Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ametoa wito kwa Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko Zanzibar kuanzisha eneo maalum kwa maonyesho ya biashara kwa lengo la kutanua zaidi uhusiano wa kibiashara kati ya Zanzibar na Mataifa mengine Duniani.

Alisema maonyesho ya Kibiashara siyo tu yanavutia na kushawishi wawekezaji lakini pia huongeza ushirikiano karibu baina ya wafanyabiashara wenyewe kwa wenyewe .

Balozi Seif alitoa wito huo wakati akilifungua tamasha la Pili la Biashara la mwaka 2015 la maadhimisho ya kutimia miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar linalofanyika katika uwanja wa mishezo wa Maisara Mjini Zanzibar.

Alisema lengo kuu la Tamasha la biashara Zanzibar ni kushajiisha ukuaji wa biashara kwa azma ya kuirejeshea Zanzibar hadhi yake ya kuwa kituo cha biashara katika mwambao wa Afrika Mashariki kwa karne kadhaa zilizopita.

Balozi Seif alifahamisha kwamba uwepo wa matamasha kama haya Zanzibar hutoa fursa kwa wageni kujipangia muda wa kutembelea Zanzibar kwa mapumziko pamoja na kujipatia mahitaji yao ya bidhaa tofauti zinazozalishwa ndani na hata kwa zile Taasisi za nje zinazoshiriki maonyesho hayo.

Alisema wafanyabiashara pamoja na wajasiri amali wanapaswa kuitumia vyema fursa hiyo adhimu ya tamasha la biashara ili wakuze biashara zao kwa vile ni moja kati ya sekta muhimu ya kukuza uchumi na kutoa ajira kwa wananchi walio wengi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali itaendelea kushirikiana na wafanyabiashara wa pande zote mbili za Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Afrika Mashariki katika kuhakikisha sekta ya biashara inazidi kukua sambamba na matamasha ya biashara ili kuongeza idadi ya wageni.

Balozi Seif alisisitiza umuhimu wa matamasha kama haya ya biashara kujumuishwa pia maonyesho ya utamaduni wa Mzanzibari kama kazi za sanaa ya mkononi, vyakula vya mwambao wa pwani ya Afrika Mashariki na Muziki ambao unaonekana kutoweka katika Historia kutokana na mabadiliko ya utandawazi.

Aliwaomba wafanyabiashara kuziepuka bidhaa zilizo chini ya kiwango kwani kufanya hivyo kutamfanya mnunuzi wa bidhaa zao kupoteza fedha bure pamoja na kuharibiwa mipango yake.

Balozi Seif alieleza kwamba Serikali imeanzisha Taasisi inayosimamia viwango kwa lengo la kukuza ubora wa bidhaa zinazozalishwa pamoja na zile zinazoagiziwa nje ya nchi masuala ambayo yanakwenda sambamba na mikakati ya kuwasaidia wjasiri amali wa Zanzibar katika kufikia viwango vinavyokubalika katika masoko ya Kimataifa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameipongeza Wizara ya Biashara Zanzibar kwa kushirikiana na mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania { Tantrade } pamoja na Jumuiya ya Wafanyabiashara Zanzibar kwa wazo lao la pamoja la kuanzisha na kuendeleza Tamasha la Biashara hapa Zanzibar.

“ Na hili ni tamasha la Pili huku tukisherehekea miaka 51 ya Mapinduzi ya Januari mwaka 1964 lengo likiwa kushajiisha ukuaji wa biashara kwa azma ya kuirejeshea Zanzibar hadhi yake ya kuwa kituio cha Biashara Mwambao wa Afrika Mashariki “. Alisema Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliipongeza Mamlaka ya Maendeleo ya Baisra Tanzania { Tanzania Trade Development Authority – Trade } kwa uamuzi wake wa kuisaidia Wizara ya Biashara Viwanda na Masoko Zanzibar katika taaluma ya Maonyesho na matamasha ya Baishara.

Balozi Seif aliitaka Mamlaka hiyo kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika sekta hiyo ili ifikie hatua ya kujiendesha yenyewe katika sekta hiyo muhimu ya Uchumi wa Taifa.

Aliwashukuru washiriki wa wa tamasha hili la Biashara Zanzibar kutoka ndani na nje ya Nchi, Taasisi za Umma na zile Binafsi, Mapampuni kwa kushiriki kwenye tamasha la mwaka huu na kuwaomba washiriki kwenye matamasha yanayokuwa yanaandaliwa hapa Zanzibar.

Mapema Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Zanzibar Mh. Nassor Ahmed Mazrui alisema ukuaji wa sekta ya B iashara hapa Nchini umeongeza mapato ya nchi sambamba na huduma za fedha.

Waziri Mazrui alisema Tamasha la Biashara la Mwaka huu limeshirikisha zaidi ya Makampuni 160 katika ya 200 yaliyoomba kushiriki katika Tamasha hili kutoka Tanzania Bara na wenyeji Zanzibar yakiwemo Makapumi mawili ya Kigeni.

Alifahamisha kwamba mbali ya bidhaa mbali mbali zitakazouzwa na kuonyeshwa kwenye Tamasha hilo la bishara lakini pia huduma za Michezo ya Watoto itakuwepo ili kuwapa fursa watoto watakaotembelea Tamasha hilo kupata burdani.

Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko aliwapongeza washiriki wa Tamasha la kwanza la mwaka J ana lililofanikiwa vyema kutokana na kukusanya mapato zaidi hya shilingi Milioni 220,630,150/- kutokana na bishara za papo kwa papo.

Alisema Tamasha la mwaka pia lilipokea maombi ya wateja kutoka makampuni na watu binafsi kwa ajili hya kupata huduma zenye gharama ya zaidi ya shilingi Milioni 90,000,00o/-.

Tamasha la Pili la Biashara la mwaka 2015 la maadhimisho ya kutimia miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar limeanza Tarehe 7 Januari mwaka huu wa 2015 na kuendelea hadi Tarahe 13 Mwezi huu.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top