Wananchi wameombwa kuendelea na harakati zao za kujitafutia maendeleo baada ya kumalizika kwa bunge Malum la Katiba hivi karibuni na kuachana porojo zinazopigwa na baadhi ya watu ambazo zinaweza kuviza maelekeo wao.

Ombi hilo limetolewa na Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi wakati akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Mvuleni Kidoti kiliopo Wilaya ya Kaskazini “ A “, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Mama Asha ambae alikuwa akikabidhi fedha taslimu,vifaa mbali mbali pamoja na vyarahani kwa Vikundi sita vya Ushirika vya akina mama wa Kijiji hicho kutekeleza ahadi aliyowapa hivi karibuni alisema baadhi ya watu hao wakorofi wamezoea kuwatumia wananchi kwa kukamilisha matakwa yao binafsi.

Alisema wakorofi hao ambao wapo nje na ndani ya nchi kwa kipindi kirefu sasa wengine wakiwemo miongoni mwa wananchi hao wamefikia hatua ya kutia fitina kwa nchi na mashirika hisani ili Zanzibar izuiliwe misaada wakisahau kwamba wanaoumia ni wananchi wanyonge.

Hata hivyo Mama Asha alieleza kwamba kutokana na umahiri wa Viongozi wa Chama cha Mapinduzi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar awamu zilizopita walifanikiwa kuvuka vikwazo na njama hizo mbaya.

Aliwakumbusha wananchi hao kwamba awamu ya Tano ya Rais Mstaafu wa Zanzibar Dr. Salmin Amour ilikumbwa na kadhia hiyo wahusika wa uchochezi wa fitina hizo walikuwa ni wale wale wanaoendelea kupotosha Wananchi ambapo hivi sasa wameshika bango dhidi ya katiba iliyopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba.

“ Tulikuwa mashahidi wa vitendo vya wafitini hawa waliochochea mpaka Zanzibar ikasusiwa na kunyimwa misaada na mashirika ya maendeleo Duniani zikiwemo hata chanjo za watoto wasio na hatia ambao ni malaika wa mungu“. Alisema Mama Asha.

Mapema Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Kaskazini Unguja Bibi Caterina Pitadau alikemea tabia ya baadhi ya wanasiasa ya kukebehi mambo yanayofanywa na wanasiasa wenzao waliojitolea kuwatumikia Wananchi.

Bibi Caterina alisema tabia hii mbaya ya wanasiasa wasio na muelekeo wa maendeleo kamwe haitaweza kukidhi mahitaji ya Kimaendeleo ya wananchi wanaowaongoza katika maeneo yao.

Katika Mkutano huo Mke huyo wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alikabidhi Vyarahani, fedha Taslim, Majora ya Vitambaa, Kanga pamoja na vifaa vya ushoni kwa Vikundi sita vya akina mama wa Kijiji cha Mvuleni vikiwa na thamani ya shilingi za Kitanzania Milioni Nne na Laki Mbili { 4,200,000/- }.

Vikundi hivyo vya ushirika vya akinamama hao ni pamoja na Tusaidie waja wako, Ushirika wa Chumvi,Hatuyumbishwi, Mshikamano, Mola Tubariki pamoja na Tusiwe nyuma.

Mapema Mama Asha alipata fursa ya kuukagua msikiti wa Ijumaa wa Kijiji cha Mvuleni ambao uko katika hatua za mwisho kukamilika kwake baada ya kufanyiwa matengenezo makubwa.

Matengenezo hayo yanaendelea kufanywa kupitia mchango wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofanya ziara katika Kijiji hicho miezi michzche iliyopita na kushawishika kuunga mkono wazo la waumini wa Kijji hicho la kutaka kuupanua zaidi ili uweze kutoa huduma kwa upana zaidi.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top