake walidanganywa na kupewa matumaini makubwa ya maisha kiasi kwamba sasa wanaishi katika maisha ya dhiki na udhalili.

“ Wanachama wa CCM lazima wawe makini na hadhari na Watu wanaotafuta fursa za kutaka kuongoza kabla ya wakati uliopangwa kwa mujibu wa katiba, sera na miongozo ya chama “. Alitahadharisha Balozi Seif.

Akizungumzia upigaji wa kura ya maoni na uchaguzi Mkuu unaolikabili Taifa ndani ya mwaka huu wa 2015 Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Balozi Seif alitanabahisha kwamba vyombo vya dola vitakuwa makini katika kukabiliana na vikundi au mtu ye yote atakayeamua kusababisha vurugu kwenye chaguzi hizo.

Alisema mbinu za kisiasa zilizokuwa zikitumiwa na baadhi ya wafuasi wa vyama vya kisiasa kwa kuwatumia vijana katika kuvuruga amani ya nchi zinaeleweka na kamwe Serikali zote mbili hazitakuwa tayari kuona amani hiyo inachezewa kizembe.

“ Kwanini Serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi viwaachie watu wasababishe vurugu na uvunjifu wa amani ya Nchi ? “. Aliuliza Balozi Seif.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa amempongeza Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mh. Moh’d Raza kwa kusimamia ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Chama Tawi la Ghana akionyesha kutekeleza kwa vitendo agizo la CCM la kuwataka wanachama wake wajenge Ofisi zitakazofanana na chama chenyewe.

Balozi Seif alisema ukamilikaji wa ujenzi huo wa Ofisi utawapa fursa nzuri wanachama wa Tawi hilo kufanya vikao vyao ndani ya ofisi na kuacha tabia ya kurundika vikao kwani waelewe kwamba nje ya vikao ni kukaribisha fitina zitakazozaa makundi na kukigawa chama.

Akimuunga mkono Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mh. Moh’d Raza Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Balozi Seif aliahidi kuwasaidia Wanachama wa Tai la Ghana Seti ya TV, Deki pamoja na King’amuzi chake ili kuwapa fursa wanachama na wananchi wa Kijiji hicho kupata Habari na Matukio mbali mbali ya Kitaifa na Kimataifa.

Akisoma Risala ya Wana CCM wa Tawi la Ghana Katibu wa Tawi hilo Bibi Khadija Awadh Omar alisema Tawi lao lilijengwa mwaka 2000 lakini ujenzi wa Miundo mbinu ya Bara bara liyopita pembezoni mwa Jengo hilo umesababisha ubovu wa jengo hilo.

Bibi Khadija alisema Jengo hilo limeanza kujengwa tena mnamo Tarehe 24 Oktoba mwaka 2014 chini ya usimamizi wa Mwakilishi wa Jimbo hilo ambapo hivi sasa liko tayari kwa matumizi na lina vifaa vyake kamili vya ofisi ikiwemo huduma za umeme.

Naye Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mh. Moh’d Raza akitoa shukrani zake kwa kuungwa mkono wana CCM na wananchi wa Jimbo hilo katika ujenzi wa Jengo hilo alihimiza umuhimu wa ushirikiano utakaoongeza nguvu za kuleta faraja kwa masuala yoyote watakayoamuwa kuyapanga.

Mh. Raza aliwaahidi wanachama hao wa CCM na Wananchi hao kwamba Uogozi wa Jimbo hilo utahakikisha kwamba bara bara zote za ndani zilizomo kwenye Jimbo hilo zinashughulikiwa ipasavyo ili kuwapa unafuu wa mawasiliano ya usafiri wananchi wa vijiji hivyo.

Akitoa salamu zake kwenye hafla hiyo Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Taifa ambae pia ni Rais Mstaafu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mzee Ali Hassan Mwinyi aliwapongeza Wananchi wa Kijiji cha Ghana kwa kupata jengo jipya la Chama.

Mzee Mwinyi alisema Kijiji cha Ghana kina Historia kubwa ya uhusiano wa watu wote waliokuwa wakishirikiana Barani Afrika kudai Uhuru wao kutokana na madhila ya wakoloni.

Alisema Kijiji cha Ghana kimeleta mchango mkubwa katika upatikanaji wa Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 ambapo Mikutano mingi ya kupanga njia za kudai Uhuru iliyoongozwa na Rais wa Kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Karume ilifanywa kwenye Kijiji hicho.

“ Bwana Abeid Karudi Ghana Kavaa Pakacha Mchana. Ni ubeti wa Shairi ya moja kati ya nyimbo za wakati wa kudai uhuru lilioimbwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa Kusini Unguja Nd. Ramdhan Abdullah Ali kwenye ghafla hiyo “. Lengo la kuimba kwake shairi hilo ni kukikumbusha kizazi kipya juhudi zilizochukuliwa na wazazi wao wakati wa kudai uhuru wa Visiwa hivi.

Ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Chama cha Mapinduzi Tawi la Ghana Jimbo la Uzini uliosimamiwa na Mwakilishi wa Jimbo hilo umegharimu jumla ya shilingi za Kitanzania Milioni 45,000,000/-.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top