Na Mwandishi Wetu, Kibaha
Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM Ndg. Nape Nnauye amewaibukia tena wasaka urais ndani ya CCM na kudai kuwa Chama hicho hakitatoa mwanya kwa wanaosaka uteuzi huo kwa kununua wajumbe mbalimbali wa vikao husika.

Nape ameyasema hayo jana kwenye mafunzo kwa wachungaji wote wa huduma ya Efatha nchini yaliyofanyika Kibaha mkoani Pwani. Nape alikuwa akitoa mada inayohusu nafasi ya CCM na uhusiano wa CCM katika jamii.

Pamoja na Nape ambaye aliwakilisha CCM kwenye mafunzo hayo walikuwepo watoa mada wengine kutoka vyama vingine vya upinzani nchini.

Akizungumzia mada ya nafasi na uhusiano wa CCM ndani ya jamii, Nape alisema historia ya Chama hicho ambayo haiwezi kwa vyovyote kufanana na ya chama chochote kilichopo au kijacho nchini ni moja ya sababu kubwa ya Watanzania kuendelea kukiamini Chama hicho. Aliongeza kuwa sababu kubwa ya pili ni misingi ambayo Chama hicho kinaiamini ambayo ndio imelifanya taifa la Tanzania kuwa taifa.

Nape alisema CCM ipo kila kona ya nchi na hivyo inamtandao mkubwa kuliko taasisi yeyote nchini, na hiyo ndio moja ya siri za uimara wa CCM.

Akizungumzia swala la maadili Nape alidai kuwa CCM ndio chama duniani chenye nyaraka nyingi na bora zinazozungumzia maadili ya viongozi. Pamoja na nyaraka hizo alisema mfumo wa uchujaji majina hasa kwa nafasi ya urais kupitia CCM hautoi nafasi kwa mgombea yeyote wa nafasi hiyo kupita kwa kununua uteuzi huo.

Alisema Nape kuwa wasaka urais wanaohangaika kutoa pesa zao kujaribu kununua uteuzi wa CCM wanapoteza muda na pesa zao kwani Chama hicho hakitawateua kugombea nafasi hiyo.

Nape akatumia nafasi hiyo kuwaomba wachungaji hao kukiombea Chama hicho na viongozi wake wawe na ujasiri wa kulisimamia hilo kwani kupitisha wagombea walionunua uteuzi huo ni kukaribisha laana kwa nchi.

" Nawahakikishia kuwa hakuna mnunua urais atakayepenya mchujo ndani ya CCM. Kuruhusu mtu wa namna hiyo kupenya ni kuleta laana kwa nchi yetu,hivyo viongozi wa dini tuombeeni tuwe na ujasiri wa kutosha kukataa laana hii" alisisitiza Nape.

Nape alisema mwanzoni mwa mwaka huu wa 2015 Katibu Mkuu wa CCM Ndg. Kinana akitoa salaam za mwaka mpya za CCM mjini Tanga, aliwaambia Watanzania kuwa CCM imekuwa ikisimamia maadili kwa miaka yote lakini mwaka huu itaongeza ukali ili kuhakikisha nchi inapata viongozi waadilifu watakaoisaidia nchi kupiga hatua zaidi.

Anasema Nape hakuna atakayeingia madarakani kwa rushwa atakayeunda serikali itakayokusanya kodi. Bila kukusanya kodi hakuna namna nchi itapiga hatua ya maendeleo na huduma za kijamii zitadumaa na hivyo kusababisha maisha magumu na hiyo itakuwa laana kwa nchi.

0 comments:

 
Top