Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Serikal ya Mapinduzi ya Zanzibar ina nia ya kutaka kujenga Wodi maalum kwa ajili ya kulazwa watoto wadogo wanaopatwa na majanga mbali mbali ya kuunguwa kwa moto.

Balozi seif alisema hayo wakati alipofanya ziara fupi ya kukagua watoto walioungua moto ambao wamelazwa katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Mjini Zanzibar mara baada ya kumalizika kwa kilele cha maadhimisho ya kutimia miaka 51 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaelewa vizuri matatizo yanayowakumba watoto wanaopatwa na majanga hayo ya moto ambao hulazimika kulazwa zaidi ya mtoto mmoja kwenye kitanda kimoja.

Balozi Seif alisema hali hiyo mbali ya kwamba haipendezi kuonekana lakini pia inaweza kusababisha maambukizi ya maradhi mbali mbali kwa watoto wanaolazwa pamoja.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwataka wazazi na walezi kuwa waangalifu na matukio ya majanga ya moto ambayo huonekana kushamiri zaidi katika baadhi ya vipindi na kusababisha vifo na hata vilema kwa watoto wao.

Mapema Muuguzi wa Zamu wa Wodi ya Watoto katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Bibi Mary Jadi alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba ajali za moto zinazowakumba watoto katika maeneo mbali mbali hapa nchini zimekuwa zikiongezeka siku hadi siku.

Bibi Mary alisema ipo haja ya kufanywa kwa utafiti wa kina kuelewa sababu zinazopelekea kuongezeka kwa majanga hayo na juhudi zifanywe kwa makusudi ili kupunguza au kuondosha kabisa tatizo hilo ambalo huonekana kushamiri zaidi katika kipindi cha mfungo wa mwezi mtukufu wa ramadhani.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top